Nitumie wasaa huu kumimina salamu nyingi za Krismasi kwa wasomaji wetu. Ni jambo la kumshukuru Mungu kuona kuwa tunaelekea ukingoni mwa mwaka 2012 na kujiandaa kuuanza mwaka 2013.

Ninapenda kuwashukuru wote ambao mmekuwa mkifuatilia safu hii na zaidi sana kwa kusoma gazeti letu hili JAMHURI, ambalo wakati wote tumethibitisha kuwa tunaanzia wanapoishia wengine.

 

Wapo wasomaji ambao wananifahamu tangu zamani (kwa maana ya makala zangu) nikiwa naandikia magazeti ya Rai na Tazama. Hata hivyo, wapo wasomaji ambao wamenifahamu karibuni kupitia gazeti hili.

 

Wakinga tuna msemo usemao ukimfahamu aliyekanda mkate, ni rahisi kuuamini mkate huo na utamu wake huongezeka. Kwa muda sasa nimejikita katika uchambuzi wa masuala ya kujitambua, ujasiriamali, biashara, uchumi na uwekezaji.

 

Ingawa mara kadhaa huwa naleta uzoefu na utambulisho kuhusu mimi; kupitia mifano na maelezo ndani ya makala zangu; leo naona ni busara nikajitambulisha kwa kinagaubaga kwa wasomaji wetu. Naamini kuwa ukinifahamu mimi mkanda mkate wa “Anga za Uchumi na Biashara”, itaongeza utamu wa safu!

 

Januari 10, 2013 nitakuwa ninatimiza umri wa miaka 26 na kuanza ngwe ya mwaka mwingine wa 27. Umri huu si haba, kwa sababu kimahesabu ni kuwa tayari nimeshaishi robo karne na nimeanza kuifukuzia nusu karne! Kuandika kupo kwenye damu na ni kipaji ambacho, licha ya kupita katika mabonde mengi, lakini hakikuweza kufutika.

 

Niliandika makala yangu ya kwanza nikiwa na miaka 19, nilipokuwa kidato cha tano, kwenye gazeti la Rai. Makala hiyo naikumbuka sana ilikuwa na kichwa, “Tumekiuka kanuni, sasa majibu yanatugomea.” Kwa maana hiyo utaona kuwa nimekuwa katika uandishi wa makala kwa miaka minane mfululizo hadi sasa.

 

Shukrani za pekee ninazipeleka kwa mwalimu aliyenihamasisha na kunifundisha uandishi wa makala, ndugu Markus Honorius Mpangala.  Huyu ni nguli wa uchambuzi wa masuala ya kimataifa na ameendelea kuwa karibu nami akinielekeza na kuninoa zaidi. Hivi nilivyo kiuandishi ni matokeo ya juhudi zake kwangu. Mungu ambariki sana!

 

Awali nilikuwa nikiandika makala mchanganyiko hasa makala za siasa na saikolojia.  Baada ya kujiunga na chuo kikuu kusomea shahada ya mambo ya Uchumi na Biashara, ndipo nilipoanza kuandika makala za biashara na uchumi. Tangu wakati huo hadi sasa nimejikita zaidi katika uchambuzi wa makala kwenye eneo hili ukilinganisha na maeneo mengine.

 

Mbali na kuwa na ujuzi wa uchumi na biashara kutoka darasani, lakini uandishi wangu wa makala za ujasiriamali na biashara unachagizwa na mimi kupenda, kufanya na kuhusudu sana biashara na ujasiriamali. Sehemu kubwa ya chambuzi zangu huwa nazitoa ama kutoka uzoefu wangu binafsi, ama kutoka kwa watu wengine wanaofanya biashara na ujasiriamali kwa vitendo.

 

Nilianza biashara yangu ya kwanza nikiwa na umri wa miaka 21, kwa kutafuta mtaji kwa jasho langu mwenyewe. Wale waliofuatilia safu hii tangu mwanzoni mwa mwaka huu, bila shaka wanakumbuka maelezo ya namna nilivyofanya biashara ya kuchuuza vitunguu kule Karatu, Arusha.

 

Vile vile mtakumbuka nilivyoeleza namna nilivyofanikiwa kukua kimtaji, hadi kuanzisha chuo cha mafunzo ya kompyuta na biashara kule Mufindi na kisha kufilisika kabisa ndani ya muda mfupi. Nimekuwa nikiwapa funzo kubwa wajasiriamali wadogo na wakubwa kuhusu uzoefu wangu katika kufanikiwa na kuanguka.

 

Mara zote ukianzisha biashara bila kuwa na maono makubwa na yanayopanuka; basi anguko lako halipo mbali. Nimeanzisha, kufanikiwa na kuanguka kwenye biashara kadha wa kadha, ikiwamo biashara ya kumiliki magari ya abiria; lakini kwenye kufilisika kwa mwanzo (biashara ya chuo) tatizo lilikuwa ni ukosefu wa maono makubwa na yanayopanuka.

 

Nilijikuta nimezikamata milioni nikiwa bado kijana mdogo wa miaka 22 na ukizingatia kuwa chuo nilichoanzisha kilikuwa ni cha kwanza katika jimbo zima, basi nililewa mafanikio hayo kiduchu! Kilichofuata? Sikujua pa kuelekea kwa maana ya kukuza biashara, nikadhani nimeshafika! Hapo ndipo nilipodondokea. Hilo nalo likawa ni moja ya mafunzo katika ‘kitabu cha kujifunza kupitia kujaribu na kushindwa.’

