Ndugu Rais, tunakutana hapa kwa mara ya kwanza leo siku ya tatu ya

Mwaka huu Mpya wa 2017. Nawatakia wasomaji wangu wote na wote wenye mapenzi mema, heri na baraka ya Mwaka Mpya, uwe mwaka wa mafanikio kwenu na Mwenyezi Mungu awatimizie matamanio yenu.

 Yaliyotusibu mwaka 2016 tunayajua yote, ila kwa sasa itoshe tu kusema mwaka 2016 umetuachia mashaka mengi mno. Tunayo matamanio mengi kwa mwaka mpya lakini yaliyoandikwa juu yetu kwa mwaka huu 2017, yako katika bahasha iliyofungwa.

 Yatafunguliwa polepole kwa kipindi cha miezi kumi na mbili mtawalia. Wanadamu tuna mipango yetu lakini makusudi ya Yeye aliye juu si lazima yaendane na mipango ya wanadamu. Tumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kuuanza mwaka huu mpya kwa pamoja.

Ndugu Rais, kwa pamoja tuyainue macho yetu juu, tuzigeuze shingo zetu ili tupate kuitazama milima kule tulikotoka 2016 kisha tujiulize, tumewaachia nini watu wa Mungu kwa mamlaka tuliyopewa? Kama tumewaachia faraja na matumaini huko ndiko kubarikiwa kwetu. La, tumewaachia mashaka na kukata tamaa; huo ndiyo utakuwa, ole wetu.

Hukumu yake itakuwa juu ya vichwa vyetu. Na mwisho wetu utakuwa mchungu kuliko shubiri nasi tutayajutia mamlaka tuliyoyapewa. Ndugu Rais, mwaka 2016 umeisha nchi yetu bado haina dira. Hali hii ni ya kusikitisha sana kwa maana kukosa dira ni kukosa mwelekeo.

 Kama nchi haina dira ni nani anaweza kusema kwa haki kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imefanya nini kuelekea wapi? Tumekuwa kama ni watu wa kujaribu hiki na kukiacha na kisha kujaribu kingine.

 Tukiendelea hivi Uchaguzi Mkuu mwaka 2020 utatukuta bado tunajaribu. Wananchi watatupuuza. Lengo la utawala bora na sifa kuu ya utawala unaofaa ni kuwalinda na kuwastawisha watawaliwa.

 Kiongozi anayechaguliwa na wananchi atakuwa na busara pale tu atakapoelewa kuwa jukumu lililo bora kwake ni kuwatengenezea wapiga kura wake jamii yenye upendo, umoja na mshikamano. Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ametuachia mfano mwema wa utawala uliotukuka. Aliijenga jamii yetu katika upendo, umoja na mshikamano. Na hapo ndipo amani ya kweli hutamalaki.

Kiongozi asiyecheka, akaongoza nchi kwa kufuata mstari huku akizingatia sheria za nchi na kuiheshimu Katiba, hupendwa na watu wake kwa miaka mingi kama Edward Moringe Sokoine anavyopendwa mpaka leo.

Bali kiongozi mbabe, mtishi, aliyejaa vitisho na kujidai, hujibomoa mwenyewe kwa kiburi chake kama akina Idi Amin walivyojibomoa. Zinapotokea habari kuwa Mkuu wa Mkoa wa Singida, Rehema Nchimbi, ametengua uamuzi wa waziri na kuamua mnada wa wananchi uendelee walio makini hutafakari.

 Uamuzi wa mkuu wa mkoa huyu, unaonesha kujali wananchi na kuonesha upuuzi wa baadhi wa viongozi wetu. Kama Rais hakumpongeza wananchi tunampongeza.

Rais wangu, nina imani kubwa na washauri wa Rais wetu, lakini hii haiondoi ukweli kwamba mshauri namba moja na wa muhimu kuliko washauri wote wa Rais yeyote duniani, ni Rais mwenyewe kwa maana halazimiki kukubali ushauri wowote hata kama ushauri huo ni dhahabu tupu. Na hii ndiyo maana ya lile neno kuwa Rais wa kweli ni lazima awe mwenye fikra zilizo juu ya washauri wake.

