Mvua zilizonyesha kwa wiki kadhaa zimesababisha uharibifu mkubwa wa miundombinu ya barabara na madaraja katika Mkoa wa Dar es Salaam hasa katika wilaya za Kinondoni na Ilala.
Ziara zilizofanywa na gazeti hili katika maeneo kadhaa katika Mkoa wa Dar es Salaam zimebaini kuwa wilaya hizo mbili zimeathirika sana. Hali si mbaya sana wilayani Temeke, wilaya ambayo miundombinu yake ya barabara imeimarishwa katika miaka ya hivi karibuni.
Wakizungumza na gazeti hili, wakazi wa Kinondoni na Ilala wameiomba serikali kuhakikisha tatizo hilo linatatuliwa haraka ili kuwawezesha kushiriki kikamilifu kwenye shughuli za kiuchumi.
Wilaya ya Ilala
Wakazi wa Gongo la Mboto Ulongoni wameiomba serikali kuwajengea daraja linalounganisha Ulongoni ‘B’ na Ulongoni ‘A’ kwani ni muhimu sana.
Akizungumza na JAMHURI, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Ulongoni ‘A’, Abrahaman Munisi, anasema wananchi wengi katika eneo hilo wanahangaika kutokana na kuharibika kwa daraja hilo.
“Hivi sasa watu, wakiwamo wanafunzi, wanalazimika kuvuka katika eneo ambalo halina daraja na si salama. Inaponyesha mvua hali inakuwa mbaya zaidi kwa sababu maji yanajaa,” anasema.
Anasema wafanyabiashara wanaotoa huduma za usafiri kuelekea Ulongoni ‘A’, Bangulo na Mongo la Ndege wamesitisha huduma za usafiri kutokana na ubovu wa barabara.
Munisi anasema amekwisha kutoa taarifa ya tatizo hilo la daraja kwa ngazi husika na matarajio yake ni kuwa tatizo hilo litatatuliwa haraka.
Kwa upande mwingine, anasema amewaunganisha baadhi ya vijana kama madereva wa bodaboda na Bajaj na kuwaomba watengeneze daraja la muda katika eneo hilo.
Akizungumzia tatizo hilo, Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara, anasema kuwa anayafahamu matatizo ya eneo hilo kwa kina, na kwamba ujenzi wa madaraja yote mawili utaanza mara moja baada ya mkataba kusainiwa.
Anasema wiki ijayo Mkurugenzi wa Halmashauri atasaini mkataba wa kujenga madaraja yote mawili ya Ulongoni ‘A’ na ‘B’.
“Tunajenga madaraja ya kudumu. Baada ya muda tatizo la usafiri kwa wakazi wa maeneo yale litakuwa ni historia,” anasema Waitara.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Ulongoni, Jacob Kiss, amethibitisha kuwa mchakato wa ujenzi wa madaraja hayo tayari umeshaanza na Sh bilioni nne zinahitajika kwa ajili ya ujenzi wa madaraja hayo.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Ulongoni A, Sikitiko Salehe, anasema kuwa baada ya daraja kuzolewa na maji ya mvua, hali ya usafiri na usalama kwa wanafunzi imekuwa mbaya.
“Si wanafunzi tu, hata walimu nao wamo hatarini, kwa sababu pale mtoni hakuna daraja,” anasema na kubainisha kuwa hali hiyo imesababisha kushuka kwa mahudhurio.
Mwalimu Sikitiko anasema kutokana na hali hiyo, wanafunzi na walimu wanalazimika kulipa mara mbili ya nauli ya kawaida ili kupata usafiri utakaowafikisha shuleni na kuwarejesha makwao.
Mkazi wa Ulongoni A, Saitara Mahuvi, anasema tangu daraja hilo lizolewe na maji, wamekuwa wakipata shida sana ya usafiri, kwani hivi sasa wanalazimika kulipa mara mbili ya nauli ili kupata usafiri unaozungukia maeneo mengine.
“Hakuna mwanasiasa tuliyemuona kuja kusaidia… huwa wanakuja na maneno mazuri wakati wa kampeni, lakini nyakati hizi za shida hatuwaoni,” anasema.
Katibu wa kikundi cha madereva wa Bajaj katika eneo hilo, Ignatus Salaheli, anasema kuwa baada ya kuona hali hiyo waliamua kuchangishana Sh milioni mbili ambazo zimetumika kujenga eneo la kupita kwa muda.
Makongo Juu
Eneo jingine ambalo barabara yake imeathirika kwa kiasi kikubwa na mvua ni Makongo Juu ambako Mwenyekiti wake wa Serikali ya Mtaa, Saida Mahumbe, anasema maeneo kadhaa hayafikiki kutokana na ubovu wa barabara.
Anasema hali ya barabara katika eneo lake ni mbaya na inasababisha hata kutopitika kwa baadhi ya sehemu, na wananchi wengi wanalipa gharama kubwa kwa safari za kwenda sehemu mbalimbali kujitafutia riziki.
Kwa upande wake, Salma Shabani, mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Makongo Juu, anasema ubovu huo wa barabara unawaathiri sana kina mama.
“Siku moja nilikuwa ninamsindikiza mama anayekwenda kujifungua, ilinyesha mvua na Bajaj tuliyokuwa tumekodisha ilishindwa kupita. Kutokana na msukosuko wa barabara mbovu, mzazi akapata uchungu na kujifungua njiani,” anasema.
Tarula wanena
Mratibu wa Mamlaka ya Barabara za Mijini na Vijijini (Tarula) Mkoa wa Dar es Salaam, Mhandisi George Tarimo, anasema barabara nyingi katika wilaya za Ilala na Kinondoni zinaharibika mara kwa mara kwa sababu maeneo hayo bado yanaendelezwa.
“Katika wilaya hizi bado watu wanapimiwa viwanja na kuendelea na ujenzi wa makazi tofauti na Temeke,” anasema.
Anasema ofisi yake ina taarifa kuhusiana na changamoto ya usafiri katika maeneo mengi kutokana na barabara na madaraja kuharibiwa na mvua zinazoendelea kunyesha.
“Tunayafanyia kazi matatizo hayo na baada ya muda mfupi tu wataalamu wetu watakuwa kazini kurekebisha maeneo hayo, tunasubiri mvua itulie kwanza,” anasema.
Kuhusu daraja linalounganisha Ulongoni ‘A’ na ‘B’, anasema mkandarasi amekwisha kupatikana na kinachosubiriwa ni mkataba ambao upo kwa mwanasheria.
Anasema wakati wakisubiri ujenzi wa daraja la kudumu wanafanya mpango wa kuweka kivuko cha muda katika maeneo hayo ili wananchi waweze kuvuka kwenda kwenye shughuli zao kwa usalama.
Kuhusu barabara ya Makongo Juu, Tarimo anasema mkandarasi yumo katika mchakato wa ujenzi na ni matarajio yake kuwa ujenzi wa barabara hiyo utakamilika katika muda uliopangwa.