Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam

MWANAFUNZI kutoka Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), George Luambano amebuni mashine itakayosaidia kulea vifaranga viweze kukua vizuri.

Akizungumza na waandishi wa habari katika banda lao lililopo kwenye Maonesho ya Kitaifa ya Wakulima na Wafugaji (Nanenane) yanayoendelea katika Viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma, Mbunifu wa Mashine hiyo ambaye ni Mwanafunzi wa mwaka wa Nne katika chuo hicho, amesema mfumo huo utamsaidia mfugaji kulea vifaranga katika kipindi ambacho wanahitaji chanjo na matunzo mengine muhimu ili kuhakikisha vinakuwa na afya njema.

“Mimi ni mfugaji, kwahiyo baada ya kuona napata hasara ndipo nikapata wazo la kubuni mashine hii ambayo naamini itanisaidia mimi pamoja na Wafugaji wengine.

“Mashine hii inasaidia kulisha Kuku, kuwapa maji kwa muda maalumu pamoja na kuwapa joto. Pia inaweza kutoa taarifa pale ambapo maji au chakula vinakuwa vimepungua,” amesema Luambano ambaye ni Mwanafunzi wa fani ya Uhandisi wa Mitambo.

Amefafanua kuwa, mashine hiyo inatumia taa za joto na hata likipungua zinaendelea kuwaka na ikifika linalohitajika kwa kuku (nyuzi 33) taa zitazima na kuku ataendelea kukua na kwamba ina feni ambayo inaingiza hewa ndani.

Naye, Ofisa Uhusiano Mkuu wa NIT, Tulizo Chusi, amesema Chuo hicho kina kitengo cha kuendeleza bunifu zinazobuniwa na wanafunzi pamoja na wataalam mbalimbali.

“Tunafanya hivi ili kuhakikisha kwamba bunifu haziishii chuoni bali zinaifikia jamii hasa kwa wakulima na wafugaji. Hata hivyo Chuo kina kampuni ambayo inafanya kazi ya kuendeleza bunifu za vijana hawa na kuziingiza sokoni na tayari kuna bunifu zimesajiliwa na Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech) kwa ajili ya kwenda kwa walaji,” amesisisitiza.