Watu mnaweza kubishana kwa hoja, lakini si kwa kukamiana nani ni nani Visiwani Zanzibar. Kila mtu anataka, na ni haki yake kila mwananchi kutambuliwa kama yupo. Kutambuliwa huko kunafikiwaje? Vyama vyote vya upinzani vina lengo kuu moja tu- kuingia serikalini na kuboresha maisha ya wananchi kiuchumi, kielimu, kiafya na kiutawala bora. Njia zipi zitumike kuyafikia malengo hayo? Ndiyo ngoma inayochezwa kwenye uchaguzi huru.
Dini zote za Uislamu na Ukristo na hata Uhindu hazifundishi kisasi, bali zinafundisha “KUPENDANA na KUSAMEHEANA” daima.
Je, viongozi wetu wanayaamini haya katika mioyo yao ? Madaraka siyo suluhisho lakini, Haki Amani Na Maisha bora kwa kila Mzanzibari ndivyo vitakavyoleta suluhu ya huu mpasuko wa kisiasa. Ukitafakari historia hii ya mapambano ya ukombozi Zanzibar utagundua wazi kabisa kuwa wale wote wanaodai kero za Muungano wanakasumba ya UARABU na wanatamani bado kutawaliwa na Mwarabu.
Hawajakomboka kifikra (not yet libetated in mind), hawajiamini kuwa ni watu kamili na wana uwezo kama binadamu wengine wowote duniani. Watanzania tunaojua historia namna hii na tukiwa tumekomboka kifikra, kero zote hizi za Muungano tutaziona kama vichuguu na wala tusingezikuza kama Mlima Kilimanjaro. Uingereza licha ya kuungana nchi nne -Uingereza, Wales , Skotland na Ireland ya Kaskazini tangu mwaka 1801 hadi leo bado wana kero zao katika Muungano wao unaoitwa United Kingdom (UK).
Marekani licha ya kuungana nchi (States) 51 mwaka 1877 bado wana kero hadi leo na Muungano wa li-nchi lao unaitwa United States of America ( USA ). Tusisahau pia msuguano unaofukuta siku zote kati ya China na Taiwan , India na Sri Lanka na pia kati ya Uingereza na Ulaya katika Umoja wao wa N chi za Ulaya.
Kwa nini sisi vi-nchi viwili tu – Tanganyika na Zanzibar tunadai eti Muungano huu wananchi hatukuulizwa kama tunauafiki au hatuuafiki? Je, wewe unayeuliza hilo ulikuwa umezaliwa tarehe hiyo ya Muungano? Miungano ya nchi zipi unazozijua wananchi waliulizwa kwa referendum? Tusiwe wa nadharia (theoretical) sana kuliko uhalisia wa miungano duniani (practability).
Muungano huu unawezekana ilimradi kila mmoja wetu anatimiza wajibu wake. La msingi hapa ni kujitambua kuwa watu wa Bara na wa Visiwani tangu zamani wamejiona kuwa wamoja, wana asili moja; hivyo tuishi kwa amani na upendo. Kila mmoja ni Mtanzania kamili.
Kwa vile tangu mwanzo tulizembea kurekebisha kero zilizoonekana, sasa imefikia mahali UAMSHO wanaishika Serikali pabaya hata inashindwa kujitetea. Hawa wana UAMSHO si ndiyo wanajaribu kufufua usultani? Mbona tunasikia kiongozi wao siyo Mzanzibari eti alitokea Arabuni sasa atakuwaje na uchungu wa ardhi ya Afrika? Wazanzibari wote mimi nawaona kama vile asilimia 80 wazaliwa wa baada ya Muungano, wala hawajui adha za ukoloni wa sultani au Mwingereza. Wazee wao ndiyo waliojua hayo.
Ukiangalia historia utajua ukweli wa mambo. Wale waliosoma makala katika Raia Mwema toleo maalumu na. 266 la Oktoba 24 – 30 Oktoba, 2012 uk . XIV mazungumzo ya Balozi Ali Karume aliposema wazi kuwa Mwalimu aliipenda kwa dhati Zanzibar na kusema, nanukuu; “…Akafika kwa Mzee Karume wakazungumza, lakini kuna jambo walitofautiana Mzee Karume alimwambia sikiliza Bwana (Julius) nyie kule (Bara) mnagombana na Waingereza lakini sisi hapa (Unguja) tunagombana na Wamanga wangu hawa”. Huu ni ushahidi wa kihistoria kuwa kule Visiwani Waarabu ndiyo tatizo.
Neno hili “Wamanga” lina maana sana hapa. Sisi hapa Dar es Salaam nadhani na pwani yote ya mwambao neno Wamanga lilieleweka wale Washihiri waliokuwa wakitembeza vikoi na mazulia majumbani mijini wakitukopesha. Ni Waarabu wa hali ya chini sana – hasa mabaharia katika majahazi ya kutoka Arabuni.
Lakini hapa Mzee Karume alipotumia neno hili Wamanga alikuwa anamaanisha mamwinyi wale wa Kiarabu kutoka Oman , watawala wa nchi – ukoo wa kisultan.
