DAR ES SALAAM
Na Aziza Nangwa
Kwa kipindi cha cha mwaka mmoja Taasisi ya Mifupa ya Muhimbili (MOI) imefanikiwa kuwafanyia upasuaji wagonjwa 165 wa ubongo bila kupasua fuvu la kichwa.
Mafanikio hayo yamefikiwa baada ya Serikali ya Awamu ya Sita kuwekeza Sh bilioni 7.9 katika ujenzi wa maabara ya kisasa ya mashine ya Angio Suite yenye uwezo wa kuendesha upasuaji huo.
Pia mashine hiyo inawezesha matibabu ya damu iliyoganda katika mishipa ya miguu, uti wa mgongo na matatizo ya moyo.
Uwekezaji huo unaifanya MOI kuwa taasisi bora nchini na nje ya nchi katika matibabu ya kibingwa ya mifupa na matatizo ya mishipa na kuifanya kuwa kimbilio la wengi.
Tangu MOI wameanza kutoa huduma hiyo wamekuwa wakileta wataalamu kuja hapa nchini kuwafundisha madaktari bingwa wa taasisi hiyo kufanya kazi kwa haraka.
Huku ikibuni mikakati ya kuifanya huduma hiyo kuwa ya haraka na salama na walipoanzisha kambi wiki moja na madaktari bingwa kutoka India kuja kuungana na wataalamu wao.
Akizungumzia mafanikio hayo, Mkurugenzi Mtendani wa MOI, Dk. Respicious Boniface, anasema Angio Suite ni maabara kubwa na uwekezaji wake umeleta mageuzi makubwa katika sekta ya afya hapa nchini, hasa kwa wagonjwa wa mifupa na mishipa na umefanikiwa kwa asilimia 100.
“Hakuna maabara nyingine yenye vifaa vya kisasa kama hii iliyopo hapa MOI, hata katika nchi za ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
“Tunaishukuru serikali kwa uwekezaji wa vifaa vya kisasa sambamba na kuongeza wataalamu na wabobezi katika uendeshaji wa maabara hiyo,” anasema Dk. Boniface.
Vilevile anasema uwekezaji huo umepunguza gharama za safari kwa wananchi kama ilivyokuwa siku za nyuma wagonjwa walilazimika kusafiri nje ya nchi kufuata matibabu ya aina hiyo.
Anasema upasuaji wa mishipa ya ubongo unaofanywa kwa sasa na MOI unafanyika kupitia paja la mgonjwa na inatumia dakika 30 hadi 60 tu.
Akieleza hatua hiyo ya upasuaji kuwa ni tofauti na iliyokuwapo mwanzo kwa kuwa ilikuwa inawalazimu madaktari kumfanyia mgonjwa upasuaji kichwani kwa njia ya kupasua fuvu.
“Kwa sasa hatufungui fuvu la kichwa kama zamani, hatufanyi tena cerebral aneurysm, tunatumia mashine hiyo kuondoa uvimbe katika mishipa ya damu iliyopo katika ubongo wa mgonjwa na maeneo mengine ya sehemu za mwili,” anasema.
Dk. Boniface anasema kwa sasa mashine hiyo imekuwa mkombozi wa kuondoa msongamano wa wagonjwa wanaohitaji upasuaji wa ubongo.
Anasema upasuaji huo umerahisisha wagonjwa kukaa chumba cha uangalizi maalumu kwa wiki mbili na kuchukua muda mfupi na mgonjwa anakuwa na fahamu zake kabla na baada na unaweza kumhoji chochote na akakujibu tofauti na huko nyuma.
Pamoja na kuboreshwa kwa huduma hiyo, MOI kwa sasa inakabiliwa na wagonjwa wengi wanaotaka kutibiwa kwa msamaha kutokana na wagonjwa hao kutojiunga katika huduma ya bima ya afya.
Baada ya maboresho hayo, anasema idadi ya wagonjwa wanaofika MOI imeongezeka kutoka 500 kwa mwezi hadi kufikia 900 kwa sasa.
“Kabla ya maabara hii, mgonjwa mmoja akipelekwa nje ya nchi kutibiwa, matibabu yaligharimu Sh milioni 50 hadi 60, baada ya kufunga mashine hii hapa gharama imepungua hadi kufikia Sh milioni nne hadi tano,” anasema.
Kupitia maabara hiyo, anasema kwa sasa wagonjwa wenye matatizo ya mifupa na mishipa ya damu wana uhakika wa kupatiwa matibabu kwa njia salama na yenye uhakika kwa njia za kisasa.
Anasema uwezo wa mashine hiyo hauishii katika upasuaji wa mishipa ya ubongo tu, bali pia inatibu matatizo ya moyo, tumbo, miguu na tumbo kwa wanawake wenye matatizo ya uvimbe katika miili yao.
Anasema mashine hiyo ni kubwa na yenye uwezo wa kuratibu mifumo ya kitabibu katika magonjwa yote ya ubongo, mishipa na tumbo kwa wakati mmoja.
“Taasisi imekuwa na utaratibu wa kuagiza wataalamu kutoka nchi mbalimbali, ili kuwaongezea ujuzi madaktari wa ndani kwa sasa wameingia mkataba na Hospitali ya Ramaiya iliyopo nchini India.
“Lengo la kuwaleta madaktari hao na kuingia nao mkataba ni kuwawezesha wataalamu wetu wa ndani wajifunze zaidi kutumia Angio Suite,” anasema.
