Mwanamuziki Snura Mushi ametangaza kuacha muziki huku akikataza nyimbo zake zisichezwe kwenye vyombo vya habari na sehemu nyingine, Hatua hiyo imekuja baada msanii huyo kudai kuwa kwa sasa ameamya kumrudia Mungu wake.

“Watanzania na nje ya nchi mimi Snura leo natangaza rasmi kuwa nimeacha kazi za sanaa nilizokuwa nazifanya. Sababu kubwa ya kuacha ni kumrudia muumba wangu, nifuate dini yangu ya Kiislamu inavyosema na mwanamke wa Kiislamu anavyotakiwa kuwa,” amesema Snura kwenye mkutano na waandishi wa habari.

Mbali na hilo, msanii huyo amesema anajutia aliyokuwa akiyafanya kipindi akiwa kwenye sanaa.

“Nisiwe muongo najutia sana niliyoyafanya na maamuzi yangu ya kuacha sanaa niliyafanya miaka mingi iliyopita, mwanzoni wazo langu lilikuwa kuacha kimyakimya nisiseme kwa yeyote wala popote ijue tu familia yangu, ndugu zangu na watu wanaonizunguka lakini kwa sababu hivi vitu vinaishi miaka na miaka na vizazi vipya vinakuja sitaki kuwa sababu ya kuwaharibu,” amesema.

Katika hatua hiyo ya kutangaza kuacha muziki pia ameomba nyimbo zake kuacha kuchezwa kwenye vyombo vya habari.

“Nisingeweza kupita kila redio na Tv kuwakataza wasicheze nyimbo zangu, natumia fursa hii ndugu zangu kwa heshima na taadhima naomba sana mnipokelee ombi langu msicheze kazi zangu kabisa naomba mfute, fanyeni kama hakuna kilichotokea,” amesema Snura.

Snura pia ameomba siku atakayofariki picha zake zisichapishwe kwenye mitandao ya kijamii.

“Ukisikia nimekufa umehuzunishwa na msiba wangu njoo unizike kama ni mwanamke usije mtupu njoo na stara, picha ambazo hazina heshima msiposti hayo mapicha wala madude dude kwa sababu naona tukifa hayo madude ndiyo mnaposti,” amesema.

Baadhi ya ngoma alizowahi kutamba nazo Snura kabla ya kutangaza kuacha muziki ni ‘Majanga’, ‘Nimevurugwa’, ‘Chura’, ‘Shoga Yake Mama’, ‘Ushaharibu’ na ‘Shindu’.

Please follow and like us:
Pin Share