Mei Mosi, 1995 Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, akiwa mgeni rasmi kwenye Sherehe za Mei Mosi mjini Mbeya, alizungumza mambo mengi yaliyolihusu Taifa. Miongoni mwa mambo hayo ni haki ya kuwapo mgombea binafsi. Rasimu ya Katiba Mpya (ya Jaji Warioba) ilizingatia jambo hili muhimu. Hata hivyo, Bunge Maalum la Katiba (katika Rasimu ya Samuel Sitta) limeminya mno haki ya kuwapo mgombea binafsi. Ilivyo ni kama haki hiyo haipo kwani imewekewa vizingiti vizito mno. Soma maneno haya ya Mwalimu Nyerere.
Nataka kusema kauli ya mwisho kuhusu sheria ya uchaguzi ilivyo sasa hivi. Ninalo tatizo moja. Hili nataka kulisema kwa sababu nadhani ni la msingi kidogo.
Tulipokubali tuwe na vyama vingi vya siasa tulisema kwamba hivi vyama vingi vina migogoro. Mnaweza mkawa na chama cha dini, kabila, mkoa kinaitwa chama cha Mbeya ama katika nchi kikaitwa Zanzibar au Tanganyika tu. Tulisema sisi hapana ni Taifa changa. Lazima tujihadhari na chama kinachoweza kutugawa. Tunataka chama kinachokubali umoja.
Kwa hiyo, tukakataa vyama vya udini, ukabila na vya kutenganisha Tanzania. Tanzania tukaigawa, sijui inaitwa Tanganyika na Zanzibar, sijui inaitwa Tanganyika na Tanzania Zanzibar. Hapana tukatae vyama vya namna hiyo.
Kwa hiyo, tuliamua kwamba yawepo masharti ya kisheria yanayozuia vyama kuwa vya namna hiyo. Hii ni kulinda umoja ili tujenge upya kwa kuwa bado tu wachanga mno. Basi, sheria hiyo ndivyo ilivyotungwa na ndivyo ilivyo. Huwezi kuanzisha chama ambacho kinakiuka upande huo wa sheria. Hata hivyo, mimi nadhani sheria imekosea kuzuia wagombea binafsi.
Nataka nieleze sababu kwa nini nadhani kukosea huku ni kwa msingi na si kwa juu juu. Hili jambo limekosewa ni la msingi. Ndiyo maana napenda kulisema kwa nini ni la msingi. Linahusu haki yangu na yako ya kupiga kura. Hii ni haki ya uraia. Madhali wewe ni raia wa Tanzania [huna kichaa, huko gerezani, umetimiza umri unaotakiwa wa miaka kumi na minane] una haki ya kupiga kura. Ni haki yako ya uraia. Iko mfukoni mwako!
Hii haki ya kuomba upigiwe kura pia ni haki ya uraia; ni haki yako. Unaomba ubunge au chochote kile upigiwe kura na hata unaomba urais, ni haki yako ya uraia; huwezi kunyimwa maadam wewe ni raia wa Tanzania kisisasa una haki ya kuomba uwe rais.
Ukiwa katika chama ama hupo katika chama. Unayo haki inayotokana na uraia wako ya kupiga kura na ya kupigiwa kura ambayo haiwezi kudaiwa na mtu ambaye si raia wa Tanzania.
Aidha, raia wa Tanzania hawezi akanyang’anywa haki hii ya kuomba uongozi wa nchi yake tangu ngazi ya kijiji mpaka ngazi ya Taifa. Iwapo wapo wasio na uwezo huo wa kutaka kuwa rais, hiyo ni shauri nyingine. Lakini haki ninayo wakataohukumu kama nina uwezo au sina uwezo ni wananchi. Mimi sasa hivi niko hapa nawaelezeni jinsi ya kuwahukumu wenye uwezo na wasio na uwezo. Lakini sisemi hawana haki.
Haki hiyo ndiyo inayowafanya ninyi wafanyakazi, ninyi wafanyakazi mnazo haki za wafanyakazi, nikasema “lakini mmoja mmoja hatuwezi, lazima tushirikiane”. Kwa hiyo, mnashirikiana wote kwa pamoja. Hivyo ni vizuri zaidi.
Tunasema ni vizuri tuiombe na tujaribu kuitumia haki ile ya kuunda vyama. Mnaweza mkaunda vyama. Sijui wangapi wameweza kuingia katika vyama maana tunayo haki hiyo. Sasa hivi mnasema viko kumi na vitatu. Sina hakika kama vimechukua Watanzania wote. Watanzania wengine hawamo CCM, hawapo wapi na hawana chama chochote. Hata hivyo, nikikataa kuingia katika chama isiwe sababu ya kuninyang’anya haki yangu ya kupiga au kupigiwa kura. Ninayo tu na naweza nikaamua kuitumia mwenyewe tu!
