Mwalimu Magreth Magesa

Mwalimu wa Shule ya Msingi Kasamwa, Magreth Magesa, anadaiwa kusababisha migogoro ya kiutendaji shuleni hapo, hali iliyosababisha kuhamishwa kwa Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, James Magela.

JAMHURI kupitia kwa vyanzo vyake, limebaini kuwa Mwalimu Magreth Magesa amekuwa ni mtovu wa nidhamu kwa kipindi kirefu huku mamlaka husika zikimkingia kifua kwa kutokumwajibisha.

JAMHURI limebaini kuwa Mwalimu Magesa amekuwa na tabia ya utoro kazini kupitia visingizio mbalimbali na kutokuwa na uhusiano mzuri na walimu wenzake.

 “Mtu huyo alimwambia mkuu wetu kuwa, Mwalimu Magesa amelazwa Mwananchi Hospitali, lakini mkuu hakukubaliana na mtu huyo kwa vile simu ya mkononi haiwezi kuwa taarifa kamili na baadaye alimtumia ujumbe mfupi wa maneno,’’ amesema Mwalimu aliyeomba jina lake lisitajwe.

Ujumbe huo wa maneno uliotumwa kwa mwanamme huyo ambaye inasadikiwa kuwa ni mume wa Magesa na ambao JAMHURI limeuona unasomeka.

“Tunao utaratibu mzuri tu ambao ukifuatwa hakuna tatizo, lakini tunapoanza tu kutumia simu ni tatizo. Tusome alama za nyakati na kwa hili nitapata umaarufu wa bure, mhusika anajua utaratibu.’’

JAMHURI limeelezwa kuwa saa saba alasiri ya siku hiyo Mei 30, mwaka jana, Mwalimu Magesa alifika shuleni kwa usafiri wa gari dogo la mtu binafsi akiwamo na muuguzi, dereva na mwanamme mmoja.

Mwanamme huyo hakujitambulisha kwa uongozi wa shule hiyo, badala yake alikuwa akitoa maneno ya kejeli akidai uongozi wa shule hiyo unajifanya Tomaso, maneno yaliyoonesha kumlenga mkuu wa shule hiyo ambaye amekuwa mstari wa mbele kukemea vitendo vya utovu wa nidhamu vinavyofanywa na Mwalimu Magesa.

Kwa mujibu wa vyanzo vyetu, ilimlazimu mkuu wa shule hiyo kuwakaribisha ofisini kwake mwalimu na muuguzi huyo na kupewa fomu za ruhusa pamoja na ‘sick sheet’.  

Baada ya kupona na kurejea kazini, Mwalimu Magesa alionywa na kamati ya nidhamu ya Shule ya Msingi Kasamwa ambapo aliomba radhi.

Pamoja na kuomba radhi, alitakiwa pia kufidia vipindi vilivyopotea katika madarasa anayoyafundisha kwa mujibu wa kanuni namba 118 ya Kanuni za Utumishi wa Umma ya mwaka 2003 kipengele cha 2.2.

JAMHURI limefunga safari hadi katika Shule ya Msingi Nyakato iliyopo Kata ya Nyanguku, Halmashauri ya Mji wa Geita kwa ajili ya kuona na James Magela aliyekuwa Mkuu wa Shule ya Msingi Kasamwa ili kujua undani kuhusu uhamisho wake.

Hata hivyo, pamoja na kushindwa kufafanua kwa undani kuhusu uhamisho wake, alikiri kutokuwa na mchezo kwenye suala la walimu wa chini yake wanaotekeleza majukumu yao kinyume cha taratibu za utumishi wa umma.

“Unajua ndugu mwandishi, kama unavyodai umeelezwa nimehamishwa ni kweli kabisa, unajua watumishi wa umma tunaofanya kazi katika ngazi ya kuwahudumia wananchi moja kwa moja.

