Mvua kubwa zilizonyesha siku za hivi karibuni zimesababisha uharibifu mkubwa wa miundombinu katika Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani.

Barabara kadhaa, madaraja na nyumba za watu vimeharibiwa na mvua hizo, Mkurugenzi wa Wilaya hiyo, Mshamu Munde, amesema wakati akizungumza na JAMHURI hivi karibuni.

Anasema hivi sasa kuna baadhi ya vijiji vinafikika kwa shida kwa sababu barabara zimeharibika na kusababisha usumbufu mkubwa kwa wakazi wa maeneo hayo.

Amezitaja baadhi ya barabara ilizoharibiwa na mvua hizo kuwa ni pamoja na za Kata ya Bupuambako, barabara ya Kijiji cha Kiparanganda na katika Kata ya Kitomondo, barabara ya Mkurutini – Kitomondo nayo imeathirika.

Anaongeza kuwa katika Kata ya Nyamato daraja limeharibika katika barabara ya Mkanoge – Kibamba.

Katika Kata ya Shungubweni, Mto Mbezi umefurika na usafiri katika maeneo hayo na Vianzi umekuwa wa shida na wananchi wanalazimika kutumia mitumbwi kwenda sehemu mbalimbali badala ya barabara.

Munde anasema hata hivyo halmashauri tayari imekwisha kumtuma Meneja wa Wakala wa Barabara Vijijini (TARURA) kwenda katika maeneo yaliyoathirika ufanya tathmini na kazi ya kurekebisha kasoro zilizojitokeza ili kurudisha usafiri katika hali yake ya kawaida.

Amin Karimu, mmoja wa madereva wa  bodaboda wilayani humo anasema kuwa wamelazimika kuongeza nauli kwa wasafiri kutokana na ubovu wa miundombinu.

Anabainisha kuwa hivi sasa nauli ya kutoka Mkuranga hadi Shungubweni ni Sh 12,000 kwa safari moja kutokana na ubovu wa barabara.

“Kwa sababu madereva wengi wa bodaboda hawaendi huko, wale wanaokwenda wanalazimika wakati mwingine kubeba abiria wawili huku kila mmoja akilipa hizo Sh 12,000,” anasema.