Na Mwandishi Wetu, Mtwara
Kufuatia mvua kubwa iliyonyesha Februari 3,2025 imesababisha maafa kwa baadhi ya maeneo ya Manispaa ya Mtwara Mikindani mkoani Mtwara hususani kwa wanafunzi wa Chuo cha Sauti na Utumishi.
Maafa hayo yametokea mtaa Kiyangu ‘B’ ambako wanafunzi hao wapatao 35 wanaishi wamepata madhara ya kupoteza vitu vyao mbalimbali ikiwemo vyakula, simu, madaftari na vitabu vyao kuloa kutokana na ukuta wa hosteli wanayoishi kudondoka na maji kuingia kwenye vyumba vyao.
Mwanafunzi wa Chuo cha Sauti, Janeth Kalamule amesema tukio hilo limewaathiri sana wanafunzi kutokana na kupoteza baadhi ya vitu vyao na ikizingatiwa baadhi yao mitihani inaendelea wengine inakaribia.
“Wiki hii tuko kwenye wiki ya UE madaftari yamelowa tukategemea simu nazo zimeingia maji kwa hiyo inakuwa ngumu sana kwenye kusoma,” amesema Janeth.
Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mtwara, Oissa Singili amesema maji hayo yaliyopelekea kuvunjika ukuta katika hosteli hiyo ya wanafunzi ni kutokana na kuwekwa kwa kifusi kwenye barabara inayotokea bima kuelekea umoja ambayo ujenzi unaendelea na kupelekea maji kukosa muelekeo.
Akizungumza kwa niaba ya Meneja wa Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini TARURA wilaya ya Mtwara mjini, Maulidi Mushi amekanusha taarifa hizo za kuwa kifusi kilichopo kwenye barabara hiyo ambayo ujenzi unaendelea ndio sababu ya maji kuingia kwenye makazi ya watu.
“Kujengwa kwa mifereji kwenye upande wa pili wa barabara hiyo kutasaidia kupunguza changamoto ya maji kuingia kwenye makazi ya watu na tayari lipo kwenye mpango wa tarura”amesema Mushi.