“Walimu ambao tunatoa elimu kwa watoto wa masikini tusipokuwa makini tutakwamisha malengo mazuri ya Serikali yetu na mimi kama Mwalimu Mkuu, sipo tayari kutetea walimu wazembe ambao hawana tija kwa Taifa. 

“Nasema hayo kwa sababu shule kama taasisi tumejiwekea malengo lakini kwa kukumbatia walimu wa aina hiyo hatuwezi kufikia malengo,’’ amesema Magela.

Kuhusu uhamisho wake, Magela aliomba waulizwe waliomuhamisha japo yeye anaamini ni kawaida. Agosti 28, mwaka juzi, kamati ya nidhamu ya shule ilikaa kumjadili na kumuonya kutokana na mienendo yake mibaya kazini.

Januari 30, mwaka juzi, mwalimu huyo alikuja na dripu kazini akiwa na muuguzi na usafiri wa gari binafsi (siyo gari la wagonjwa) akitokea Mwananchi Dispensary ya Mwanza.

Juni 7, mwaka jana, katika kikao cha walimu (staff) walimuonya mwalimu kuacha kufanya vituko na kuonesha mfano mbaya kwa walimu, jamii na viongozi.

Julai 11, mwaka jana, Mwalimu Magesa aliitwa kwenye kikao cha nidhamu cha Idara ya Elimu Wilaya ambako aligoma kujieleza kwa maandishi ambapo kamati ilipendekeza kwa mkurugenzi afukuzwe kazi. Oktoba 4, mwaka jana, Tume ya Utumishi ya Walimu ilimpatia Mwalimu Magesa onyo kwa maandishi.

Januari 18, mwaka huu, Ofisi ya Elimu Geita ilimwandikia barua ya uhamisho Mwalimu Magesa ambayo alikabidhiwa Januari 20, mwaka huu. Barua ya uhamisho ambayo gazeti hili limebahatika kuiona iliyosainiwa na C. M Mashalla kwa niaba ya mkurugenzi, inaonesha Mkurugenzi Modest Appolinary kupewa taarifa.

Hata hivyo, katika hali ya kushangaza, Januari 23, mwaka huu, Mkurugenzi wa Mji wa Geita, Modest Appolinary, alijibu kwa Afisa Elimu kwa kuandika barua ya kumhamisha Mwalimu Mkuu Magela kutoka kwenye shule hiyo kwenda Shule ya Msingi Nyakato.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Geita, Leonard Bugomola, ni kati ya viongozi walioshtushwa na uhamisho huo kutokana na uchapakazi wa Mwalimu Mkuu Magela na kuahidi kufuatilia.

“Una hakika amehamishwa? Siamini kama amehamishwa na kama kweli amehamishwa nitafuatilia kujua kilichopo nyuma ya pazia,” amesema Bugomola.

Hata hivyo, baadhi ya wananchi wenye watoto kwenye shule hiyo, Cosmas Mazuri na Tatu Kudema, Shahidu Kashakala na Athumani Iddi, walimtaka Waziri wa Elimu, Profesa Joyce Ndalichako, kuingilia kati mgogoro huo kabla haujaleta madhara makubwa zaidi na kumrejesha mkuu huyo kwenye shule hiyo, kwa vile juhudi zake ndizo zilizozaa matunda ya kuongeza ufaulu katika shule hiyo.

“Tunamuomba Waziri Ndalichako aingilie kati kuhusu suala hili ambalo limeonekana kutuchanganya akili zetu, haiwezekani Mwalimu Mkuu aliyesimamia na kutekeleza majukumu yake ahamishwe kisa kusimamia majukumu yake; hii haikubaliki hata kidogo,” amesema Cosmas Mazuri.

Hata hivyo, uchunguzi wa JAMHURI umebaini kuwa pamoja na Mwalimu Magesa kudai mara kwa mara ni mgonjwa kwa lengo la kutohudhuria vipindi darasani, fomu za hospitali alizoziwasilisha kwa uongozi wa shule na wilaya zina walakini.

