Taifa letu kwa sasa linapita kwenye misukosuko ya udini, ukabila, ukanda na utegemezi. Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, hakusita kamwe kukemea kwa nguvu zote utengano huo, na kusisitiza nchi kujitegemea.
Akihutubia kwenye kilele cha Sherehe za Mei Mosi , 1995 mjini Mbeya, Mwalimu alizungumzia mambo hayo. Ifuatayo ni sehemu ya hotuba hiyo ambayo tunaamini ni dira ya kujenga umoja, mshikamano na maendeleo ya usawa kwa Watanzania.
Hatukuwa wamoja
Hii ni nchi mpya na ndiyo ambayo tumekuwa tunajaribu kuijenga. Kwanza Tanganyika, kwa muda mfupi na, halafu, Tanzania . Kusema kweli, sisi wengine maisha yetu ya urais wetu ni wa nchi inayoitwa Tanzania .
Nilipokuwa rais wenu, ni1ifanya juhudi za kukomboa eneo hili linaloitwa Tanganyika . Lakini, uongozi wangu niliowaongoza ninyi katika nchi huru inayojitawala na raia duniani wa nchi huru inayojitawala. Niliwaongozeni katika nchi inayoitwa Tanzania . Tanganyika niliwaongozeni kwa muda mfupi tu; tangu Disemba 1962 mpaka Aprili 1964 basi. Kipindi changu kingine chote, niliongoza nchi inayoitwa Tanzania , siyo Tanganyika . Kwa kweli, siijui Tanganyika ya watu huru. Ni muda mfupi mno.
Nchi hii Tanganyika , ni nchi changa. Watu wake waliwekwa katika sehemu inayoitwa moja na Wajerumani. Wamakonde na Wazanaki hawakuwa wamoja. Waliwekwa pamoja na Wajerumani ili watawaliwe. Jitihada ya kuwafanya wawe pamoja na kuanza kusema “Ninyi ni Wamoja” haikufanywa na Wajerumani. Hakuna Wajerumani arnbao wangeweza kusema “Ninyi ni Wamoja” kwa kuwa lengo lao halikuwa kujenga umoja. Wajerumani walichoweza kuserna ni kwamba “Ninyi ni Tofauti, Ninyi ni Tofauti!” ili waendelee kututawala.
Jitihada ya kwanza ya dhati ya kusema “Ninyi ni Wamoja” ilikuwa ni yetu sisi tulipoanzisha chama cha TANU. Shabaha yake kubwa ilikuwa ni kujaribu kujenga umoja ili tuwatimue Waingereza. Lakini mbinu yake ya kwanza kabisa iliyotajwa ilikuwa ni kufuta ukabila. “Sahau Ukabila!” tulitamka kwa ukali. Wale ambao, labda mpaka leo, wanako kakitabu ka milango ya historia ka Katiba ya TANU wataona tumeshambulia kitu ukabila. Tukaanza hatua ya kwanza kabisa, kusema “Sisi ni Taifa”. Lakini halikuwa likiitwa taifa la Tanganyika.
Tujenge misingi ya umoja ili tuelewane na tujuane kuwa ni wamoja na ni ndugu
Nataka kusisitiza nini: Kwamba sisi ni taifa changa miongoni mwa mataifa machanga. Taifa hili halijajenga mizizi mirefu ya kuwa taifa huru kuwakaribia Waingereza. Waingereza wana miaka mingapi? Sijui, labda elfu na zaidi.
Katika mataifa machanga duniani, moja ni Marekani. Lakini, Marekani wana miaka mia mbili na zaidi ya kuwa taifa. Vitaifa vingi vya Ulaya vina miaka mingi tu! Mataifa machanga haya lazima yajenge misingi inayowafanya raia wake wajiite sisi.
Tumejitahidi na ndivyo jitihada zetu zilivyokuwa. Lakini ukijenga nchi moja, unajenga misingi ya umoja ili tuelewane na tujuane kwamba sisi ni wamoja, ni ndugu. Kama tunahangaika kufanya kazi hapa, tunahangaika kwa pamoja. Kama tunahangaikia ulinzi, tunalinda nchi yetu kwa maslahi yetu pamoja.
Tunaulizana “nini mahitaji yenu?” Tunajitahidi wote, tunayapata. Kama tunataka elimu, tunasaidiana wote tupate elimu. Siyo tuseme kwamba wengine wapate elimu wengine wasipate. Kama tunataka afya, tunataka kujitahidi wote tuweze kutafuta njia kusudi wote wote tupate afya, wote tuwe na afya. Siyo wengine wapate afya wengine wasipate. Kama tunataka nyumba nzuri, wote tujitahidi kwa pamoja tuone kwamba tunajenga mazingira wezesha yatakayohakikisha kuwa kila Mtanzania atakuwa na nyumba nzuri kwa pamoja. Hapo ndipo tunaweza kushirikiana tujenge nchi pamoja.
Azimio la Arusha na Siasa ya TANU ya Ujamaa na Kujitegemea
Tukaweka kitu kimoja hapa kinaitwa Azimio la Arusha. Leo narudia kusoma Azimio la Arusha hata kama hamlitaki. Kama kuna watu Tanzania hawajali, wachukue waanze kulisoma ili waone na waniambie wanachokiona mle kibaya ni nini hasa. Asome tu kwa dhati tu na kisha aseme hiki ni kibaya.
