Askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) aliyekuwa katika ulinzi wa amani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) amefariki dunia nchini Uganda alimokuwa akipatiwa matibabu.
Askari huyo ni miongoni mwa askari 44 wa Tanzania waliojeruhiwa katika shambulio lililotekelezwa na waasi wa The Allied Democratic Forces (ADF) katika kambi ya walinzi wa amani wa Umoja wa Mataifa (MONUSCO). Shambulio hilo lilitekelezwa Disemba 7 mwaka huu na kupelekea vifo vya wanajeshi 14 wa Tanzania na 5 wa DRC.
Stephane Dujarric, Msemaji wa Katibu wa Umoja wa Mataifa alitangaza taarifa hiyo ya kusikitisha katika Makao Makuu wa UN, Mjini New York jana usiku.
Katika taarifa iliyotolewa na MONUSCO leo, imeeleza kwamba mwanajeshi wa 15 wa Tanzania amefariki dunia akipatiwa matibabu mjini Kampala.
Umoja wa Mataifa umetuma salamu za pole kwa wanajeshi, familia, ndugu, jamaa na marafiki pamoja na serikali ya Tanzania kutokana na msiba huo.