Na Mwalimu Samson Sombi,JamhuriMedia

Imetimia miaka 23 tangu kutokea kwa kifo cha Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, katika Hospitali ya Mt. Thomas jiji la London nchini Uingereza Octoba 14, 1999.

Mwalimu Julias Kambarage Nyerere alizaliwa mwaka 1922 Kijijini Butiama katika mkoa wa Mara hivyo tunapoadimisha miaka 23 ya kifo chake tunaadimisha pia miaka 100 ya kuzaliwa kwake.

Mwanamapinduzi huyo wa Afrika aliamua kwa hiari kuacha kazi ya ualimu mwaka 1955 na kuingia rasmi katika duru za siasa katika harakati za kutafuta ukombozi wa Tanganyika na bara la Afrika kwa ujumla.

Katika harakati hizo Mwalimu Nyerere aliungana na viongozi wazalendo wa Afrika akiwemo Raisi wa kwanza wa Ghana Dk Kwame Nkrumah, Keneth Kaunda (Zambia) Nelson Mandela (Afrika Kusini) Patrice Lumumba wa Zaire (DRC) Robert Mugabe wa Zimbabwe na wengine wengi waliokuwa mstari wa mbele kutetea haki za waafrika katika ardhi ya Bara lao

Viongozi hao vijana wazalendo wa Afrika walianzisha vyama vya siasa katika hatua za kuwaunganisha waafrika na kuwa na nguvu moja katika mapambano ya kumwondoa mkoloni katika ardhi ya Afrika.

Ilikuwa ni vigumu sana kwa nchi ya Afrika kupata maendeleo bila ya kuwa na uhuru wa kupanga na kujiamulia mambo yao. Katika kutekeleza azma hiyo hatua ya kwanza ilikuwa ni kupigania uhuru wa nchi hizo.

Katika harakati za kupigania uhuru wa Tanganyika Mwalimu Nyerere na wenzake walianzisha chama cha TANU ambacho kilitokana na chama cha kutetea maslahi ya wafanya kazi cha Tanganyika Africa Association (TAA)

Chama kipigania uhuru wa Tanganyika TANU kilianzishwa 7, 1954 na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alichaguliwa kuwa kiongozi mkuu wa chama huku akitumia lugha ya Kiswahili kuwaunganisha wananchi katika mapambano ya kudai uhuru

Tangayika ambayo ilitawaliwa na wajerumani na baadaye waingereza ilipata uhuru wake Desemba 9, 1961 Mwalimu Nyerere akawa waziri mkuu na baadaye Raisi wa kwanza wa Tanganyika kabla ya kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Aprili 26, 1964.

Baada ya kupata uhuru wetu, na Mwalimu Nyerere kuwasha mwenge wa uhuru juu ya mlima Kilimanjaro katika kile alicho kieleza kuwa ni kuleta matumaini mapya upendo na kuwaamulika maadui wa ndani na nje ya nchi yetu.

Mwalimu katika hatua nyingine alisema “tumeonewa kiasi cha kutosha, tumenyonywa kiasi cha kutosha, Unyonge wetu ndio ulitufanya tuonewe, tunyonywe na kupuuzwa . Sasa tunataka mapinduzi, Mapinduzi ya kuondoa unyonge ili tusionewe tena, tusinyanyaswe tena na tusipuuzwe tena”
Wananchi wengi wa Afrika waliishi katika matarajio makubwa kuwa misingi ya ahadi za maendeleo walivokuwa wametoa baadhi ya viongozi wakati wa mapambano ya kudai uhuru hali ambayo imeendelea kuwa tofauti kadri miaka inavyosonga mbele.

Baadhi ya viongozi katika mchi za Africa wamesaliti ahadi za wapigania uhuru wa bara hilo wengi wanajigeuza kuwa miungu watu walafi wa madaraka na wenye tamaa ya kujilimbikizia mali huku rushwa na ufisadi ikiwa ni mtaji wao mkuu.

Mwalimu Nyerere alielewa yote hayo akasema kupanga ni kuchagua kati ya siasa kwa maana ya kuhubiri siasa bila maendeleo na kuleta maendeleo kwa wote kwa gharama ya siasa. Akachgua maendeleo kwanza na siasa ya pili kama nyenzo tu ya kufafanua maana ya maendeleo badala ya kutumia udikteta Katika kuleta maendeleo.

Akiandika katika kitabu chake cha “Uhuru na umoja, Mwalimu Nyerere anasema kila mtu ana mahitaji makuu mawili ya msingi. Kwanza ni uhuru wa kufikia matamanio ya maisha na hofu ya kwamba yote hayo yanapatikana kwa kushirikiana na wengine Ki- ujamaa

Katika dhana ya maendeleo kufuatia uhuru, Mwalimu Nyerere alitangaza vita dhidi ya maadui watatu wa maendeleo nchini ambao ni umaskini, maradhi na ujinga. Na kwamba ili tuendelee tunahitaji nyenzo kuu nne za maendeleo ambazo ni watu, ardhi sera (siasa) safi na uongozi bora.

Aliongeza kwa kusisitiza kwamba maendeleo ya nchi hayaletwi na fedha bali huletwa na watu wenyewe na fedha ni matokeo tu na sio msingi wa maendeleo. Sera za maendeleo za Mwalimu Nyerere zililenga zaidi maendeleo ya vijijini ambako Umaskini umejikita na waliko mafukara wengi, kwa kutumia vyanzo vya mapato ya nchi na kidogo vya misaada kutoka nchi rafiki.

Mpango wa maendeleo wa Tanganyika wa kwanza wa miaka mitatu 1961/1962- 1963/1964 uliolenga kupambana na maadui hao watatu.