Pia anasema katika mkataba huo watakuwa na mabadilishano ya wataalamu mara kwa mara ili kuongeza ufanisi zaidi.
Anasema kwa sasa wanahudumia wagonjwa watano hadi sita kwa siku, na kwa mwaka wanahudumia wagonjwa 50 hadi 60.
“Kwa kweli lazima tuipongeze Serikali ya Awamu ya Sita kwa kufanikisha uwepo wa mashine hii hapa nchini kwa sababu lengo la serikali ni kufikisha huduma za matibabu yote ya kibingwa na yenye ubobezi yanapatikana nchini.
“Kambi hiyo imejumuisha madaktari kutoka nchini India ambao wamekuja maalumu kwa ajili ya kuwafundisha wazawa namna ya kutumia mashine ya Angio Suite, na kwa muda mfupi wamewafanyia watu wanne wiki moja,” anasema.
Pia anasema wataalamu kutoka sehemu mbalimbali duniani wanapofika MOI na kuiona Angio Suite wanawasifia, wanasema ipo Tanzania na Afrika Kusini tu.
Mikakati ya MOI
Dk. Boniface anasema wanalenga kutoa mafunzo ya mara kwa mara kwa madaktari wake wa ndani na nje ya nchi watakaokidhi utoaji wa huduma ya matibabu kulingana na idadi ya wagonjwa.
Anasema kwa sasa wanajiandaa kwa awamu nyingine ya nne ya ujenzi wa kituo kipya cha kisasa kitakachokuwa na wataalamu waliobobea kutoa huduma za afya kwa njia za kisasa.
“Hiki kinatarajiwa kujengwa eneo la Mbweni na kinatarajiwa kuzalisha wataalamu wengi wakishirikiana na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Muhimbili (MUHAS),” anasema.
Aidha, anasema mafunzo hayo yataenda sanjari na kufundisha wataalamu waliopo namna ya kuitengeneza mashine hiyo itakapoharibika.
Anajivunia MOI kuwa sehemu ya chuo kinachotoa mafunzo kwa sababu madaktari kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika watanufaika na mafunzo hayo.
Anasema kituo hicho cha Mbweni kitakuwa na uwezo wa kulaza wagonjwa 150 na wagonjwa wa nje zaidi ya 500 wakitarajia kupata matibabu hapo kila siku.
“Kituo hiki kitaendesha tiba kwa njia ya mazoezi, naishauri serikali kutoa fursa kwa wawekezaji kutengeneza vifaa tiba ndani kwa sababu vilivyopo vinapatika nje ya nchi na vinauzwa bei ghali,” anasema.
Anasisitiza uwekezaji mkubwa ufanyike katika dawa ili zizalishwe hapa nchini na kuipa unafuu serikali kuacha kuagiza kutoka nje ya nchi.
Akiizungumzia mashine hiyo, Mkuu wa Kitengo cha Angio Suite, Dk. Nicephorus Rutabasibwa, anasema mashine ya Angiography ni muunganiko wa mashine zaidi ya moja na ndiyo unaleta jina la Angio Suite.
“Hii ina uwezo mkubwa wa kufanya upasuaji wa mifupa na mishipa ya ubongo na inahusisha chumba, mashine ya dawa ya usingizi na zote zinaunganishwa katika kompyuta.
“Kupitia mashine hii daktari ana uwezo wa kuangalia na kuona kwenye mishipa ambayo ipo kwenye ubongo, uti wa mgongo, moyo, figo na sehemu zingine za mwili,” anasema Dk. Rutabasibwa.
Anasema mashine hiyo imerahisisha uwezo wa daktari kugundua tatizo la mgonjwa liko wapi, lina sura gani na linatibika kwa namna ipi iliyo haraka.
Kwa kutumia mashine hiyo, anasema wanapobaini ugonjwa upo katika figo, moyo, ubongo au maeneo mengine ya mwili, upasuaji hufanyika kupitia mshipa mkubwa (femoral artery).
Anayataja magonjwa ya ubongo yanayotibika kuwa ni pamoja na uvimbe katika mishipa ya damu na uzibuaji huo unafanyika kwa urahisi.
Mengine yanayotibika kwa mashine hiyo ni uti wa mgongo, kuziba matobo yaliyo wazi katika mishipa ya moyo, uvimbe katika maini, figo na maeneo mbalimbali ya mwili.
Pamoja na kuboreshwa kwa huduma hiyo, anasema bado wapo watu wanaoyapuuza maumivu katika sehemu zao za mwili, hivyo kuendelea kukaa nyumbani badala ya kufika hospitalini kupata matibabu.
“Watu wasingoje tatizo liwe kubwa, na ili kuepuka madhara kuwa makubwa wanaojihisi kuwa na matatizo waje tuwape huduma hapa,” anasema.
Naye Muuguzi Mkuu na Msimamizi wa Usalama wa mashine hiyo, Juma Rehani, anasema Angio Suite inafanya kazi ya upasuaji kwa usalama wa hali ya juu.
“Wajibu wangu humu ni kuhakikisha kabla ya upasuaji ninakagua mashine na vifaa na kujiridhisha kama vyote viko sawa,” anasema Rehani.
Anasema safu anayofanya nayo kazi katika maabara hiyo ni wauguzi, madaktari waliobobea, watu wa mionzi, wataalamu wa kusoma picha na wataalamu wanaotoa dawa za usingizi.
“Kazi yangu ni kusimamia mgonjwa anaingia salama na kutoka salama katika chumba cha upasuaji,” anasema Rehani.