Kumbukizi ya miaka 19 tangu Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, afariki dunia imemalizika huku wananchi wengi wakitaka kiongozi huyo aenziwe kwa vitendo.
Wananchi walioshiriki mijadala kwenye mitandao ya kijamii, redio, televisheni, magazeti na makongamano wameipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuthubutu kurejesha misingi iliyowekwa na Baba wa Taifa.
Baadhi ya kilio kilichosikika kutoka kwa wachangiaji ni Katiba mpya ili kujenga misingi ya haki na usawa katika nchi.
Wanaamini kwa kuwa na Katiba mpya itakayotokana na matakwa ya wananchi, demokrasia na usawa vitastawi katika jamii, tofauti na hali ilivyo sasa.
Wachangiaji wengi wameonyesha kuunga mkono juhudi za serikali za kufufua ari ya ujenzi wa viwanda nchini, mapambano dhidi ya rushwa, ujenzi wa reli na barabara, ujenzi wa vyanzo vya umeme (Stigler’s Gorge), ulinzi na rasilimali za nchi na ukomeshaji wa vitendo vya uonevu na pia kufufua tabia ya uwajibikaji miongoni mwa watumishi wa umma.
Baadhi ya wasomi na wazee wamemjadili Mwalimu kwa namna tofauti, lakini mambo makuu yakiwa ni namna alivyojenga taifa lisilo na matabaka, ukombozi wa wanyonge, vita dhidi ya rushwa na maendeleo ya watu badala ya maendeleo ya vitu.
Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kilichopo Kigamboni, Dar es Salaam, kiliendesha kongamano lililowahusisha wasomi na baadhi ya watu waliofanya kazi na Mwalimu.
Kaulimbiu ya kongamano hilo ilihusu ‘Falsafa ya Mwalimu Nyerere juu ya taifa kujitegemea na maendeleo ya viwanda Tanzania.’
Akiwasilisha mada kuhusu umuhimu wa uzalendo na uadilifu katika kukuza uchumi wa viwanda, Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Shadrack Mwakalila, amesema Mwalimu Nyerere alianzisha viwanda ili kujenga taifa imara linalojitegemea kiuchumi.
“Viwanda vilianzishwa vya nguo, kubangua korosho, kuchambua pamba, zana za kilimo… Viwanda hivi vilikuwa na manufaa makubwa kwa Watanzania maskini.
“Vilijengwa ili viweze kuimarisha uchumi kwa kupata malighafi kutoka kwa wakulima na kutengeneza bidhaa kabla ya kuuza soko la ndani na la nje ya nchi. Mwalimu aliamini kuwa ili Tanzania iweze kuendelea ni lazima tuwe na viwanda vya kutosha – hasa viwanda vya umma, kwani uchumi wa viwanda utaliepusha taifa kuwa tegemezi,” amesema Profesa Mwakalila.
Kwa bahati mbaya, anasema jitihada na mafanikio yaliyofikiwa Tanzania katika ujenzi wa viwanda hayakudumu kwa muda mrefu. Viwanda vingi vilivyoanzishwa vilikufa.
Anasema miongoni mwa sababu kubwa ya kufa kwa viwanda hivyo ni uongozi na uendeshaji mbaya, hujuma na ukosefu wa uadilifu na uzalendo.
Anaipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuja na sera ya viwanda katika kukuza uzalendo na utaifa na uadilifu kwa watumishi wa umma na uadilifu kwa sekta binafsi.
“Uchambuzi katika mada hii unathibitisha kuwa ili serikali iweze kukuza uchumi wa viwanda inahitaji watu ambao ni wazalendo, waadilifu, waaminifu, wenye nidhamu, wenye kujiheshimu, wenye mshikamano na wenye kutanguliza mbele masilahi mapana ya taifa,” anasema.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Dk. Ayoub Rioba, aliyewasilisha mada kuhusu umuhimu wa misingi ya Azimio la Arusha katika kustawisha viwanda vya ndani, anasema misingi ya Azimio hilo imeelezwa katika utu, usawa, heshima, haki na ustawi wa wananchi.
“Ni wajibu wa serikali, ambayo ni watu wenyewe, kuingilia kati kwa vitendo maisha ya uchumi ya taifa ili kuhakikisha ustawi wa raia wote; na kuzuia mtu kumnyonya mtu mwingine au kikundi kimoja kunyonya kikundi kingine na kuzuia limbikizo la utajiri kufikia kiasi ambacho hakipatani na siasa ya watu wote kuwa sawa.
“Katika kusimamia misingi ya Azimio la Arusha, serikali kupitia kwa watendaji wake ina wajibu wa kuhakikisha viwanda vinasaidia kuongeza uwezo wa taifa na watu wake kuwa huru na si vinginevyo,” anasema Dk. Rioba.
