Wiki iliyopita nilipokea ujumbe mfupi kwa njia ya simu kutoka kwa Rose (si jina lake halisi), mmoja wa wasomaji wangu wa safu hii ukisema hivi:

“Samahani daktari, mwaka mmoja uliopita nilipimwa na kugundulika kuwa nina uvimbe kwenye ovari ya kushoto. Baadaye nikapata ujauzito ambao kwa bahati mbaya uliharibika ukiwa na miezi minne.

“Kuanzia wakati huo baada ya mimba kuharibika nimekuwa nikipatwa na maumivu makali ya kiuno yasiyokoma. Nimejaribu kutafuta msaada wa matibabu kwa kuwaona madaktari na kupatiwa vipimo mbalimbali lakini bado hakijaeleweka chochote na ninaendelea kuwa na maumivu makali ya kiuno, hali hii inaniogopesha sana na ni mbaya zaidi.

“Sasa hivi maumivu haya nayapata hata wakati wa kushiriki tendo la ndoa na ninaendelea kuyapata hata baada ya kumaliza tendo la ndoa.” Kutokana na ukweli kwamba madaktari bado hawajagundua hasa nini tatizo, hii haiwezi kuwa dalili moja wapo ya saratani?” Rose alimaliza kwa kuuliza.

Kama ilivyo kwa Rose, ninaelewa kuwa wanawake wengi wanasumbuliwa na matatizo ya maumivu ya kiuno na maumivu wakati wa kushiriki tendo la ndoa yanayodumu kwa muda mrefu.

Ile dhana ya kuwa maumivu makali ya kiuno ni moja ya dalili za magonjwa ya saratani kwa wanawake ipo kwa wanawake wengi, huenda ni kutokana na kuongezeka kwa hofu, lakini pia kukosa uelewa wa kutosha juu ya magonjwa ya saratani.

Wakati wote tunapozungumzia kuhusu maradhi ya saratani, hasa zile aina za saratani zinazowashambulia wanawake, tunaona kuwa maumivu ya kiuno na mgongo yanayodumu kwa muda mrefu kama ni moja ya dalili kuu; ni kweli!

Ni vema ikafahamika kwamba kuna sababu nyingine nyingi zinazoweza kusababisha maumivu ya kiuno na mgongo na maumivu wakati wa kushiriki tendo la ndoa, tofauti na maradhi ya saratani; japo umakini unahitajika.

Je, ni nini kinasababisha hali hii?

Kwa mwanamke, matatizo mbalimbali ya kiafya kama vile maambukizi ya kwenye njia ya mkojo, hasa maambukizi haya yakiwa sugu, kuna uwepo wa uvimbe mbalimbali, aidha kwenye mfuko wa uzazi au kwenye mayai na sehemu nyingine kwenye mfumo wa uzazi.

Maambukizi kwenye mfumo wa uzazi (PID) na baadhi ya sababu nyingi za kisaikolojia, yanachangia kwa kiasi kikubwa sana mwanamke kupatwa na maumivu ya kiuno na maumivu wakati wa kushiriki tendo la ndoa.

Mwanamke anaweza kuwa na tatizo moja kati ya haya au hata zaidi na kumsababishia hali hii.

Matatizo haya kwa pamoja huwa na dalili zinazofanana, hivyo ni vigumu sana kwa mwanamke kutambua chanzo hasa cha maumivu anayoyapitia.

Iwapo maumivu haya yamedumu kwa muda wa zaidi wa miezi sita, ni dhahiri mwanamke anahitaji huduma ya vipimo na msaada wa kitabibu.

Hivyo, mwanamke anashauriwa wakati wote kuzifuatilia kwa karibu dalili mbalimbali zinazoashiria hali ya utofauti kwenye afya yake, hasa kwenye mfumo wa uzazi na kupata ushauri wa daktari.