Katika sherehe za kuadhimisha miaka 38 ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete, amenukuliwa akiwasihi wanachama wenzake kuhimiza kujitokeza mgombea atakayeiletea CCM ushindi kwenye Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba, mwaka huu.

Alimnukuu Mwalimu Nyerere akisema: “Nataka rais atoke CCM” na maelezo yake ni rahisi tu; Mwalimu Nyerere alishawahi kusema rais anaweza kutoka chama chochote cha siasa, lakini rais bora lazima atoke CCM, na huu ni wosia mzuri tu na muhimu sana.

Kumtaja Mwalimu Nyerere imekuwa desturi sasa kila tunapoingia kwenye mwaka wa uchaguzi. Na siyo jambo linalofanywa na CCM pekee, bali ni jambo ambalo hata vyama vingine vya siasa hufanya, ingawa unaweza kusema kuwa malengo ya CCM yanatofautiana kidogo na yale ya vyama vingine vya siasa.

CCM inamtaja Mwalimu kama kinga dhidi ya wale ambao wanaamini kuwa CCM ya Mwalimu na hii ya leo ni tofauti ya usiku na mchana. Havifanani hata kidogo. Kwa CCM, Mwalimu Nyerere anatajwa kama kinga dhidi ya mbu wanaokithiri na kuhatarisha afya ya chama kipindi cha uchaguzi mkuu.

Wapinzani wao huwa na nia moja ya msingi wanapomtaja Mwalimu Nyerere. Wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, nilihudhuria jijini Mwanza mkutano wa kampeni uliohutubiwa na Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba.

Sehemu kubwa ya muda uliotumika kwenye mkutano ule ilitumika na meneja wa kampeni wa CUF kunukuu maandishi na matamshi ya Mwalimu Nyerere na kulinganisha yanatofautiana kwa kiasi kikubwa na mwenendo katika sera na uamuzi wa CCM na Serikali yake.

Kwenye mwaka wa uchaguzi baadhi yetu ambao hatuonei haya kuunga mkono sera na uongozi wa Mwalimu Nyerere tunapata faraja kubwa sana. Tunamsikia Mwalimu Nyerere kwa marudio ambayo siyo ya kawaida.

Tunakumbushwa kuwa alikuwa ni kiongozi aliyeongoza nchi kwa misingi ya haki na usawa kwa raia wote; aliyekuwa muadilifu na ambaye alitanguliza maslahi ya nchi kwa kila uamuzi uliofanywa chini ya utawala wake. Hakuvumilia rushwa na alichukua hatua kali dhidi ya wale ambao walionekana kukiuka maadili ya uongozi. Na tutasikia mengi kuliko haya niliyotaja hapa.

Kwa kifupi, zile zinazoonekana kuwa sera na sifa bora za uongozi ambazo Mwalimu Nyerere anahusishwa nazo zitatumika na vyama vya siasa kama vigezo vya kupima baadhi ya viongozi watakaojitokeza kuwania nafasi mbalimbali za uongozi wakati wa uchaguzi.

Siku moja baada ya uchaguzi, watakaochaguliwa watafurahi wakati wale ambao hawakuchaguliwa watalalamika, au mahakamani au nje ya mahakama na Mwalimu Nyerere na sera zake pamoja na sifa zake za uongozi zitafungiwa kabatini mpaka uchaguzi mkuu ujao mwaka 2020.

Wengi wetu tutarudi kupambana na changamoto za maisha ya kila siku, lakini wakati huo huo sisi mashabiki wake tutajihesabu tena na tutaendelea na jitihada zetu za kumuenzi. Tunashukuru kuwa kwa sasa tunasaidiwa na msimamo wa Mwenyekiti aliyechaguliwa wa Umoja wa Afrika, Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe, ambaye anaweka jitihada mahususi na nguvu za umoja huo kukumbuka mchango wa Serikali ya Tanzania chini ya uongozi wa Mwalimu Nyerere kuchangia ukombozi wa Bara la Afrika.

Hoja yangu hii: Tunamkumbuka Mwalimu Nyerere wakati wa shida tu, lakini wakati wa raha (baada ya ushindi wa uchaguzi) hatumkumbuki tena. Na hili linaelekezwa kwa CCM zaidi. CCM ingemtumia Mwalimu Nyerere kwa miaka yote mitano baada ya uchaguzi badala ya wakati wa kampeni tu, ingepungukiwa na matatizo mengi ambayo inakabiliwa nayo.

Nitaje misimamo machache ya Mwalimu Nyerere ambayo tungeishikilia kama Taifa ingetuepusha na  mengi. Baadhi imetajwa na Mwenyekiti Kikwete huko Songea. Matumizi makubwa ya rushwa za kila aina wakati wa kampeni za uchaguzi yamefanya CCM kuwa chama cha viongozi ambao wapo madarakani kwa uwezo wa fedha zao, na kwa tabia ya wapigakura ya kukubali rushwa kuwa kigezo cha msingi cha kuchagua kiongozi.

