Yuko mwandishi mashuhuri wa habari Visiwani Zanzibar, aliyewahi kuwa mwandishi wa habari wa aliyekuwa Waziri Kiongozi, Maalim Seif (huyu mimi kiutani namwita “uncle chocolate”), aliandika makala katika Tanzania Daima, “Benjamin William Mkapa ninayemjua” Jumapili tarehe 13 Machi 2008 uk. 13.

Ameandika maneno haya, namnukuu; “…Mkapa aliniambia hawaelewi Wazanzibari kwanini walikuwa wanapenda MIVUTANO NA SIASA ZA CHUKI, UHASAMA NA MAJUNGU na HAWAPENDANI. Mwandishi huyo alijibu kwa maneno haya, nanukuu; “…Nilichomwambia ni kwamba, hali kama hii imekuwa kama MARADHI ya watu wanaoishi katika VISIWA, lakini nilifikiri ya Zanzibar yalikuwa YAMEFURUTU ADA”. Huyu mwandishi anajua hali halisi na tabia ya wenzake kule Visiwani. Ndiyo maana anakiri kuna maradhi yaliyofurutu ada huko Visiwani.

 

Miaka michache sasa imepita tangu majeshi ya Umoja wa Afrika (AU) kutoka Tanzania, Senegal, Sudan na Libya yalipoteka Kisiwa cha Anjouan kwa kushirikiana na majeshi ya Comoro. Askari mateka kutoka jeshi la muasi Kanali Barca walifurahia kujisalimisha kwa majeshi ya Tanzania kuliko kwa yale ya Comoro.  Walipoulizwa kisa cha kufanya hivyo walijibu bila kusita, “Watu wa Comoro wana visasi”.

 

Jibu hili linalingana na matamko yale ya mwandishi wa Zanzibar. Kwa hiyo, kuwekeana kisasi ni miongoni mwa tabia za watu wa Visiwani. Hiki ni kizingiti kimoja cha mtafaruku Visiwani Zanzibar.

 

Tuanzie hapo, Wazanzibari walilelewa kimatabaka huko nyuma walipokuwa Waarabu mamwinyi, Wahindi wachuuzi na Waafrika watwana. Kule kuwaweka sawa kama watu huru kulileta hisia za chuki na visasi katika mbari hizi. Mimi naona kutokuaminiana  ndiyo mzizi mkuu wa mpasuko wa kisiasa katika visiwa na pia kati ya Visiwani na Bara.

 

Katika historia tunaelezwa kuwa Serikali ya Zanzibar imepita awamu kadhaa hadi leo. Awamu ya kwanza ni ile enzi ya Mzee wetu, Abeid Amani Karume. Ile inasemekana ilileta maendeleo ya haraka na mabadiliko ya fikra. Lakini wengine wanadai ilikuwa inatawala kwa “decree”. Je, tunakumbuka Marekani walipojitoa kutoka Uingereza mwaka 1776? Nao walitawala kwa “decree” hivi hivi na Katiba yao inaonesha hali hiyo.

 

Julai 4, 1776 walipojitangazia Uhuru wao sehemu ya Katiba yao ilitamka haya, nanukuu; “…We, the people of the United States establish and ordain the constitution”. Katiba yao waliyoitangaza ilikuwa inaonesha wazi amri na maelekezo namna hii.

 

“It makes its constitution the permanent medium of its orders and prohibitions to all branches of the federal government and to many branches of the state governments:  they must do what the constitution directs and leave undone what it forbids” (Encyclopedia Britannic Vol. 22 uk. 755).

 

Kwa hiyo, ni utamaduni unaotumika baada ya mapinduzi, Serikali lazima itawale kwa “decree” kwa muda ili kutuliza hali ya utawala.

 

Utawala wa awamu ya pili ulileta Katiba ya demokrasia na ukafanyika uchaguzi. Wakapata Baraza la Wawakilishi badala ya Baraza lile la Mapinduzi (BMZ). Kipindi cha awamu ya tatu kilikuwa kifupi sana. Hiki kilijenga heshima ya Mzanzibari na kuboresha uchumi wa Taifa. Kipindi cha awamu ya nne zaidi ya vingine vyote kulitokea mtafaruku kati ya Pemba na Unguja. Ilikuwa dhahiri kisa si siasa, bali ni kumbukumbu za huko nyuma enzi za Mapinduzi.

 

Inasemekana Wapemba walibezwa na Wamakunduchi na sasa Wapemba walitaka kulipa kisasi kwa kuonesha chuki yao bayana kwa mtawala wa Zanzibar – Mmakunduchi. Baadaye kilifuata kipindi cha awamu ya tano kinachojulikana kama kipindi cha mzinduko wa uchumi na harakati za demokrasia halisi – kipindi cha komandoo. Kikafika kipindi cha sita cha mwanasiasa kijana, mzalendo na mwanademokrasia. Huyu alifuata nyayo za Mzee Karume, kumalizia ujenzi wa maghorofa, kujenga nyumba safi, kujenga mabarabara na visima kwa wananchi.

 

Lakini baada ya kipindi cha Karume mdogo tumeingia hiki cha saba cha MPEMBA. Kilio kikubwa cha Wapemba kilikuwa mbona Wapemba hatupati urais wa hii Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar? Mungu amewasikia Wapemba. Rais ni mwana wa Pemba na Makamu wa Kwanza wa Serikali ya ushirikiano ni Mpemba – kilichobakia nini? Hivyo, Wazanzibari wanalotakiwa kufanya ni kujenga Taifa lao kiuchumi na kuboresha miundombinu.

 

Baada ya kuelewa hayo yote, ndipo mtu anajiuliza kwa nini Wazanzibari bado wana chuki na visasi miongoni mwa wao kwa wao? Kwa nini basi wasisahau ubaguzi ule wa kimbari wa zamani? Au kwa nini Wazanzibari hawawezi au hawataki kusameheana na kusema yaliyopita si ndwele tugange yajayo? Wakati naandika makala hii tumo katika awamu ya saba. Ni ya Wapemba jamani.

 

Mimi naona Wazanzibari walivyo sasa wote ni wazawa wa kizazi kipya Zanzibar. Hakuna Mwarabu, hakuna Mhindi, hakuna Mshirazi na wala hakuna Mwafrika wa kuja. Walioko Zanzibar sasa wote wamezaliwa pale, wamekulia pale, wamesoma pale na sasa wanafanya kazi pale.

 

Hakuna sababu za kuchukiana. Wote ni Wazanzibari safi hawa. Jambo la msingi la kulielewa ni kwamba Zanzibar ni ya Wazanzibari si ya Waarabu, si ya Washirazi, si ya Waafrika na si ya yeyote mwingine. Zanzibar ni ya Wazanzibari na Uzanzibari hauna kabila.

 

Ukweli ni kwamba Wazanzibari wengi zaidi ni watu wa mchanganyiko wa damu mbalimbali – mtu wa rangi yoyote anaweza kuwa Mzanzibari – na hivi ndivyo vilivyo hivi sasa. La muhimu ni kwamba mtu huyo amepata Uzanzibari wake kwa njia ya halali na kwa kufuata sheria za nchi kuhusu uananchi wa Zanzibar.