Desemba 6, 2012 Gazeti JAMHURI linatimiza umri wa mwaka mmoja. Mwaka mmoja si kipindi kirefu, lakini kwa uhai wa chombo cha habari, hasa katika mazingira ya nchi yetu, ni kipindi kirefu mno.
Tunawashukuru sana wote waliojitokeza kutuamini, kututia moyo na kutuunga mkono katika azma yetu ya kuanzisha chombo hiki. Tulianzisha Gazeti hili tukiamini kuwa tunaingia kwenye ushindani mkali sana kutokana na ukweli kwamba Tanzania ni moja ya nchi chache kabisa katika Afrika zenye vyombo vya habari, hasa magazeti, kwa wingi.
Wakati tukianza kuitekeleza dhima hii, wapo waliotukatisha tamaa. Lakini tukiri kuwa hao walikuwa wachache. Wengi walitutia moyo, na kwa hakika tunadhani nasaha na maombi yao vimetuwezesha leo kuadhimisha mwaka mmoja.
Kama tulivyosema kwenye toleo letu la kwanza lililotoka Desemba 6, 2011; dhima yetu kuu ni kulitumikia Taifa letu kwa uadilifu na weledi kadiri tuwezavyo. Tuliahidi kutofungamana na upande wowote wa wanasiasa au wafanyabiashara. Tuliahidi kutomwonea mtu wala kumbemba mtu kwa kukitumia chombo hiki. Tuliahidi Jamhuri liwe Gazeti ambalo kila Mtanzania anaweza kujivunia kulisoma.
Ni ukweli ulio wazi kwamba ahadi hizo tumeweza kuzitekeleza kwa kiwango cha juu sana. Kinachofurahisha ni kwamba hatujapata malalamiko ya upendeleo au ya kuwasafisha baadhi ya watu. Msimamo huo tunaendelea nao maana wasomaji wengi wanataka iwe hivyo.
Wakati tukianzisha Gazeti hili wapo watu tunaoweza kuwaita wapuuzi waliojaribu kutuhusisha na makundi ya wanasiasa. Wapo waliodiriki kusema Jamhuri limeanzishwa na baadhi ya wanasiasa kwa ajili ya maandalizi yao ya kuingia Ikulu. Kwa bahati nzuri wasomaji wameweza kujiridhisha pasi na shaka kwamba maneno hayo yalikuwa na yanaendelea kuwa uzushi na uzandiki.
Bahati mbaya ni kwamba katika Tanzania, hata kama mtu akiwa na umri wa miaka zaidi ya 35 (kama tulivyo sisi waanzilishi wawili wa Jamhuri), bado ataonekana kuwa hawezi kufanya kitu hadi abebwe. Hii ni dhana potofu. Lazima tujifunze kuthubutu. Kwetu sisi tumethubutu na kwa hakika tumeona inawezekana. Wahenga walisema, “Penye nia pana njia”.
Ndani ya mwaka mmoja kampuni ya Jamhuri Media Limited imeonesha dalili njema za kukua. Mafanikio haya yasingepatikana kama si kuungwa kwetu mkono na wasomaji na watangazaji. Ndani ya mwaka mmoja watu kadhaa maarufu wamezuru ofisi zetu na kutupatia ushauri mbalimbali wenye lengo la kututia moyo na kuboresha kazi zetu. Kwao wote, tunasema asanteni sana.
Tunachukua fursa hii kuwashukuru kwa namna ya pekee wasomaji na watangazaji wote. Wengine bila kujali uchanga wetu, walituunga mkono kwa dhamira ya kuona tunapata nguvu za kujiimarisha na kusonga mbele. Mchango wa wasomaji na watangazaji ni mkubwa mno, kiasi kwamba hatuna maneno sahihi ya Kiswahili ya kuwashukuru zaidi ya kusema, “Asanteni sana sana sana!” Tunawaomba muendelee kutuunga mkono.
Ahadi yetu ni kuendelea kuitumikia Tanzania na Watanzania kwa mujibu wa maadili ya taaluma ya uandishi wa habari. Kama tulivyosema kwenye toleo la kwanza, tunarejea kusema kuwa kwetu sisi Tanzania na Watanzania ni zaidi ya kila kitu. Tunashirikiana nanyi kulijenga Taifa letu na kuhakikisha rasilimali za nchi yetu zinawanufaisha Watanzania wote.
Tunahitimisha shukrani zetu kwa kuowamba wasomaji na watangazaji wote nchini kuendelea kutuunga mkono. Tumedhamiria kuwathibitishia walimwengu kuwa tumethubutu, tunaweza.
Mungu Wabariki Wasomaji na Watangazaji,
Mungu Ibariki Tanzania,
Mungu Ibariki Afrika.
Asanteni sana.