Lakini, msije mkanielewa vibaya kuhusu kile ninachotaka kusema kwamba raia yeyote wa Tanzania anaweza kusema “mimi mgombea urais”. Tutamwambia: “Ah! Unaweza bwana peke yako kweli utasimama hivi kwa Tanzania peke yako utapitapita huku na kule watakupigia kura?”
Unaweza kumlaumu na kumhukumu useme: “Wewe ni mjinga”. Lakini huwezi kusema huna haki hiyo. Ni haki yake. Anaweza kuwa mjinga. Labda kuwa ni mtu anayedhani kwamba “Watanzania wakishaona uso wangu, hata kama sina kitu, watanichagua”. Anaweza kuwa si mgombea makini, lakini ni haki yake.
Sasa sheria inawanyima raia wa Tanzania haki hiyo. Mtu mmoja akaenda mahakamani kudai haki hiyo akasema “sheria hii si haki”. Jaji mmoja akahukumu akasema “naam, si haki”. Mimi nakubaliana na maamuzi yale ya Jaji kabisa. Jaji alikuwa sahihi, hata kama alihukumu vile kwa bahati, kwa sababu haki hii iko katika Katiba. Ingekuwa haiko katika Katiba, ungekuwapo ubishi, lakini imo ndani ya Katiba. Kwa hiyo, Jaji akasema: “Naam, hawawezi kumnyima haki”.
Sasa Serikali watafanyaje? Badala ya kukubali uamuzi wa Jaji, kwa kweli walichokifanya kwa kweli ni kuifuta. Ndiyo, hamwezi kufuta haki za raia. Hamna uwezo wa kufuta haki za raia. Ndugu Waziri, hamna uwezo wa kufuta haki za raia. Hamuwezi kweli kabisa kabisa.
Serikali haiwezi ikasema haki hii inakera kidogo. Inakera kisiasa tu, lakini na siyo kimaadili. Sheria hii inawakera kisiasa halafu mnaifuta, mtatunga kesho sheria nyingine itawakera, mtaifuta. MTAFUTA NGAPI?
Sasa mimi nina ugomvi huo. Na ni ugomvi wa kasoro kubwa, si kasoro ndogo. Ingekuwa kasoro ndogo, nisingejua. Hatuwezi kumnyima raia haki yake. Mimi napenda watu watumie hii haki yao ndani ya vyama. Kama vile nilivyosema, mfanyakazi unayo haki ya mshahara na kudai mshahara mzuri. Unaweza kudai peke yako tu hivyo hivyo. Unayo haki, ijapokuwa haiwezi kukupa nguvu. Mfanyakazi kutoingia kwenye chama hakumpotezei haki yake ya kudai mshahara mzuri hata kidogo. Kunampunguzia ile nguvu ya kufanikiwa peke yake; Lakini, anayo haki bado, inabaki ni haki yake. Huyu raia wa Tanzania akisimama peke yake tu, hana uwezo ule ule kama angekuwa anasimama na wengine.
Tujifunze kutoka historia ya uchaguzi wa mwaka 1961.
Sasa mfano mmoja nautumia mwisho kabisa. Mwaka wa elfu moja tisa mia na siti na moja tulikuwa na uchaguzi mkuu. Akatupinga kijana wetu mmoja anaitwa Herman Sarwatt. Ndiyo, si ulikuwa uchaguzi wa vyama vingi? TANU ilikuwa imechukua viti vingi bila kupingwa. Kiti cha Mbulu tulikuwa tumemweka chifu mmoja anaitwa Chifu Amri Dodo. Mwanàchama wetu mmoja alikuwa anaitwa Herman Sarwatt akasema. Alaa! Hiki chama changu hakina akili hata kidogo. Hawa viongozi wangu hawana akili! Hawa machifu ndiyo zamani wakitaka kutufunga wakati tukigombana na mkoloni. Leo wanamchukua Chifu Dodo aliyetaka kutufunga sisi ndiye awe mbunge wetu katika jimbo la Mbulu?
Sasa sisi tulikuwa tumekwisha kumchukua huyu kuwa ndiye mgombea rasmi wa TANU. Kijana yule akatupinga. Mimi nilitokea hapa Mbeya na nikasafiri kutoka Mbeya kwenda Mbulu kumtaiti yule mgombea wa TANU. Nikashindwa.
Wananchi wa Mbulu hawana uanachama tena, wengi tu wakasema ‘TANU wamekosea’. Wakampa kura Sarwatt. Wakafanya hivyo, mwanachama wa TANU akasimama mwenyewe akatushinda! Ilikuwa haki yake. Hatukuiondoa.
Mimi nadhani kwamba kwa kuwa sasa tunarudisha vyama vingi, vile vile tunarudisha haki zote zile zilizokuwapo za raia pamoja na haki; siyo haki ya kuunda vyama, bali pia wagombea binafsi kusimama kama Sarwatt alivyofanya.