Kamwe asingeweza kugombana na Washihiri mabaharia watembeza vikoi na mazulia mabarabarani. Huu ni uelewa wangu wa kisiasa wa Visiwani. Na ndiyo wengi wana UAMSHO; ndiyo wanaolilia usultani urudi; na ndiyo wanaotaka Muungano uvunjike. Sidhani kama yupo mwenye mbari ya kibantu anataka Muungano uvunjike.
Kwa mtazamo wangu na kuamini kwangu ni kuwa upo upotoshwaji unaofanywa kwa makusudi kabisa katika historia ya Zanzibar . Sijui nia na madhumuni ya upotoshaji huo, lakini kunalenga kuonesha matatizo yote ya Visiwani yamesababishwa na Wabara. Waandishi wenye asili au mbari ya Kiarabu wanapotosha historia ile ili kupaka rangi mbaya Muungano.
Kwa yeyote aliyesoma makala ya KALAMU YA ZANZIBAR (na Ahmed Omar Khamisi) katika matoleo ya gazeti liitwalo FAHAMU (Na. 218 la Novemba 27 –Desemba 3, 2012 na toleo Na. 219 la Desemba 4 –Desemba 10, 2012) uk. 16 kuna kichwa cha habari, “Akina Borafya ni simba waliokosa nyama mbugani watakula mabuchani”. Akiwa na akili timamu ataelewa na kutambua makala zile zinalenga watu, kamwe hazizungumzii mambo (issues). Sasa kuwasema watu au kuwasemea watu ni ufinyu mkubwa wa falsafa nzima ya shabaha na malengo ya Serikali ya Umoja Visiwani.
Hapa panaibuliwa chuki na uhasama ule wa zamani ili kuonesha nani anafaa Visiwani na nini asili ya mitafaruku tangu enzi hizo za uhasama wa ukabila, upemba uunguja na ubara. Kumbe zile jitihada za waheshimiwa Amani Abeid Karume na Maalim Seif Sharrif Hamad kuleta Umoja wa Kitaifa Visiwani ili wote waishi kwa amani na upendo zinahujumiwa, maana bado wapo wale wanaoota kuibua ya kale kwa sababu zao binafsi.
Ndiyo maana nilisema huko nyuma kwamba kila mwamba ngoma anavutia ngozi upande wake tu na hasikii wala hataki kuona upande wa wenziwe. Makala zetu kwa mtazamo wangu zilenge kudumisha huu Muungano wetu na kamwe zisilenge kuubomoa.
Serikali ya Umoja iimarike na idumishe Muungano. Je, wangapi wanajua kuwa mbunifu wa hili jina la nchi yetu “ TANZANIA ” ni kijana wa mbari ya Kiasia? Huyu anaitwa MOHAMED IQBAL DAR mzaliwa wa Tanga akiwa kijana wa miaka 18 shuleni Mzumbe alibuni na kuunganisha herufi TAN kutoka Tanganyika na herufi ZAN kutoka Zanzibar kwa kuongezea herufi IA kama kimalizio cha nchi nyingi za Afrika mathalani Nigeria, Algeria, Tunisia, Zambia, Mauritania. Basi kwa utundu wake akaongeza naye herufi hizi IA baada ya kuunganisha majina ya TAN – ZAN – IA kaibua jina la Taifa letu la Muungano kuwa TANZANIA . Huyu ni muumini wa Muungano.
Kwa hivi sasa anaishi Birmingham , Uingereza. Ni msomi na mhandisi wa radio. Yeye anaona fahari sana kwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar . Huko Uingereza aliko anajivunia Utanzania wake. Huu ndiyo ninaoita moyo wa uzalendo. Kila Mtanzania anapaswa kuwa nao na kujivunia. Sielewi nini kinawasukuma baadhi ya Wazanzibari kuchokonoa na kuupekecha Muungano na kutothamini (dilute) ili umoja wa Serikali yao ya Visiwani kwa kuelezea yale makovu ya kale. Makovu ndiyo baadhi ya nyufa zenyewe katika Muungano wetu.
Jamani eee tulichelea kuziba ufa sasa tutalazimika kujenga ukuta. Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere alisema pale Kilimanjaro Hotel mnamo Machi 13, 1995 kuwa ufa wa kwanza ni Muungano katika zile nyufa tano alizozungumzia siku ile. Kwanini tangu mwaka 1995 hadi leo hatukuchukua hatua za kuuziba? Watanzania tusihadaiwe na Uamsho wa Zanzibar . Tuwe ngangari na Muungano huu kwani ndiyo mboni ya Tanzania yetu.
Muungano ukivunjika tu, basi huo ndiyo utakaokuwa mwisho wa Tanzania . Nje ya Muungano hakuna sisi Wazanzibari, wao Watanganyika, hakuna. (Nyerere: Nyufa uk. 10 sentensi ya kwanza, ibara ya pili).
Brigedia Jenerali mstaafu Francis Mbenna anapatikana katika simu 0715 806758. Alikuwa mwalimu wa sekondari na Afisa wa JWTZ. Ni mwanahistoria na ameandika kitabu cha HISTORIA YA ELIMU TANZANIA toka 1892 hadi sasa (Dar es Salaam University Bookshop).