Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Mbeya
MWALIMU wa Shule ya Msingi Mbugani Wilayani Chunya aitwaye,Herieth Lupembe (37) na mwanafunzi wa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari Isenyela, Ivin Tatizo (15) wameuwawa na vitu butu kichwani wakiwa nyumbani kwao Kijiji cha Kiwanja wilayani hapa.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo Kamanda wa Polisi mkoani Mbeya, Benjamin Kuzaga amesema kuwa tukio limetokea Machi 31, 2024 majira ya saa 2:30 usiku wakati marehemu akiwa nyumbani kwake sebuleni.
Kamanda Kuzaga amesema kuwa katika nyumba hiyo alikuwepo marehemu na watoto wawili ambao ni Ivon Tatizo na Haris Barnaba Mtweve [06] Mwanafunzi wa darasa la kwanza katika Shule ya Msingi Ken Gold aliyejeruhiwa kwa kupigwa kitu butu kichwani.
Aidha Kuzaga amesema uchunguzi wa awali umebaini kuwa, mtu huyo aliwavamia marehemu na kuanza kuwashambulia na baada ya kufanya hivyo alifunga milango kwa nje na kuondoka na funguo.
Chanzo cha tukio hili bado kinachunguzwa na majeruhi mtoto Haris Mtweve anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linaendelea na uchunguzi wa tukio hili ikiwa ni pamoja na msako dhidi ya mtu au watu waliohusika. Aidha, linatoa wito kwa mtu yeyote mwenye taarifa za mtu au watu waliohusika katika tukio hili kutoa taarifa ili wakamatwe.