Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Tabora
Mwalimu wa shule ya msingi Chipukizi Kata ya Igunga wilayani Igunga Mkoani Tabora Andrew Rutabagisha (41) ametiwa mbaroni na Mahakama ya Hakimu Mfawidhi wilayani hapa baada ya kukutwa na kosa la wizi wa fedha za uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 kiasi cha sh. 200,000.
Mwendesha Mashitaka wa Serikali kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), wilayani hapa Mazengo Joseph aliiambia mahakama mbele ya hakimu wa wilaya Hudi Hudi kuwa Mshtakiwa alitenda kosa hilo kati ya Oktoba 23, 2015 na Oktoba 26, 2015.
Mazengo aliiambia mahakama kuwa mtuhumiwa akiwa Msimamizi wa Uchaguzi katika kata ya Mbutu Wilayani hapa alitumia kiasi cha sh. 200,000 kwa manufaa yake binafsi kwa kufanya marejesho kuwa alikodisha vifaa vya kutangazia matokeo akijua kabisa hakufanya hivyo.
Alibainisha kuwa mtuhumiwa alitenda kosa hilo kinyume na kifungu cha 22 cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa ambapo baada ya kusomewa shitaka hilo mshtakiwa alikana kutenda kosa hilo, wakati wa kusikilizwa shauri hilo jumla ya mashahidi 7 walitoa ushahidi mahakamani hapo.
Baada ya kusikiliza ushahidi wa pande zote mbili Hakimu Hudi alisema ushahidi uliotolewa umemtia hatiani pasipo shaka mtuhumiwa, hivyo mahakama inamuhukumu kutumikia adhabu ya kifungo cha mwaka mmoja jela au kulipa faini ya sh. 500,000 ambapo alikubali kulipa faini na kuachiwa.