Kocha wa Timu  ya Soka  ya Mwadui ya mkoani Shinyanga, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’, ametamba kwamba timu hiyo itakuwa bora katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara kuliko zote zinazoshiriki.

Akizungumza na JAMHURI hivi karibuni,  Julio amesema kuwa timu hiyo itatoa upinzani mkali kwa timu za Simba,  Yanga  na Azam FC.

“Simba na Yanga hakuna mpira pale bali kuna makelele, niliwahi kufundisha timu ya Kajumulo, sikuwahi kufungwa na Simba wala Yanga na hata sasa nikifanya usajili wangu hakuna timu ya kunifunga kati ya timu hizo,” amesema Julio na kuongeza:

“Mwadui ni timu kubwa, ipo tangu zamani. Unapozungumza timu ya Mtibwa ni ndogo kiumri kwa Mwadui, Prison, Azam zote ni za siku hizi,” amesema.

Amesema Mwadui ilipotea katika ulimwengu wa mpira kutokana na kukosa watu wanaopenda mpira katika eneo la mgodi huo wa Mwadui.

Amesema kwa sasa wamejitokeza watu wanaopenda mpira na kuamua kuwekeza katika timu hiyo, hivyo watarajie mazuri kutoka kwake.

Julio, kocha mwenye maneno mengi na tambo nyingi, amesema kwamba mbali na Simba na Yanga hata Bingwa wa sasa, Timu  ya Azam, ikae chonjo. Anatambua kwamba Azam FC ni timu tajiri, lakini haiwezi kushinda utajiri wa timu yake ya Mwadui.

“Hii timu inamilikiwa na Wazungu wanaouza almasi duniani kote, wanataka timu yao ifanye vizuri ili tutangaze biashara yao kama ilivyo kwa Azam  ambayo bidhaa zake nyingi zinaishia hapa Tanzania tu, hivyo kuna kazi kubwa ya kufanya,” amesema Julio.

Amesema anachosubiri kwa sasa ni kuushauri uongozi wa timu hiyo kuandaa bajeti nzuri kwa ajili ya usajili bora.

Azam ilianzishwa mwaka 2007 kama timu ya wafanyakazi wa kampuni ya SSB ambao waliuchukulia mchezo huo kama sehemu ya  kujiburudisha.

Azam FC aliingia Ligi Kuu mwaka 2008/2009 na kumaliza ikiwa nafasi ya nane. Msimu uliofuata Azam ilijiimarisha zaidi na kumaliza ligi ikiwa nafasi ya tatu.

Kwa sasa Azam ni mabingwa wa soka nchini baada ya kuwavua waliokuwa mabingwa wa ligi hiyo, Yanga.

Mwadui, inayotumia Uwanja wa Kambarage, Shinyanga, ni moja ya timu kongwe nchini, sasa imeanza kufufua matumaini mapya.

Miaka 13 imepita tangu mji wa Shinyanga kushuhudia michezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara na sasa faraja imekuja baada ya Stendi United na Mwadui kupanda rasmi daraja na kucheza ligi hiyo.

Stendi imefanikiwa kupanda daraja baada ya kupata pointi za “mezani” kutokana  na rufaa iliyokatwa dhidi ya Timu ya Kanembwa JKT,  hivyo kupata  pointi tatu na mabao mawili.

Stendi United ilikuwa ikigombea nafasi ya kupanda daraja katika kundi C ikiwa na pointi 26.

Mwadui  ilipanda daraja baaada ya kuifunga timu ya Polisi Dodoma mabao 2-1, ushindi huo umekifanya kikosi hicho kuwa na pointi 31 ambazo hazikufikiwa na timu yoyote katika kundi lake.

Kwa upande wao, Stendi United wamepanda daraja baada ya  kuifunga timu ya Toto African kwa mabao 2-0, matokeo ambayo yaliifanya Stendi United kufikisha pointi 29 na baada ya kusikilizwa na kukubaliwa rufaa yao walifikisha pointi 32.

Timu hizo zimeungana na Ndanda FC ya Mtwara na Polisi Morogoro kuingia katika Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao.