Vyama vikubwa Visiwani vilikuwa ARAB ASSOCIATION, INDIAN ASSOCIATION na AFRICAN ASSOCIATION. Na kutokana na vyama hivyo, vikajazaliwa vyama kama SHIRAZI ASSOCIATION na UMMA PARTY.
ARAB ASSOCIATION:
Chama hiki kilianzishwa na mamwinyi Waarabu mara baada ya sheria ya kukomesha utumwa Zanzibar ilipoanza kutumika (Zanzibar Slave Decree) mwaka 1909. Kilikuwa na madhumuni ya kudai haki za Waarabu kwa kuachiwa watumwa wao huru:-
(i) Kilidai fidia kutoka kwa Mwingereza
(ii) Kilitaka hadhi ya Waarabu ilindwe katika mambo ya Serikali na umilikaji ardhi.
(iii) Kilidai Waarabu watayarishwe katika mambo ya utawala na;
(iv) Kilikataa nafasi za utawala kutolewa kwa Waafrika wala kwa Wahindi. Arab Association iliwahesabu Waafrika wote kuwa ni wageni (Gazeti la Alfalaq Zanzibar, na Kitabu “Mapambano ya Ukombozi” TPH by Mrina na Mattoke uk. 63.)
INDIAN ASSOCIATION:
Kilianzishwa mwaka 1910. Madhumuni yake yalikuwa kutetea masilahi ya biashara za Wahindi. Pili, walikuwa wanapambana na mabepari Waarabu kudai fedha walizokopesha (money lenders) ambako Waarabu wengi walishindwa kulipa, hivyo walinyang’anywa ardhi zao walizoweka rehani wakati wa kukopa.
AFRICAN ASSOCIATION
Waafrika hawakuwa wanatambuliwa na Mwingereza kama watu, hivyo waligawanywa gawanywa wasiweze kabisa kuungana. Mzungu mmoja, Bwana Shamba Mkoloni aliwakejeli kwa kusema hivi, nanukuu; “Ni wazi kwamba Mwafrika si sawa na Mzungu katika akili, maadili na maumbile. Waafrika wa Zanzibar kama SAA KUBWA ya UKUTANI. Wanahitaji kila wakati kuhimizwa na kukemewa. Ni kama watoto ambao wana hulka za Waarabu ambao wamewafunza”.
Nadhani ni kweli (Tazama kitabu cha Gallagher: “Afrika and the Victorious”, pia kitabu “Mapambano ya Ukombozi ZANZIBAR” (TPH) – Mrina & Mattoke uk. 28). Kwa kejeli namna hiyo Mwafrika hakuweza kuaminiwa kuunda chama.
Basi, ikatumika mbinu ya kuunda klabu za mpira. Klabu hizi za michezo ya mpira ndiko mahali Waafrika walikoweza kujikusanya na kukaa pamoja kupeana mawazo. Mwaka 1933 klabu hizi zikavunjwa na kukaundwa klabu moja iliyojulikana kama “African Sports Club”.
Mwaka 1934 wanamchezo wale waligeuza chama kile na kuwa Chama cha Waafrika (AFRICAN ASSOCIATION). Kilijumlisha wanaume na wanawake. Madhumuni ya African Association yalikuwa kukomesha manyanyaso wanayoyapata Waafrika kule Visiwani. Lakini ili chama kitambuliwe, ilibidi kiandikishwe serikalini kama vile vingine. Serikali ya mkoloni ikihofia Waafrika kuamka kutoka usingizini, ilileta vitimbwi vya kuwagawa ili wasambaratike.
Kwanza, iliwaambia Waafrika kuwa African Association ni chama cha Wakristo; oneni nyimbo zao nyingi ni za kidini. Mkiingia huko mtabadilishwa imani zetu. Pili, walisema African Association ni cha watoka Bara – watumwa walioachwa huru – ninyi wa Zanzibar na Pemba ni wa asili ya Washirazi, msijiunge na chama kile.
Uchochezi huo ulizaa matunda yaliyokusudiwa kuwatenganisha Waafrika wa Zanzibar katika makundi mawili. Baadhi ya Waafrika walijitoa, walifukuzwa kutoka AA. Hao ndiyo walioanzisha chama kipya cha wenyeji wa Visiwani na kikaitwa SHIRAZI ASSOCIATION kilichoundwa mwaka 1938.
Inafaa hapa kuelewa Washirazi ni watu gani kwa kadiri ya tafsiri ya Sheikh Issa bin Nasser Al-Ismaily, ambaye ni Mwarabu wa Oman. Anasema hivi na namnukuu “… wakiwa Washirazi au Waarabu wote hao ni jinsi moja. Mshirazi wa kizazi cha Zanzibar na Mwarabu wa kizazi cha Zanzibar ni kitu kimoja. Huyu aitwaye Mshirazi ndiye Mwarabu mwenyewe na huyu aitwaye Mwarabu ndiye Mshirazi mwenyewe”. (Tazama ZANZIBAR Kinyang’anyiro na Utumwa uk. XXXIX ibara ya kwanza).