Kutokana na fomu hizo kuonesha daktari wa Mwananchi Hospital aliyempokea, aliyempa ruhusa ya kwenda shuleni kuomba ruhusa akiwa na dripu, aliyempa ruhusa ya kumaliza matibabu ni daktari Kayanga, jambo ambalo linaacha maswali mengi kana kwamba hospitali hiyo inaye daktari mmoja.

Mbali na hilo, uchunguzi pia umebaini kuwa fomu ya kupokelewa hospitali inaonesha hakulazwa na badala yake alitibiwa na kuruhusiwa siku hiyo hiyo ya Mei 30, mwaka jana, lakini cheti cha kumruhusu kutoka hospitali kinaonesha aliruhusiwa kutoka hospitali Juni 2, mwaka jana.

Uchunguzi huo umebaini kuwa fomu hizo za hospitali hazina tarehe ya kumruhusu kutoka hospitali, lakini pia magonjwa yaliyoandikwa ni malaria na typhod wakati cheti cha kukamilisha matibabu kinaonesha magonjwa tofauti yaani malaria na UTI.

Zipo pia dosari kadhaa kwenye uhamisho wa mkuu wa shule ambapo unaonesha mkuu wa Idara ya Elimu ya Msingi hakushirikishwa, wakati uhamisho wa Mwalimu Magesa mwajiri ambaye ni mkurugenzi alipewa taarifa.

Mwalimu Magesa alipotafutwa na mwandishi wa makala hii, aliomba atafutwe baada ya muda kwa vile kwa wakati huo hakuwa sehemu nzuri kutoa ufafanuzi suala hilo.

“Najua upo kazini, nimekwambia siwezi kuongea chochote kwa vile nipo sehemu mbaya, hapa nipo dukani nahudumia wateja na wateja wamejaa, hivyo naomba usubiri kidogo nikimaliza kuwahudumia nitakubipu,” amesema Magesa.

Hata hivyo, katika hali isiyokuwa ya kawaida, Mwalimu Magesa alipopigiwa tena simu hakukana wala kukiri, na badala yake alidai kuwa masuala hayo yalishapita na yalizungumziwa yakaisha huku akimpatia simu mwanaume aliyedai ni mume wake, kwa madai ndiye msemaji wake ambaye alianza kumporomoshea matusi mwandishi wa habari.

 “Wewe mwandishi una mamlaka gani ya kumpigia simu mke wangu, unakibali cha kumpigia simu huyu, msiwe wapumbavu, acheni upumbavu wenu…yaani wewe mwandishi ni mpumbavu mpumbavu,” ametukana mwanaume huyo aliyedai mume wa Mwalimu Magesa.

Kwa upande wake, Afisa Elimu Mji wa Geita, David Mkumbo, amesema uhamisho huo ni wa kawaida na si wa uonevu kama ambavyo imekuwa ikielezwa.

Naye Mkurugenzi  wa Halmashauri ya Mji wa Geita,  Modest Appolinary, alidai kuwa kinachoendelea Shule ya Msingi Kasamwa ni siasa na si suala jingine na waliamua kuwahamisha walimu hao ili kuondoa migongano iliyokuwa hapo kati ya Mwalimu Magesa na Magela ambao wamekuwa na tofauti kwa muda mrefu, jambo alilodai lingeweza kuathiri shule hiyo.

Aidha, mkurugenzi huyo alidai kabla ya kuwahamisha walimu hao, aliwaomba kila mmoja aandike maelezo yake kutokana na utofauti uliopo kati yao na walifanya hivyo ili kusikiliza pande zote mbili kuepuka mmoja wao kulalamika kwamba ameonewa. Baada ya kuwasilisha ofisini kwao, aliamua kuwahamisha wote uhamisho aliodai ni wa kawaida.

Katibu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) wilayani Geita, John Kafimbi, alidai kuwa kinachoendelea kwenye Shule ya Msingi Kasamwa kimetokana na uamuzi ambao unatolewa kinyemela pasipo ushirikishaji wa pande zote mbili.