Kiongozi anayenunua nafasi yake hawezi kupoteza muda wake kusimamia maendeleo ya wapiga kura wake. Kipaumbele kwake kitakuwa ni kutumia nafasi yake ya uongozi kutafuta ‘fursa’ za kurudisha pesa alizotumia kwenye uchaguzi.

CCM yapaswa kurudi kwenye Azimio la Arusha. Nitaje mambo kadhaa ya msingi ya Azimio la Arusha: kiongozi ni mume na mke wake, au mke na mume wake. Mimi ningependa kuliongezea Azimio: “na familia yake ya karibu.”

Tunapaswa kuhoji uhalali wa kiongozi anayechaguliwa akiwa na hali ya kawaida na hata akistaafu akiwa na hali ya kawaida, lakini wanaomzunguka kuwa matajiri wa kupindukia.   Tutahoji kwa nguvu zaidi iwapo hao wanaomzunguka hawakuwa matajiri mpaka huyo kiongozi alipochaguliwa.

Kiongozi anayeruhusiwa kuwa mfanyabiashara ni hatari kwa nchi kuliko jambazi. Huyu anapochaguliwa hawezi kutulia; kila atakapopata nafasi atatafuta pesa, kwa njia halali na hata zile ambazo zinaweka doa kwenye uadilifu wake.

Leo hii Tanzania tunahangaika na matatizo ya kila aina yaliyoletwa na jambo moja tu: viongozi kuruhusiwa kuwa wafanyabiashara. Na hili ni tatizo ambalo lipo kuanzia ngazi ya chini kabisa mpaka ya juu kabisa ya uongozi wa nchi yetu.

Kwanini hatujiulizi swali moja dogo tu ambalo halihitaji hata elimu ya darasa la saba? Kwanini ni lazima kiongozi awe pia mfanyabiashara? Kiongozi asipokuwa mfanyabiashara tutahatarisha usalama wa Taifa? Hapana.

Ukweli ni kuwa kuendelea kuruhusu ndoa kati ya uongozi na biashara kunaweza kuhatarisha usalama wa Taifa. Katika kashfa zote za fedha ambazo zimeikabili nchi kwenye serikali za awamu zote hutakuta mkulima au machinga kwenye orodha ya wanaotuhumiwa, ila kiongozi hakosekani au kajificha tu nyuma ya pazia.

Lakini walioruhusu hali hii watakwambia kuwa kutenganisha uongozi na biashara ni sera ya Ujamaa. Huu ni upuuzi. Wananikumbusha abiria wa ndege raia wa Kenya niliyekaa naye jirani aliyebaini nasoma kitabu cha hotuba za Mwalimu Nyerere. Aliniambia kuwa amesikia kuwa Nyerere aliharibu nchi kwa siasa ya Ujamaa.

Nilimwambia Kenya inatoa elimu ya bure mpaka ngazi ya sekondari. Nilimuuliza iwapo Kenya ni nchi ya kijamaa. Alisema hapana. Nilisema kuwa kuna mambo mengi ambayo kiongozi anaweza kuhusishwa nayo ambayo ni masuala ya busara tu, lakini kwa sababu tu serikali yake iliamua kuwa rasilimali za Taifa zimilikiwe na serikali kwa niaba ya wananchi, basi mambo yote iliyoyafanya yakahusishwa na sera za kijamaa. Nilimshauri asome mwenyewe na aache kuambiwa. Asiposoma mwenyewe, nilimwambia, ataambiwa yale yaliofanywa na Kenya na Korea ya Kusini ni busara lakini ya Mwalimu Nyerere ni siasa. Na hapa natumia neno siasa kama uamuzi usiofaa.

Mwalimu Nyerere alisema hata nchi za kipebari zina maadili ya uongozi. Wanaoamini kuwa tunaweza kuendelea kwa usalama kuwaruhusu viongozi wetu waendelee kufanya biashara au ni wale wanaofaidika na utaratibu huu, au ni wale ambao wanaunga mkono mfumo wenyewe kwa sababu za kiitikadi tu. Lakini kama tunataka kuzungumzia ukweli, hii hali inaitafuna nchi na siyo hali inayopaswa kuachwa iendelee.

Miaka ipatayo mitano iliyopita, Rais Kikwete akizungumza kwenye kilele cha mbio za Mwenge mkoani Tanga, alisema kuwa kuruhusu viongozi kuwa wafanyabiashara ni suala linaloleta mgongano wa kimaslahi. Najua Rais wetu ana kazi nyingi na suala hili linaweza kuwa limeshuka kwenye orodha ya umuhimu kwenye utekelezaji.

Lakini iwapo ana nia ya dhati ya kumuenzi Mwalimu Nyerere angerejea kwenye suala hili na kulitafutia ufumbuzi wa kudumu, siyo ndani ya CCM pekee bali kwa nchi nzima. Hapo tutakuwa tunamuenzi Mwalimu Nyerere wakati wote si wakati wa uchaguzi tu.