 

Tunapoelekea kuuanza mwaka 2013, ninawashauri wajasiriamali na watu wengine wote kupanga malengo. Malengo bora ni yale unayopanga na kuyaandika. Bahati mbaya sana idadi ndogo ya Watanzania ndiyo wanaopanga malengo katika maisha; na katika hiyo idadi ndogo, wanaopanga malengo kwa kuandika ni wachache mno. Malengo yaliyopo kichwani kwako tu, tunayaita ni matakwa (wishes) na kutimia kwake hakuna ‘guarantee’.

 

Ukiachilia mbali malengo, kuna kitu kikubwa zaidi kiitwacho maono (vision). Maono ni picha kamili kuhusu maisha yako ya baadaye katika maeneo yote –  kiuchumi, kifamilia, kiroho, kijamii na kadhalika. Mtu binafsi ndiye anayeamua nini anataka kitokee ama aweje hapo baadaye.

 

Unapokuwa katika biashara, unatakiwa uwe na maono kuhusu biashara yako itakavyokuwa kwa mwaka mmoja, miaka mitano 5, 10, 20 hadi 50 ijayo. Kuwa na maono kutakusaidia kupima nguvu unayoiweka katika biashara zako ukilinganisha na kule unakotaka ufike. Ieleweke kuwa malengo huwa yanapangwa kwa kuzingatia maono uliyonayo.

 

Ni wakati wa wafanyabiashara kuachana na vimaono vidogo vidogo, badala yake tujaribu kuwa na maono makubwa. Sifa ya maono mazuri ni yale ambayo yanakupa hamasa ya kupambana wakati wote na ambayo kila unapopiga hatua unajisikia fahari.

 

Mwaka huu unapoanza, moja ya malengo yangu ni kuvumbua, kubainisha na kushirikisha fursa mbalimbali za kibiashara na kiuwekezaji kwa Watanzania wengi kwa kadiri niwezavyo. Lengo hili linatokana na maono niliyonayo kwa muda mrefu ya kuwasaidia Watanzania wengi kupata uhuru wa kiuchumi na kifedha (financial freedom).

 

Nimekuwa nikikazana kutoa elimu, ujuzi, uzoefu na maarifa yanayolenga kuwafanya watu wakombolewe kiuchumi kupitia njia mbalimbali. Nimekuwamo gazetini mwaka mzima, karibu kila wiki (isipokuwa kwa wiki mbili); nimekuwa nikiandika katika blogs na katika mitandao ya kijamii ikiwamo Facebook.

 

Ukiacha hilo, nimekuwa nikikutana na kutoa ushauri, nasaha na hamasa kwa makundi mbalimbali ya watu wenye kiu ya kuwa na uhuru wa kiuchumi na kifedha. Kwa kuwa kila mwisho wa mwaka ni wajibu wa kila anayekuwa na malengo, kufanya tathmini ya mafanikio ya utekelezaji wa malengo.

 

Nami pia kwa lengo hili la kushirikisha fursa; nina ujasiri wa kusema kuwa nimefanikiwa kwa sehemu kubwa. Hata hivyo, nina changamoto kubwa hasa ninapoyatazama maono niliyonayo. Kwa maana hii, mwaka 2013 nina malengo makubwa zaidi ya niliyokuwa nayo mwaka huu wa 2012.

 

Wafuatiliaji wa safu hii ni mashahidi kuwa nimefanya juhudi kubwa kuwasilisha na kushirikisha fursa mbalimbali. Ninafurahi sana kuona kuwa wapo Watanzania wengi ambao walichangamkia fursa mbalimbali. Nimepata wasaa wa kushirikiana na wadau hawa moja kwa moja ujuzi na uzoefu nilionao. Nimejifunza mengi kutoka kwao.

 

Mojawapo ya fursa nilizozishirikisha kwa uzito sana ilikuwa ni uwekezaji katika mashamba ya miti. Niwapongeze wasomaji na Watanzania ambao walichukua hatua ya kuidaka fursa hii. Nafahamu kuwa makumi ya Watanzania wengine wanajiandaa kuwekeza katika kilimo hiki. Kwangu mimi ni faraja na fahari kubwa ninapoona wengine wakifanikiwa katika eneo hili la kiuchumi.

 

Ili kurahisisha taarifa za uwekezaji hasa katika kilimo na ufugaji, kampuni ya biashara ambayo mimi ni mwasisi na mmiliki mwenye hisa nyingi kupitia kitengo cha Fresh Farms (T), tuko katika hatua za mwisho kukamilisha tovuti itakayobeba taarifa na msaada wa uwekezaji katika maeneo hayo. Tovuti hii ambayo inatazamiwa kuwa hewani kuanzia leo, ipo katika anuani ya www.freshfarmstz.com.

 

Ninaamini kwamba wasomaji mtaendelea kuifuatilia safu hii pamoja na gazeti hili kwa ujumla katika mwaka 2013. Pia wale wanaohitaji kuagiza vitu mbalimbali nje ya nchi yakiwamo magari wasisite kuwasiliana nami; kwani kampuni ninayoiendesha imedhamiria kuwasaidia wajasiriamali na Watanzania wengine wanaotamani kuagiza bidhaa mbalimbali nje ya nchi.

 

Mwisho niwatakie sikukuu njema na uwajibikaji mwema. Watanzania tunahitaji ushindi mkubwa kiuchumi mwaka 2013.

tel: 0719 127 901