Na Mwandishi Wetu
Bondia, Hassan Mwakinyo ‘Champez’ anatarajiwa kupigana na bondia kutoka Zimbabwe, Enock Msambudzi Januari 27 mwaka huu visiwani Zanzibar.
Pambano hilo la kwanza tangu kuachiwa huru na Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa nchini (TPBRC) baada ya kuwa kifungoni kwa takribani mwezi na majuma mawili kufuatia kutumikia adhabu ya kifungo cha mwaka mmoja na faini ya Sh milioni moja.
Akizungumzia pambano hilo lililopewa jina la ‘Mtata Mtatuzi’, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Zanzibar, Ramadhan Bukini amesema pambano hilo litapigwa kwa mara ya kwanza katika uwanja mpya wa ndani wa masumbwi ‘indoor arena’ ndani ya Uwanja mpya wa Amaan complex.
“Pambano hili litafungua fursa kwa wawekezaji kuona fursa za kiuchumi zilizopo visiwani humo,” amesema Bukini.
Kwa upande wake, Mwakinyo amesema yupo katika maandalizi mazuri kuelekea pamabano hilo ambalomipango inaendelea kuhakikisha linakuwa na mkanda wa Shirika la Masumbwi Ulimwenguni (WBO).
“Nipo katika maandalizi mazuri sana. Nimejihakikishia hakuna atakayejuta kunishabikia,” amesema Mwakinyo
Naye, balozi wa pambano hilo na mwandishi wa habari, James Tupatupa amesema pambano la Mwakinyo limebeba taswira ya mapinduzi kutokana na uimara na umahiri wa bondia huyo.
“Mapinduzi rasmi ya ngumi yanaenda kufanyika Zanzibar, kwani linaenda kuwa zaidi ya pambano la kawaida,” amejinadi Tupatupa
Jumla ya mapambano 11 yanatarajiwa kushuhudiwa siku hiyo ambapo wanamasumbwi kutoka mikoa ya Zanzibar, Mbeya, Tanga na Dar es Salaam wanatarajiwa kuburudisha usiku huo.