Hivi karibuni kumezuka vurugu baina ya Wakristo na Waislamu katika mji wa Tunduma mkoani Mbeya, wakigombea uchinjaji mifugo ingawa siku zote Waislamu ndiyo wamekuwa wakitekeleza jukumu hilo.

Vurugu hizo zilianza siku chache baada ya Wakristo wanaomiliki bucha za nyama kuiandikia barua Serikali, kuomba kibali cha kuruhusiwa kuchinja mifugo badala ya kuwategemea Waislamu.

 

Hata hivyo, Serikali ya Wilaya haikuwapa kibali hicho kwa maelezo kwamba suala hilo ni la kitaifa, huku ikiwataka wawe wavumilivu wakati likiendelea kutafutiwa ufumbuzi.

 

Vuguvugu hilo lilianza Machi 28, mwaka huu, baada ya Wakristo kupeleka barua yao serikalini, lakini kutokana na Sikukuu ya Pasaka hawakupewa majibu, hivyo kujiamulia kujichinjia mifugo.

 

Kutokana na hali hiyo, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Momba, ilikutana na viongozi wa Kikristo na Kiislamu kutafuta suluhu ya mvutano huo, lakini walishindwa kufikia mwafaka, hali iliyoilazimu Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Mbeya, ikiongozwa na Mkuu wa Mkoa, Abbas Kandoro, kuingilia kati.


Katika mkutano huo, baadhi ya Wakristo walikubali ushauri wa kuendelea kuvuta subira ikiwa ni pamoja na kuendelea kudumisha amani na utulivu katika mji huo.

 

Kamati hiyo iliwaomba viongozi wa pande zote pamoja na wananchi kwa jumla, kuangalia masuala yanayotakiwa na imani zao, hususan katika suala la chakula ili kudumisha amani wakati Serikali inashughulikia.


Hata hivyo, siku moja baada ya uamuzi huo, vurugu kubwa zilizuka kuanzia saa 4:30 asubuhi, baada ya baadhi ya watu kuanza kuchoma matairi na kufunga barabara, hivyo kusababisha wakazi wa mji huo kulazimika kufunga shughuli zao kwa zaidi ya saa 10, hali iliyosababisha Jeshi la Polisi kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya waandamanaji.

 

Katika vurugu hizo, askari mmoja na raia mmoja walijeruhiwa huku jingo la msikiti likiharibiwa milango na madirisha.

 

Watu zaidi ya 50 walikamatwa huku Diwani wa Kata hiyo kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Frank Mwakajoka, na Mchungaji wa KKKT  Tunduma,  Neema Mwamafupa, kutafutwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kuhamasisha watu kushiriki  vurugu hizo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Diwani Athumani, aliwasihi wananchi kuacha vurugu hizo akisema zinachochewa kisiasa.


Lakini suluhisho pekee la kuondoa vurugu hizi hapa nchini, ni Serikali kuruhusu mashine maalumu za kuchinja mifugo katika maeneo korofi na yanayochochea vurugu za kidini. Umuhimu wa mashine hizo unatokana na kufungwa kwa mitambo maalumu itakayokuwa ikiendeshwa kwa umeme, hivyo kuondoa hofu ya uvunjifu wa amani na utulivu.

 

Chanzo cha vurugu hizo inaelezwa kuwa ni maslahi kwa baadhi ya Waislamu wanaohusika katika uchinjaji mifugo. Watu 45 wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Mbozi, wakituhumiwa kuhusika katika vurugu hizo.


Kamanda Athumani amethibitisha kufikishwa mahakamani kwa watuhumiwa hao, na kuongeza kuwa katika vurugu hizo jumla ya watuhumiwa waliokamatwa ni 94 akiwamo Mchungaji wa KKKT, Neema Mwamafupa, na Diwani wa Kata ya Tunduma, Frank Mwakajoka (CHADEMA). Upelelezi kuhusu watuhumiwa 49 unaendelea, wakiwa nje kwa dhamana.

 

Kamanda Athumani amesema kesi ya washitakiwa hao imepangwa kusikilizwa mahakamani hapo Aprili  18, mwaka huu, ikiwa ni kesi ya jinai namba 71/2013.

 

Amesema utulivu na usalama vimerejea Tunduma wiki iliyopita, na kwamba wananchi wanaendelea na shughuli zao kama kawaida.

 

Diwani wa Kata ya Tunduma Mwakajoka aliamua kujisalimisha katika Jeshi la Polisi, baada ya kupata taarifa za kuwa alikuwa akitafutwa kwa tuhuma za kufanya vurugu hizo.


Kamanda wa Polisi anaendelea kutoa wito kwa wananchi wa Mji wa Tunduma na Mkoa wa Mbeya pamoja na viongozi wa dini na wanasiasa, kuendelea kuhimiza amani ambayo ndiyo msingi wa maendeleo ya Taifa lolote duniani.


Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro, amewataka wananchi kuwa wavumilivu katika kipindi hiki ambacho Serikali ngazi ya Taifa, inashughulikia mgogoro huo, huku akiwataka Waislamu kuendelea kuchinja mifugo kama ilivyozoeleka.

Hata hivyo, maagizo hayo ya Mkuu wa Mkoa yameonekana kuungwa mkono na baadhi ya watu, huku wengine wakiyabeza na kuyapinga.