Sanaa ya muziki nchini Tanzania inakuwa siku hadi siku. Kuna viashiria fulani ambavyo kwa namna moja ama nyingine, vinaonesha ukuaji wa sanaa hii ambayo mojawapo ya kazi zake ni kuburudisha na kuelimisha.

Kumekuwa na ongezeko la wasanii siku hadi siku katika staili ya msanii mmoja mmoja na hata katika viwango vya kuunda makundi na bendi za muziki, japokuwa bendi nyingine ziko katika soko kwa mwendo wa kuchechemea kutokana  na kukosa ubunifu.

 

Lakini muziki wa kizazi kipya maarufu kama Bongo Fleva unashika kasi ya aina yake, kwa sababu vijana wengi wanaochipukia sasa katika sanaa ya muziki wameona kama hiyo ndiyo njia ya ‘kutokea’ na kujipatia umaarufu.

 

Katika kundi la wasanii wa Bongo Fleva kuna wanamuziki ambao kwa kiwango kikubwa wameweza kufanikiwa. Hii imetokana na ubunifu wao wa utengenezaji wa muziki huo na hatimaye kuweza kushika soko la ndani na nje ya nchi. Pia kuna waliokwenda mbali zaidi na kuanzisha vitegauchumi ambavyo vimetoa ajira kwa vijana wengine wa Kitanzania.

 

Mbali na hayo, wanamuziki wengine wameishia kulewa sifa na kujenga umaarufu wa kuwa na majina makubwa – zaidi ya hapo hakuna la ziada. Mwanamuziki wa aina hii akipita mitaani anaambulia kuitwa jina lake tu, lakini mfukoni hana hata shilingi moja. Nathubutu kusema kuwa kwa sasa kuna waliogeuka ombaomba kwa kutangaza umaarufu wao wa enzi zilizopita.

 

Hii ni hatari. Na hii ni kwa sababu ya kufanya mambo kwa kuiga, kukurupuka na bila kuwa na mipango endelevu. Wanamuzuki wetu wameamua kuwa watumwa wa kutukuza tamaduni za Magharibi na kusahau utamaduni wetu.

 

Kuna wakati nilimsikiliza msanii fulani wa Bongo Fleva akihojiwa katika mojawapo ya vituo vya radio hapa nchini. Alitakiwa kutaja baadhi ya vyombo vilivyotumika kutengeneza ala za muziki wake, lakini alisema hiyo ni kazi ya mtengenezaji wa muziki (prodyuza) na wala si kazi yake.

 

Ni kweli kuwa huu ni wakati wa kufanya mambo kidijitali zaidi lakini kuna haja ya kuangalia pia soko la kimataifa katika muziki. Itakuwa ngumu kwa msanii kuingiza muziki wake sokoni katika kiwango cha kimataifa endapo ameiga kazi ya msanii wa nchi nyingine. Halikadhalika hajui hata vifaa vinavyotumika kutengeneza muziki wake.

 

Hali hii ya baadhi ya wanamuziki kutofahamu mambo ya msingi kama hayo, imewasababishia kushindwa kuimba moja kwa moja na bendi jukwaani (live) na badala yake kuimba kwa kufuatisha ala zilizotengenezwa tayari.

 

Jambo jingine la kushangaza wasanii hao hao ndiyo vinara wa kushinda tuzo mbalimbali za ubora katika muziki. Zinahitajika juhudi za makusudi kwa waandaaji na watoa tuzo kwa wasanii bora wa muziki, kuzingatia vigezo muhimu katika kupata washindi wa tuzo hizo.

 

Siamini kuwa hakuna msanii asiyejua kuwa mojawapo ya kazi ya msanii wa aina yeyote ile ni kutangaza utamaduni wake kwa wengine na si kuiga tamaduni za wengine ambazo hata hajui chimbuko lake wala maana yake.

 

Kinachoonekana katika muziki wa kizazi kipya ni kurudia yaliyokwisha kufanywa na wanamuziki wa kutoka mataifa mengine. Hii inafanyika ama kwa kuiga ala za muziki au kubadilisha maneno katika kutoka lugha moja hadi nyingine.

 

Kuiga jambo si vibaya lakini si kurudia kazi ya mtu mwingine kwa kubadilisha lugha na vitu vingine. Kwa mfano, ukisikiliza muziki wa mwanamuziki Felix Wazekwa na Kofi Olomide unafanana kwa karibu,  lakini staili yao si ya kuiga.

 

Sasa hivi limekuwa jambo la kawaida katika shughuli mbalimbali za burudani utasikia majina ya makundi ya burudani kama vile Makhirikiri, Michael Jackson, P Square na mengineyo.

 

Msanii akipanda jukwaani anatoa burudani kama ya Makhirikiri. Je, ni kweli Tanzania hatuna muziki wetu unaoweza ukaenda kimataifa ukawa kama vile Makhirikiri na tukatangaza utamaduni wetu? Au ndiyo uvivu wa kufikiri?

 

Wanamuziki wanahitaji kubadilika na kuwa na mtizamo wa kupenda utamaduni wao zaidi kuliko wa kigeni, kuepuka upepo huu wa nchi za Magharibi ambao kila kukicha unawasambaratisha wanamuziki wa kizazi kipya. Hali hii inachangia tatizo la mmomonyoko wa maadili.

 

Kuna haja ya wanamuziki wetu kuwa na hali ya utambulisho  katika utengenezaji muziki wao, japokuwa kuna baadhi wamefaulu katika hili. Kwa mfano mwanamuziki Jose Chameleon wa Uganda amekuwa maarufu katika ukanda huu kutokana na staili yake ya utengenezaji wa muziki wake.

 

Mambo haya ya kupenda kuiga ndiyo yamesababisha baadhi ya watu katika jamii kuona kuwa muziki wa kizazi kipya ni muziki wa kihuni.

 

Baadhi ya wanamuziki waliokuwa wakipiga Bongo Fleva zamani na sasa wamegundua kuwa muziki huo hauna jipya, na sasa wamehamia katika staili nyingine na wengine wameamua kuanzisha bendi zao ili kupiga muziki wenye ladha tofauti.