Ndugu Rais, tumeufunga mwaka 2016 lakini zogo la ununuzi wa ndege

nyingi mpya limekataa kufungwa pamoja nao. Nia njema na nzuri ya Rais wetu ya kukazania ndege tusikubali ipotoshwe na watu wachache wasiomtakia mema.

 Lakini na maneno yanayotoka katika vifua vya Watanzania wenye nia njema pia, yasipuuzwe hata kidogo. Hapa inatakiwa elimu kwa wote. Mfano ni huu ujumbe;

“Mwalimu mkuu makala yako imenigusa sana. Mwanangu alikosa nafasi Form V. Nikampeleka Shule ya CCM (Sangu Mbeya), sasa amenyimwa mkopo elimu ya juu kisa kasoma ‘private’. Kwangu hitaji langu si ndege ila mwanangu asome.”

Baba mimi mwenyewe ni mstaafu wa TTCL. Wastaafu wengine wanapolipwa pensheni ya laki moja kama Bunge lilivyoagiza lakini sisi wa TTCL bado tunalipwa Sh. 50,000 tukiambiwa Serikali haina fedha, halafu wewe baba uje na mabilioni uliyotumia kununua ndege; jiweke katika nafasi yangu, utanielewaje?

 Tusikimbilie kuwalaumu wanaolaumu

Ndugu Rais, biashara ya ndege ina historia ndefu katika kumbukumbu za ulimwengu huu. Ulikuwapo wakati Waethiopia waliwahi kuishi kwa kutegemea uchumi wa nchi yao uliojengwa kwa kutumainia ndege zake. Kwa miaka mingi Shirika la Ndege la Ethiopia (Ethiopia Airlines) lilikuwa mfano wa kuigwa si tu katika bara la Afrika bali pia hata duniani.

Tulifurahia sana kusafiri na ndege hizo katika miaka ya 1990; lakini mara ya mwisho niliposafiri na ndege hizo mwanzoni mwa mwaka jana, hadhi yake ilikuwa tofauti sana. Shirika kwa ujumla limechoka.

Ndugu zetu wa Kenya na Kenya Airways yao na hasa walipoungana na Shirika la Ndege la Ujerumani walitamba sana angani. Leo Shirika la Ndege la Kenya linadai kupata hasara kubwa zaidi kila mwaka unaofuata.

Kuna mgogoro wa kutaka kupunguza wafanyakazi. Baba, kununua ndege kuna ubaya gani? Lakini tunanunua ndege katika mazingira gani? Jumuiya ya Afrika Mashariki ilipovunjika wengine tulikuwa ni wafanyakazi wa jumuiya hiyo. Air Tanzania kama nakumbuka vizuri ilianza na ndege saba. Baba, waliishakwambia, ziko wapi?

Tusiulize majina yao, lakini ndiyo hawa hawa waswahili utakaowakabidhi hizo ndege waziendeshe? Mara ya mwisho kuziona ndege zetu za iliyokuwa Air Tanzania ni pale wananchi walipoambiwa kuwa kuna ‘wasauzi’ wanataka kuunganisha ndege zao na zetu. Kama walifanikisha au vinginevyo, lakini tokea siku hiyo hakuna Mtanzania hata mmoja aliyewahi kuuona japo ubawa au tairi ya iliyokuwa Air Tanzania.

 Kwa hiyo, baba hizi ndege basi. Kati ya waliokunywa Faru John kama walikunywa, na waliokunywa ndege zote hizi nani zaidi? Tuwaache waendelee kutamba na tuwaongezee nyingine?

Ndugu Rais, uliposhika nchi uliwaambia Watanzania kuwa kila ulipogusa palikuwa jipu. Nchi ilikuwa imeooza. Ukaja ukasema tena vizuri zaidi kuwa unataka kuinyosha nchi. Je, kununua ndege si kuijenga nchi kabla haijanyooka?