Katika mada yake kuhusu mtazamo wa Mwalimu Nyerere juu ya Azimio la Arusha na taifa linalojitegemea, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Montanus Milanzi, amesema mitazamo ya Baba wa Taifa ni tunu na amali ya kujivunia ambayo kila kiongozi na mwananchi hana budi kuienzi na kuitumia kuleta maendeleo kiuchumi, kisiasa na kijamii.
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Bashiru Ally, anasema uzalendo uliofundishwa na Mwalimu Nyerere ni wa kitaifa unaounganisha makabila, tamaduni na dini.
“Kwa hiyo tunapoanza kusifia uzalendo tuupe sifa. Uzalendo aliouhimiza Mwalimu ni wa kitaifa. Alitambua tunayo makabila mengi, tuna dini nyingi na tamaduni mbalimbali, lakini zote zikusanywe na utamaduni wa kitaifa tujenge taifa,” anasema.
Katibu Mkuu huyo anasema wananchi walipoacha kujadiliana masuala ukazuka uzalendo wa kibaguzi ukiwemo wa kikabila, kidini na wa kupenda vitu.
“Tuwe wakweli, hii hali ipo na wakati mwingine imekuwa na wakati wa kutisha. Mtu anatafuta uongozi anaanza kuwasiliana na kabila lake. Au mtu anaangalia kabila lake limepunjwa au limezingatiwa.
“Hivyo hivyo, kwenye dini na siku hizi kuna ubaguzi hata wa kupenda vitu na anasa. Mtu anaiba, lakini waliomchagua wanamwita jasiri, mjanja. Hiyo tukiizoea nayo inaweza ikawa uzalendo wa kusifu wezi,” anasema.
Profesa wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu cha Dar es Salaam (DUCE), Bernadetta Killian, anawashangaa wanaompinga Dk. Bashiru kwa kuikosoa CCM wakati hata Mwalimu Nyerere aliwahi kuikosoa kwa utendaji wake.
Profesa Killian anasema kiongozi mzuri ni yule anayejikosoa hata mwenyewe kutokana na utendaji wake.
“Dk. Bashiru alikikosoa chama chake alipokuwa mkoani Morogoro kwenye shughuli za chama, lakini watu waliposikia hivyo wakaja juu kweli – nawashangaa kwa kweli,” anasema Profesa Killian.
Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Profesa Mwakalila, ametoa rai kwa Dk. Bashiru kuwahamasisha viongozi wa CCM kwenda chuoni hapo kusomea maadili na utawala bora.
Waziri wa zamani, Paul Kimiti, akizungumza katika kongamano hilo amesema wakati wa Mwalimu Nyerere walifundishwa juu ya uongozi bora.
Anasema mwaka 1971 Mwalimu aliandika kitabu kilichokuwa kinahusu uongozi bora vijijini na alikigawa bure kwa wananchi na wengi, hasa vijijini, lakini sasa viongozi wa kisiasa wanapiga kelele badala ya kutilia mkazo kilimo bora.
“Tulikuwa na vipindi Redio Tanzania, tulikuwa tunaelimisha wananchi kuhusu kilimo, lakini sasa viongozi wetu wa siasa hawatoi hata elimu hiyo kwa wananchi tena kama ilivyokuwa enzi zetu,” anasema.
Kimiti aliyewahi kufundisha hapo chuoni, anatoa mwito kuwatumia wataalamu ili kutimiza falsafa ya Baba wa Taifa juu ya nchi kujitegemea na maendeleo ya viwanda.
“Tanzania ina wataalamu wengi ambao wakitumika vilivyo, lazima lengo la falsafa hii ya Mwalimu itimie, kwa sababu hata mimi kipindi kile alikuwa akinitumia kuwafundisha vijana kuhusu masuala ya siasa na kilimo na tulikuwa tukifikia lengo,” anasema.
Naye, Buberwa Kaiza, anasema hata msomi akiulizwa kuhusu dhana ya viwanda hawezi kutoa jibu la kueleweka, na kwamba likizungumziwa suala hilo wengi wanadhani ni lazima kuwe na viwanda vikubwa.
Awali, akifungua kongamano hilo, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako, amemfananisha Rais John Magufuli na Mwalimu Nyerere, akisema amekuwa mstari wa mbele kupigania masilahi ya taifa na kupambana na viongozi wanaokwenda kinyume cha matarajio ya Watanzania.
“Mwalimu Nyerere alikuwa kiongozi wa mfano, ambaye katika maisha yake aliweka mbele masilahi ya taifa kuliko masilahi yake binafsi,” amesema Profesa Ndalichako.
Mwalimu Nyerere alifariki dunia Oktoba 14, 1999 katika Hospitali ya Mtakatifu Thomas nchini Uingereza alikokuwa akitibiwa saratani ya damu (leukemia).
Mwalimu alizaliwa Aprili 13, 1922 kijijini Butiama, akiwa mmoja wa watoto wa Chifu Nyerere Burito.