Katika hatua nyingine Mwalimu Nyerere alitangaza Azimio la Arusha mwaka 1967 kurejesha na kuimarisha mpango wa maendeleo vijijini kwa kushirikisha sekta zote kwa kubinafsisha njia kuu za uchumi kuwa mikononi mwa umma na kuhakikisha maendele kwa wote.

Mwalimu Nyerere alieleza umuhimu wa amani katika kujiletea maendeleo na kwamba amani haiwezi kujileta yenyewe inapaswa kutafutwa na kuendelezwa. “Msifikiri amani mnayojivunia leo imejileta yenyewe . Azimio la Arusha halikuondoa umaskini lakini lilitoa matumaini kwa watu matumaini ya haki kwa wote ambayo wananchi wanaendelea kuyaishi na kadri inavyokuwa hivi amani itaendelea kuwapo.

“Watu wakianza kupoteza matumaini katika maendeleo kutalipuka volkano ya kuangamiza. Ninyi viongozi msifikiri watu wataendelea kukaa kimya bila kuona maendeleo’’ alisema Mwalimu Nyerere.

Mwalimu anaeleza dhana ya maendeleo ya vitu na watu kwamba ni uchangamkiaji wa vitu visivyoweza kuchangia uzalishaji wa mali na huduma kwa raia katika hatua yake ya maendeleo na ustawi wa jamii kwa ujumla
Anatoa mfano kwa kusema “Barabara mpya inampanulia mtu uhuru wake kama anaitumia kwa usafiri. Kuongeza idadi ya majengo ya shule ni maendeleo kama majengo hayo yanaweza kutumika na yanatumika kuongeza ujunzi na elimu kwa watu”

Kuhusu uhuru na maendeleo Mwalimu Nyerere anaeleza kwamba hivyo ni vitu viwili ambavyo vina uhusiano mkubwa sana na maana ya uhuru ni kuleta maendeleo ya watu

“Uhuru na maendeleo ni vitu vinavyohusiana sana uhusiano wao ni sawa na uhusiano baina ya kuku na yai bila kuku hupati mayai na bila mayai hupati kuku watakwisha. Vilevile bila ya uhuru hupati maendeleo na bila ya maendeleo ni dhahiri kwamba uhuru wako utapotea” alisema Mwalimu Nyerere.

Mwalimu alianzisha viwanda, na vyama vya ushirika katika kanda na mikoa mbalimbali hapa nchini lengo likiwa ni kuongeza uzalishaji, kutoa ajira, kuinua pato la taifa kuleta maendeleo na ustawi wa jamii ya watanzania kwa ujumla.

Wakati wa ukoloni na baada ya uhuru Mwalimu Nyerere alihubiri sana umuhimu wa umoja kama silaha madhubuti ya kuyasaka maendeleo na hatimaye nchi kujitegemea

Mwaka 1961 katika mkutano wa hadhara Wilayani Korogwe Mkoa wa Tanga Mwalimu Nyerere alisema “ Sijaleta uhuru wa Tanganyika bali ni umoja wenu ndio ulioleta uhuru na umoja huu unatakiwa kuendelea”

Mwalimu Nyerere ni moja ya waasisi wa umoja wa nchi huru za Africa (O.A.U), 1963 na sasa umoja wa Afrika (AU) na pia alifanikisha kuziunganisha nchi ya Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964 muungano ambao unaendelea kudumu na kuwa mfano katika Afrika huku akifuta ukabila , ubaguzi wa kidini na rangi katika nchi yetu.

Julai 29, 1985, Baba wa taifa Mwalimu Nyerere alihutubia Bunge na kuliaga baada ya uamuzi wake wa kung’atuka madarakani kwa hiari yake na kueleza mafanikio na juhudi za ujenzi wa Taifa lililoshikamana.

“Kazi moja muhimu sana kwangu mimi na kwa watu wa nchi hii ambayo niilieleza kwenye hotuba ya uzinduzi Desemba 1962 ilikuwa ni ya kujenga Taifa lililoshikamana kwa misingi ya utu na usawa wa binadamu. Nilipohutubia umoja wa mataifa mwaka mmoja kabla niliahidi pia kwamba misingi ya ujenzi wa Taifa letu itakuwa uamuzi wa kiungwana na kuheshimu utu na usawa wa Binadamu. Kitaifa na kimataifa suala la umoja ilikuwa ndio hoja yangu kuu wakati nilipohutubia tena Bunge Aprili 25, 1964 nikiwaomba kuridhia makubaliano ya kuunganisha nchi mbili huru za Tanganyika na Zanzibar.

“Naamini naweza kusema bila wasiwasi kwamba katika hili la msingi zaidi kati ya malengo yote tulivyokuwa nayo baada ya miaka chini ya 25 . tunayo sababu ya kuona fahari tuna taifa lililojengwa juu ya msingi ya usawa wa binadamu”.

Kuhusu ukabila na ukanda hapa nchini Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa mstari wa mbele kukemea na kusisitiza kwamba Tanzania hatutambuani kwa makabila bali kwa utaifa wetu.

“Hapa katika mfumo wa makuzi shule na katika siasa tunashukuru sana Baba wa Taifa letu Mwalimu Nyerere ametukuza bila kuangalia makabila yetu. Ametukuza hivyo. Tunapofanya kazi hapa na mimi binafsi niko hapa bila kuangalia kabila fulani’’ anaeleza Rais Samia

Mtaalamu wa elimu ya urai mwalimu Leonard Kitindi wa manispaa ya Morogoro anasema tumuenzi Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere kwa kudumisha umoja wa kitaifa na haki za binadamu.

0755985966