Na Mwandishi Wetu, JakhuriMedia, Bunda
Mkuu wa Wilaya ya Bunda Dkt. Vicent Anney amesema mvua za El Nino zimekuwa sababu kubwa ya ongezeko la wanyamapori aina ya mamba ambao wamekuwa wakitoka maeneo yao ya asili na kwenda maeneo ya wananchi na kuleta madhara kwa maisha na mali zao katika vijiji vya Kasahunga na Mayolo Wilayani Bunda.
Dkt. Vicent ameyasema hayo leo Januari 18, 2024 katika ziara ya Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania – TAWA, Mabula Misungwi Nyanda iliyofanyika wilayani humo kwa lengo la kuwatembelea waathirika wa mamba na kutoa pole.
“Na mwaka huu, Kamishna hali hii imeongezeka sana baada ya kuwepo kwa mvua ya El Nino ambayo imesababisha mamba kutoka katika maeneo yao ya asili kwenda kusogea kwenye maeneo ya wananchi” amesema.
Akifafanua zaidi suala hilo, Dkt. Vicent amesema mamba wamekuwa wakisafirishwa na mikondo ya maji ya mito kuelekea ziwani jambo ambalo limesababisha wanyamapori hao kuonekana kwa wingi katika kingo za Ziwa Victoria nyakati za jioni na alfajiri na hivyo kusababisha madhara kwa baadhi ya wananchi wanaokwenda kuchota maji au kuoga kando ya Ziwa hilo.
Hata hivyo pamoja na changamoto hiyo, Mkuu huyo wa Wilaya amepongeza jitihada za dhati zinazofanywa na timu ya Maafisa na Askari wa TAWA Kanda ya Ziwa akithibitisha kuwa wanafanya kazi usiku na mchana katika harakati za kuwadhibiti mamba hao na kutoa rai waongeze kasi ya kutoa elimu ya kujikinga na kuwadhibiti wanyamapori hao kwa wananchi wa maeneo yenye changamoto hiyo.
Kwa upande wake Kamishna wa Uhifadhi wa TAWA Mabula Misungwi Nyanda amesema kutokana na kuongezeka kwa vilio vya wananchi vinavyotokana na matukio ya mamba katika vijiji vya Kasahunga na Mayolo Wilayani humo, imemlazimu kufanya ziara mahsusi katika vijiji hivyo ili kujionea hali halisi ikiwa ni pamoja na kuwatembelea na kuwapa pole familia za ndugu walioathiriwa na wanyamapori hao na kufikisha salamu za rambirambi kutoka Serikalini.
Kamishna Mabula amesema Serikali inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na uongozi wa Wizara ya Maliasili na Utalii inayoongozwa na Waziri Angellah Kairuki wamepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya changamoto ya mamba inayowakabili wananchi hao na kuahidi kuongeza ulinzi kwakuwa kipaumbele cha kwanza kwa Serikali ni uhai wa wananchi wake na siyo wanyamapori.
Kwa minajiri hiyo, Kamishna Mabula ametoa maelekezo kwa Maafisa na Askari wa TAWA kwa kushirikiana na wananchi kuwasaka mamba wote walioleta madhara kwa wananchi au wenye viashiria vya kuhatarisha maisha ya binadamu katika maeneo hayo na kuwaua kwa mujibu wa Sheria.
Pia amewataka wananchi wa vijiji hivyo kuchukua tahadhari wanapofanya kazi zao pembezoni mwa Ziwa hilo ikiwa ni pamoja na kuweka makazi yao umbali wa Mita 60 kutoka ziwani.
Naye Diwani wa Kata ya Kasahunga Mhe.Fortunatus Maiga ameipongeza Serikali kwa kusikia kilio cha wananchi wa Kata hizo na hivyo ameiomba kujenga miundombinu ya maji katika Kata yake ili kuokoa maisha ya wananchi wanaokwenda kuchota maji ziwani pamoja na kuwavuna mamba hao ambao wanahatarisha maisha ya binadamu.