MV Nyerere imeamsha uchungu
Na Deodatus Balile
Ajali ya MV Nyerere iliyotokea Septemba 20, 2018 katika Ziwa Victoria imeamsha uchungu wa wakazi wa Kanda ya Ziwa. Imenikumbusha siku ya Jumanne ya Mei 21, mwaka 1996 ilipozama meli ya MV Bukoba na kuua watu zaidi ya 800. Takwimu zinatofautiana. Wapo wanaosema walikufa watu 1,000 na wengine wanasema walikufa 800. Vivyo hivyo kwa kivuko cha MV Nyerere takwimu zinatofautiana. Wapo wanaosema wamekufa 400, wengine wanasema wamekufa 200, wengine wanasema 160.
Mbali na ajali ya MV Bukoba (1996) katika Ziwa Victoria zipo pia meli za MV Spice Islander (2011) katika Bahari ya Hindi, ambako zaidi ya watu 200 walipoteza maisha, huku MV Skagit nayo ikizama kwenye bahari hiyo hiyo na kupoteza maisha ya watu karibu 150 mwaka 2012.
Sitanii, nikirejea kilichotokea katika ajali ya MV Bukoba, kitu hicho hicho naamini uchunguzi utakibaini kwenye kivuko cha MV Nyerere. Kwamba MV Bukoba ilikwisha kupoteza kitu kinachoitwa ‘Center of Gravity’. Kwamba meli hiyo ilikuwa inatembea kwa kudra za Mwenyezi Mungu. Baadhi ya wataalamu tayari wameanza kueleza tatizo linalorandana na hilo.
Kwa wanaokumbuka meli ya MV Bukoba ilisafiri kutoka Bukoba na ikapinduka umbali wa maili nane kutoka Bandari ya Mwanza. Hata kivuko cha MV Nyerere kimesafiri kutoka Ukerewe hadi Ukara, kikaanguka wastani wa mita 50 kutoka mwaloni. Sura ile ile kuwa wananchi walipoona gati, kama ilivyotokea kwa MV Bukoba, wakajikusanya kwa wingi sehemu ya kutokea wawe wa kwanza kushuka, matokeo yake yakawa majanga.
Kuna kila dalili kuwa taratibu hazikufuatwa. Wenye kuendesha kivuko hiki wamejaza watu kuliko uwezo wa kivuko. Rais John Magufuli amesema kivuko kilikuwa na uwezo wa kubeba abiria 100 au wakizidi 101. Mpaka naandika makala hii, miili iliyokwisha kuopolewa ilikuwa inakaribia 209, na abiria 41 walikuwa wameokolewa.
Hapa kuna maelezo kuwa kivuko hiki kinachopaswa kubena angalau magari matatu madogo, ndani yake kilikuwa na lori lililosheheni mizigo. Ikumbukwe maelezo yaliyopo inaonekana kuwa Ukara lilikuwapo gulio. Hii ina maana kivuko kilikuwa na mzigo wa kutosha. Wafanyabiashara hapana shaka walikuwa wanawahi soko.
Sitanii, pia zipo taarifa kuwa ingawa kivuko kilibadilishiwa injini Julai, mwaka huu bado hakikuwa sawa kiufundi. Mbunge wa Ukerewe (Chadema), Joseph Mkundi, mbali na kukilalamikia alipata kusema idadi ya safari za kivuko iongezwe kutoka mbili hadi tatu ili kuepusha madhara yanayoweza kutokea.
Hata hivyo, binafsi nadhani nchi yetu inapaswa kuchukua hatua kubwa zaidi. Miaka 22 iliyopita ilipotokea ajali ya MV Bukoba tulipaswa kushituka na kujipanga. Katika ziwa hili, Kenya inalimiliki kwa asilimia sita, Uganda asilimia 45 na Tanzania asilimia 49. Kwa mantiki hiyo Tanzania ndiyo yenye eneo kubwa la maji ya Ziwa Victoria.
Tukio la Jumanne, Mei 21, mwaka 1996 walipofariki dunia karibu watu 1,000 kwa MV Bukoba kuzama, lilipaswa kuwa fundisho. Kama nchi tulipaswa kununua meli ya uokozi (crane) kubwa na kuwa nayo ndani ya Ziwa Victoria. Sikuridhika kuona kivuko kimepinduka saa saba mchana, lakini siku nne baadaye hatujaweza kukiopoa. Ina maana hatuna vifaa.
Leo watu zaidi ya 200 wamepoteza maisha na huenda bado hata baada ya ajali hii hatutafanya chochote. Tutakuwa tumefanya kosa kubwa tusiponunua meli ya uokozi kujiandaa kwa majanga katika Ziwa Victoria. Huu ni uhalisia. Hata kama tutatunga sheria kali kiasi gani, naamini miaka ijayo bado ajali zitaendelea kutokea.
Kimsingi, namwamini Rais John Magufuli. Tofauti na awamu zilizotangulia ambapo neno mchakato lilitawala, naamini akiamua tunaweza kununua crane ya majini ikawapo Mwanza. Hata kama tukinunua meli inayobeba mizigo kawaida, lakini bado ikawa na uwezo wa kuinua meli iliyozama tukaepuka hasara ya kununua meli ikakaa miaka 22 kusubiri ajali nyingine, lakini nadhani uamuzi huo inatupasa tuufanye sasa.
Watumishi wanaokiuka sheria na kanuni za usalama wa abiria wala hao tusiwaonee huruma. Tuwachukulie hatua kali na liwe fundisho kwa wengine. Jamii inalalamika. Haikuona hatua kali dhidi ya waliosababisha ajali ya MV Bukoba, Skagit au Spice Islander, ila sasa tunadhani zamu hii vyombo vya sheria vitatoa fundisho kali na la kudumu. Poleni Watanzania kwa ajali hizi.
Mwisho