Mtu mmoja amefariki dunia na wengine watatu wamo katika hali mbaya baada ya kunywa pombe iliyotengenezwa na mwalimu wa somo la Kemia wa Shule ya Sekondari ya Chole.

Miongoni mwa waliokunywa pombe hiyo ni Ramadhani Pakacha na Shaibu Pakacha, ndugu wa familia moja, ambapo pamoja na Shaibu kukimbizwa katika Kituo cha Afya cha Maneromango kupata tiba baada ya kunywa pombe hiyo, alifariki dunia.

Mtendaji wa Kijiji cha Maneromango, Nassoro Mmanga, amesema analifahamu tukio hilo lililotokea wiki mbili zilizopita, ambapo watu walifika nyumbani kwake kumpa taarifa kuwa watu wanne katika kijiji chao wamepoteza fahamu kwa sababu ya kunywa pombe kali iliyotengenezwa kwa kemikali na Mwalimu Ladislaus Mkama katika mabaara ya shule.

Mmanga ameliambia JAMHURI kuwa alikwenda kuwaona wagonjwa hao waliozidiwa na kilevi akakuta wanatapika matapishi ya njano na vitu vyeusi vyeusi, hivyo akashauri wapelekwe hospitalini haraka.

Kwa mujibu wa mashuhuda, Mwalimu Mkama alikuwa na utaratibu wa kuchanganya kifuniko kimoja cha kemikali za maabara na lita mbili za maji, ila zamu hii alichanganya kifuniko hicho na soda ya Sprite.

Mmanga amesema ilikuwa ni kawaida ya Mwalimu Mkama kuiba kemikali na kwenda kwa wanakijiji kuwapatia kinywaji hicho kama pombe, lakini inavyosemekana siku hiyo alizidisha kipimo, kwani hata yeye alikunywa kinywaji hicho kikamdhuru na akapoteza fahamu.

Cha kushangaza, Mwalimu Mkama mara zote alikuwa anawaambia wateja wake kuwa ikitokea wakazidiwa kwa kunywa kinywaji hicho wasitumie tiba ya hospitali kwani ingewaua.

Amesema wanakijiji walioathirika katika tukio hilo ni Shaibu Ali Pakacha (aliyefariki dunia), Ramadhani Ali Pakacha, Karimu Besta na yeye Ladislaus Mkama. 

Daktari wa Kituo cha Afya Chole, Rashidi Pengu, amethibitisha kuwapo kwa tukio hilo. Mkuu wa Shule ya Sekondari Chole, Ngonyani, amesema Mwalimu Mkama alifika kazini Jumatatu ya wiki iliyopita, lakini baada ya muda mfupi alitoweka na kwenda kusikojulikana.

Mmoja wa wanafunzi wa Kidato cha Kwanza, Saiwan Telelesfory, amesema amekuwa akisikia tetesi kwamba Mwalimu Mkama anachanganya kemikali za maabara na kuwa kinywaji, lakini yeye hajawahi kumuona.

Rehema Mbegu ambaye ni mfanyabiashara wa pombe za kienyeji Chole, amesema kitendo cha mwalimu huyo kutengeneza kinywaji kilikuwa kinamkosesha wateja katika klabu yake.

Ali Salehe Pakacha, ambaye ni baba wa Shaibu aliyefariki dunia, ameeleza kusikitishwa na tukio hilo. Kwa upande wake Ramadhani Pakacha aliyenusurika, amesema Mwalimu Mkama alifika akiwa ameshikilia chupa iliyokuwa na kimiminika alichomwambia ni methanol kinachokuwepo katika maabara. 

Aliwaambia kuwa kinywaji hicho kinatibu maradhi ya tumbo, minyoo na homa ya matumbo kwa mtu kuchanganya kifuniko kimoja na lita moja ya maji, na walivyokunywa kikawadhuru.

Ofisa Elimu wa Wilaya, Patrick Gwivana, amekemea tabia hiyo ya kutumia kemikali za maabara kinyume cha matumizi halali, akisema jambo hilo halikubaliki.

Mkuu wa Polisi wa Wilaya, OCD Eva Stesheni, ameliambia JAMHURI kuwa suala hilo lipo chini ya uchunguzi wa polisi.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya, Musa Gama, naye amethibitisha kupata taarifa hizo, huku Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya, Grayson Mramba, akisema suala hilo ni la aina yake.