Na Lookman Miraji, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Mwanamitindo wa Kimataifa wa Tanzania Mellen Magese ametangazwa kuwa jaji mkuu wa Tamasha la Samia Fashion Festival litakalofanyika Novemba 30 mwaka huu visiwani Zanzibar.

Akizungumza mara baada ya kutangazwa kuwa Jaji Mkuu wa Tamasha hilo , Millen Magese amesema kuwa ni heshima kubwa na furaha kwake kusimama kama Jaji Mkuu wa Samia wa Fashion Festival na kwamba anajivunia kushuhudia wakati huu wa kihistoria ambao unasherehekea ubunifu, stara, na urithi wa kipekee wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

“Kwa zaidi ya miaka ishirini, nimejitolea maisha yangu katika sekta ya mitindo, urembo, Nimezunguka duniani, nikifanya kazi na chapa kubwa na maarufu, nimeona jinsi mitindo inavyothaminiwa katika nchi za ulaya na mataifa mengine, si tu kama sanaa bali kama alama ya utambulisho, urithi, na fahari.

“Niliposikia kuhusu mpango huu wa kipekee, sikusita, nilichukua ndege haraka kuja nyumbani kuwa sehemu ya safari hii ya kihistoria, kwa tamasha hili si tu kuhusu mavazi; ni kuhusu heshima yetu kama watanzania,”alisema.

Mwanamitindo huyo ambaye kwasasa anaishi nchini Marekani alisema kuwa uandaaji wa vazi la Samia ni alama ya stara, uongozi, na heshima kwani ni zaidi ya vazi ya kawaida.

Alieleza ilikuwa ni ndoto yake ya siku nyingi kuona vazi la Samia linakuwa ishara ya kitaifa na kimataifa, chanzo cha fahari kinachowakilisha uzuri, nguvu, na umoja wa Tanzania.

“Tukubaliane kufanya kitu cha kipekee, kitu kitakachotupeleka ulimwenguni na kuacha alama katika historia. Kwa wabunifu, wanamitindo, na wote wanaoshiriki, tambueni kuwa hampo tu katika sehemu ya tamasha, bali mnakuwa sehemu ya historia ya kizazi kitakachovutia dunia. Hebu tufanye wakati huu uwe wa kukumbukwa milele.”

Pia ametoa rai kwa watanzania kuendelea kuunga mkono juhudi za Rais , Dkt: Samia Suluhu Hassan ambaye kwa kushirikiana na wizara ya utamaduni, sanaa na michezo wameendelea kusimama imara kuhakikisha sekta ya utamaduni katika tasnia ya mitindo na urembo inapewa nafasi kubwa katika taifa.

Aidha kwa upande mwingine akizungumza kuhusiana na tamasha hilo la mitindo la Samia Fashion Festival muasisi na mwandaaji wa tamasha hilo, Khadija Mwanamboka alisema kuwa amewashirikisha wanamitindo mbalimbali na kuungana nao katika tamasha hilo ili kusaidia watoto wanaoishi na virusi vya UKIMWI na Saratani.

Mwigizaji maarufu nchini İdris Sultan alisema anajisikia furaha kuwa sehemu ya walioshirikishwa katika eneo la majaji na kueleza umefika wakati kwa watanzania kutoa nafasi kwa wanawake wenye uwezo ukiwemo uongozi na kusisitiza Rais Samia amekuwa mfano mzuri na wa kuigwa .

Orodha ya majaji wengine watakaosimamia tamasha hilo ni Jokate Mwegelo ,Martin Kadinda, Faraja Nyalandu, pamoja nae Nancy Sumari .

Tamasha hilo la mitindo la Samia linatarajiwa kufanyika wikiendi hii ya Novemba 30 ,2024 visiwani Zanzibar.