Wakazi zaidi ya tisa wa Kijiji cha Ngelenge kilichopo katika Kata ya Ruhuhu wilayani Ludewa mkoani Njombe wamekosa makazi baada ya mvua zilizoambatana na upepo zinazoendelea kunyesha mkoani hapa na kubomoa baadhi ya nyumba.
Mtendaji wa kata hiyo Yusuph Lukuwi amesema kuwa maafa hayo yametokea usiku wa kuamkia leo Machi 17,2023,majira ya saa 7, usiku, ambapo baadhi ya nyumba zimeezuliwa mapaa huku nyingine zikianguka na kusababisha baadhi ya wakazi kupata majeraha.
“Mvua ilianza majira ya saa 7 usiku watu wakiwa wamelala ndipo ukazuka upepo mkali na kuezua mabati pamoja na kuangusha kuta kwa baadhi ya nyumba lakini tunachoshukuru hakuna madhara makubwa kwa binadamu bali wamepatwa na majeraha madogo madogo kutokana na kuangukiwa na tofali za nyumba” amesema.
Aidha kwa upande wa mmoja wa wahanga wa maafa hayo aliyefahamika kwa jina moja la Aida anayekadiliwa kuwa na umri wa zaidi ya miaka 80 amedai kuwa wakati upepo huo ukivuma na kubomoa nyumba yake alikuwa amelala na hakusikia chochote mpaka kulipokucha ndipo akashangaa kuona juu kuko wazi huku upande wa nyumba yake ukiwa umebomoka.
Wakazi hao wameiomba Serikali kuchukua hatua za haraka katika kuwasaidia ili waweze kupata makazi kwani kwa sasa wamejishikiza kwa ndugu na majirani.