Ada ya mja hunena, muungwana ni kitendo. Hii ni methali chanya na tambuzi kwa mtu yeyote anayejisifu au anayetambuliwa ni muungwana. Muungwana ni mtu mwenye adabu na tabia zinazokubalika katika jamii; adinasi. Maana ya pili mtu asiye mtumwa.

Kwa mujibu wa Kamusi ya Kiswahili Sanifu, adinasi (wadinasi) ni mtoto anayetoka katika ukoo bora kama vile ukoo wa kifalme, kitajiri au mlango wa ukoo maarufu; mtoto wa watu, muungwana, binadamu.

Methali hiyo ni maarufu na hutumika mno na Waswahili katika kuelezea au kusifu jambo fulani katika kutimiza ahadi. Ahadi ni deni. Ni msemo pacha unaotoa maana ya uungwana na kusogeza mbali utumwa ambao daima ni unyonge na uchache wa ukweli.

Viongozi wetu wengi hapa nchini, katika dola, taasisi za dini, jumuiya za wananchi, vyombo vya uamuzi na vyombo vya siasa hupenda kuzungumza neno uungwana katika kuweka mustakabali na kuwafahamisha watu mambo wayatendayo wao (viongozi) ni ya kiustaarabu na kiungwana, lau kama baadhi yao hawako hivyo.

Kwa mujibu wa uongozi, wao ni kusaidia, kutetea na kuwapatia stahiki zao wananchi ndani ya mfumo wa uendeshaji maisha katika jamii. Wanapokuwa majukwaani au mbele ya vyombo vya mawasiliano na umma, husema kuwa hawapendi kuona wananchi wanakosa haki zao za msingi na kuminywa kwa demokrasia na mtu au kikundi cha watu.

Ni ukweli wajibu wa kiongozi yeyote ni kuelekeza na kusimamia watu katika kazi au shughuli fulani kwa maslahi ya jamii. Ndiyo maana viongozi wa dini wanahubiri neno jema la Mwenyezi Mungu ili watu wawe wachamungu na waumini kwelikweli. Viongozi wa dola wanatoa maelekezo na miongozo ili raia waishi kwa amani na salama.

Si hivyo tu, viongozi wa jumuiya wanatoa hamasa na mafunzo ya mila na desturi ili watu watii taratibu na kanuni ndani ya jamii. Viongozi katika vyombo vya uamuzi hutunga sheria na kuona haki inatendeka. Viongozi wa siasa nao huhamasisha na kushawishi wananchi kuelewa na kutii taratibu za kupata haki, mbinu za ujenzi wa uchumi uliyo bora na namna ya kuishi kwa upendo na utulivu.

Viongozi wote hao wanapotoa kauli zao, hazina budi ziendane na vitendo vyao vikibeba utimilifu wa ahadi, vishawishi vya upendo, utii wa kanuni na sheria za nchi, wajibu wa kufanya kazi na kukataza vishawishi vya kuwagawa watu katika misingi kujenga na kuimarisha chuki na uhasama.

Sitaki nikuweke katika kundi la ushahidi kwa haya nisemayo, lau kama una macho unaona vitendo na una masikio unasikia kauli za baadhi ya viongozi nchini wanavyohamasisha chuki baina ya raia na Serikali, wananchi na vyombo vya uamuzi, vyombo vya usalama na wananchi wenyewe ndani ya nchi yetu.

Viongozi hao wanajinadi kuwa wanawatetea wananchi kupata haki zao za msingi za binadamu kwa njia za kiungwana na kistaarabu. Nashangaa! Mbona wanaacha kutii kanuni zilizopo na kuvikimbia vyombo vya uamuzi ambako haki ndiko inakopatikana?Kulalama na kushawishi kufanya ghasia wananchi ndiyo kudai haki? Je, uungwana hapo uko wapi?

Kwa kauli zao, hawatambui mamlaka zilizoko madarakani kwa maelezo mbalimbali ikiwamo uchakachuaji wa mchakato wa kuingiza mamlaka hizo madarakani. Wakati huohuo, wanataka mamlaka ziwasikilize na kuwatimizia haki na mahitaji yao kutokana na kanuni zilizopo. Je, utii na tabia njema ndani mwao ziko wapi?

Wanaeleza wanapenda amani na hawataki mikono yao kuwa na damu kushika mamlaka kuu za nchi. Pembeni wanawaambia vijana subirini wakati bado, lakini wanawahamasisha wasitii maagizo ya vyombo vya usalama, je, huo ndiyo uungwana ni kitendo?

Wanazungumza kuwa wanaonewa na hawasikilizwi hoja zao. Wanaamua kuziba midomo; hawataki kusema tena. Mmh! inakuwaje wanasusa vikao vya kidemokrasia? Wapi watapata haki yao ikiwa chombo cha kidemokrasia wanakikimbia na kujitia ububu? Vipi tiba stahili itapatikana? Hawaoni hiyo ni dhuluma kidemokrasia kwa wananchi? 

Ni kweli kuziba midomo ni kitendo cha kidemokrasia. Ni busara? Inakuwaje wao hawataki dhuluma lakini wanafanya dhuluma kwa wananchi? Haikosi kuja jambo! Naomba kuwasihi viongozi wetu kwamba thamani ya uungwana ni kitendo cha ukweli kwa pande zote mbili – kwao na kwetu (viongozi na wananchi) bila kujali itikadi za kisiasa.

Kumradhi. Kumbukeni wahenga wamesema serikali ni serikali hata kama iwe ya kuku ni serikali. Lazima serikali hiyo ithaminiwe, itiiwe na iheshimiwe. Isipuuzwe sababu imepewa ridhaa na wahusika. 

Kuendelea kujisifu kutafuta haki na kupenda amani ilhali unajenga viashiria vya kuvunja amani hiyo siyo mantiki ya muungwana ni kitendo, bali ni ada ya mja (binadamu) kunena. Mjirekebishe.