Siasa va Ujamaa
Linasema Azimio la Arusha, kwa msingi kabisa, kwamba “Nchi yetu ni ya Wakulima na Wafañyakazi”. Sasa mnasemaje? Imeacha kuwa ni nchi ya Wakulima na Wafanyakazi? Kwa hiyo, kama tunaijenga nchi hii, tunaijenga kwa faida ya Wakulima na Wafanyakazi. Ndivyo Azimio la Arusha linavyosema. Ukweli huo umekwisha? Umefutika? Umefutwa na nani? Nini kimefuta ukweli huo kwamba nchi hii ni ya Wakulima na Wafanyakazi? Ninyi hapa ni Wakulima na Wafanyakazi. Mtaona wafanyabiashara wadogo wadogo, siku hizi wengine wanaitwa Wamachinga. Lakini, hasa hasa, nchi hii bado ni nchi ya Wakulima na Wafanyakazi. Kama tutafanya jitihada za kuijenga nchi hii, tutajenga uchumi wake na huduma zake za umma ambazo lazima ziwafae Wakulima na Wafanyakazi. Hali hiyo imebadilika lini?
Siasa va Kujitegemea
Tukasema kwamba “Hatuna budi kujenga nchi hii kwa kujitegemea”. Hatuwezi kuwa tunataka maslahi yetu ya Watanzania ya afya bora, maisha bora na elimu nzuri lakini eti tudhani tunaye mjomba huko nje atakuja kutuletea maslahi hayo. HATUNA! Tutajenga nchi hii kwa faida yetu wenyewe sisi wenyewe. Akipatikana mtu kutusaidia, tutamshukuru. Lakini kazi ya kujenga nchi hii kwa manufaa ya Watanzania wote ni kazi ya Watanzania, si kazi ya mtu mwingine. Msimamo huo tukauita Siasa ya Kujitegemea.
Msingi huo umekufa. Hivi mmeshapata mjomba? Hivi kweli mtawadanganya Wafanyakazi hawa msiwambie “chapeni kazi kama mnataka maslahi yenu yaboreshwe, tuchape kazi kwa faida yetu!” Tuache kuwambia wakulima kwamba “ kama tunataka maendeleo, tuchape kazi hivyo hivyo”.
Hivi mtawambia hawa kwamba “tumeshapata mjomba msiwe na wasiwasi!” Mjomba huyo ni nani? Mimi nitafurahi kumwona. Nitakwenda kumwona, lakini sitamwuliza lo lote. Nitafurahi kumwona. Halafu mkinionyesha, “ndiye huyu mjomba”, nitacheeka! Hali ya nchi hii haijabadilika hata kidogo. Tunaweza kujenga nchi kwa maslahi ya Watanzania kwa siasa ya kujitegemea tu, lakini kwa manufaa ya wote.
Manufaa ya wote ndicho tulichokiita ujamaa.
Nchi ya Kijamaa
“Nchi ya Ujamaa”, tukasema, “ni nchi ambako kila mtu anafanya kazi. Kama ni mkulima, anafanya kazi; kama ni mfanyakazi, anafanya kazi”. Lililokuwa la msingi na linalotawala ni mfanyakazi: maslahi yanatokana na kazi yake na jasho lake. Watu ambao hawana ulazima, kimsingi ya kupata maslahi yao kutokana na jasho lao wenyewe wapo. Watoto wadogo hawana jukumu hilo . Eti chakula chao kitokane na nguvu zao wenyewe? Hao ni wanyonyaji wa haki sawa kwani wanawanyonya mama zao. Ni haki yao .
Lakini zee na madevu yake hatulitazamii limnyonye mama yake. Watoto wadogo tu wanayo haki hiyo. Vile vile, kuna watu ambao hawana uwezo wowote ule wa kujifanyia kazi- sio uwezo wa kutokuwa na kazi! Wako watu hawawezi. Wana vilema fulani ambao hawawezi kufanya kazi wajipatie riziki kwa kazi na kwa nguvu zao wenyewe. Hawa wana haki ya kulishwa na kutunzwa na umma pamoja na jumuiya zote. Hali kadhalika, wako watu wazima ambao wamefanya kazi zao. Walipofika umri wao wa kushindwa, hawawezi kufanya kazi tena. Ah, basi tena. Hawajiwezi hawa, tuwatunze. Hawa ni haki kuwatunza. Wamo watu wa aina hiyo wanajulikana kila mahala.
Nchi ya Kibepari
Hata hivyo, mbali ya makundi hayo, wapo watu wengine ambao wanapata riziki yao kwa kufanya kazi na wengine wanapata riziki yao kwa kafanyiwa kazi. Nasema nchi ya namna hiyo inaitwa ya kibepari. Nchi inakubali wengine wafanye kazi na kupata riziki yao kwa jasho kama inavyosema misahafu, wengine wanafanyakazi kwa kunyonya kama watoto wadogo kama vile vilema na vizee. Ni majitu yanakaa na uwezo wao yanatumia wengine kama vyombo. Kwa hiyo, mfanyakazi na randa ni sawa sawa. Nasema nchi ya namna hiyo inaitwa ni nchi ya kibepari.
Sasa katika dunia ya siku hizi maneno hayo si inazuri sana kuyasema. Na mimi nawakumbusheni tu na wala sijayasema! Mimi sina taabu, nawakumbusheni tu. Hill Azimio la Arusha, ambalo sasa mnalitemea mate, lilikuwa linasema hivyo na, kutokana nalo, kuna mambo fulani tukaanza kuyapata.
Baadhi ya matunda ya Azimio la Arusha
Moja ya mambo yanayopaswa kuzingatiwa ni la hali yetu mbovu ilivyokuwa kwanza wakati tunajitawala. Nchi tuliyoipokea kutoka kwa wakoloni ilikuwa ni masikini sana . Ilikuwa nyuma kabisa kwa upande wa elimu. Tulipojitawala, tulikuwa na wahandisi wawili. Kijana mmoja aliitwa Mbuya na alifariki katika miaka miwili hivi baada ya kujitawala. Tulikuwa na madaktari kumi na wawili wakati tunajitawala mwaka wa sitini na moja.