Hapo ni wazi Mshirazi ni Mwarabu wa kule kusini mwa Irani, mji uitwao Shirazi. Walifika Visiwani Zanzibar tangu mwaka 924, ambako Waarabu wa Oman walifika miaka ya 1840 hivi. Hivyo mazalia ya Waarabu wale Washirazi na wananchi wa asilia visiwani ndiyo hao Waswahili. Mwarabu anawatambua kama wenyeji wa asili Visiwani.
Zanzibar kukawa na vyama vinne kila kimoja na madhumuni ya kutetea kundi moja la watu wa Zanzibar kutegemea mbari zao – Waarabu, Wahindi, Waafrika na Washirazi. Lakini kile chama cha Waarabu kilijiona ni bora zaidi kuliko vyama vingine, basi kikawa mstari wa mbele kupambana na mkoloni Mwingereza. Mwaka 1946 Mwingereza alishirikisha Waarabu na Wahindi katika Baraza la Kutunga Sheria. Na kwenye miaka ya mwanzoni mwa 1950 hivi, mkoloni akaona wakati umefika na Waafrika washirikishwe. Hapo sasa Mwarabu akang’aka. Itakuwaje bwana na mtwana wakae pamoja kutunga sheria?
Aliona jambo lile lingekuwa kushusha hadhi ya jamii ya Kiarabu kule Zanzibar. Hapo basi Arab Association ikalisusia Baraza la Kutunga Sheria mwaka 1955. Ndipo sasa Mwarabu akakigeuza kile chama chake cha Arab Association kiwe ni chama cha siasa na kidai Uhuru wa Zanzibar kutoka kwa Mwingereza. Akakibadili jina na kikaitwa “HIZBU el WATAN ili RAIATI SULTAN” yaani Chama cha Raia wa Sultani. Lakini jina hili la Kiarabu kwa Kiingereza ndilo lililoitwa “The NATIONALIST PARTY of the SUBJECTS of the SULTAN of ZANZIBAR (NPSS)”.
Dhahiri chama hiki ni cha mbari ya Waarabu tu. Mwafrika huthubutu kujiunga humo. Tangu hapo kikabadilisha jina na kuitwa HIZBU au Zanzibar National Party (ZNP) kwa hiyo kinajulikana zaidi kisiasa kama HIZBU (ZNP). Kuanzia hapo Waafrika wakaona upungufu wa kuwa na vyama viwili eti cha wabara, African Association na cha wazawa wa Zanzibar na Pemba walioitwa Washirazi yaani Shirazi Association.
Ndipo waliamua kuviunganisha ili wawe nao na nguvu ya kupinga utawala wa Mwingireza na wa Sultani. Basi, Februari 1957 vyama hivi vikaungana na kuitwa Afro-Shirazi Party (ASP). Ikumbukwe kuwa Zanzibar ilikuwa inakaliwa na watawala wawili, kwa hiyo Uhuru halisi ulikuwa kung’olewa Mwingereza na hatimaye kumng’oa Sultani Mwarabu.
Kulitokea mfarakano katika ASP uliosababisha baadhi ya Washirazi watoke au wafukuzwe kutoka ASP, na hatimaye waliunda chama chao kilichojulikana kama ZANZIBAR and PEMBA PEOPLES PARTY (ZPPP). Pia wakati huo huo aliyekuwa Katibu Mkuu wa ZNP, Abdulrahman Mohamed Babu, alijitoa ZNP na kuunda chama chake chenye kuwa na fikra za kimapinduzi na kuipinga vikali Serikali ya Sultani na mamwinyi wa Kiarabu.
Chama hiki kilifanana kiasi na ASP katika kudhamiria kuwatetea wanyonge. Hiki kiliitwa UMMA PARTY. Waarabu walikiita chama hiki cha Babu eti ni “KIRUKIA” (parasite) – mti wenye usugu usiokuwa na mfano – ni wa hatari sana. Licha ya kufungwa jela na wakoloni na vitimbwi vingi (alivyofanyiwa na Ali Muhsin, kiongozi wa ZNP, Babu alitorokea Dar es Salaam), lakini chama chake cha Umma kilikua na kupata wafuasi wengi waliopendelea kuwatetea wanyonge na kupinga usultani na umwinyi wa Waarabu. Hivyo Zanzibar ikajikuta ina vyama vinne vya siasa – ASP, ZNP, ZPPP na Umma Party.
Historia hii nimeitoa kuchimbua mzizi halisi wa mtafaruku huko Visiwani. Uhasama ulianzia mbali huko nyuma vyama vya siasa vilipoundwa. Waarabu walichukizwa kuona Waafrika wanataka Uhuru na kuwa sawa nao. Waarabu walidiriki kutamka kuwa ASP kilikuwa chama cha wageni kutoka Bara, na kwamba chama halali Visiwani kilikuwa ZNP, kile chama cha raia wa Sultani.
Mbinu zilifanywa kuzuia hata Mzee Abeid Amani Karume asijiandikishe kuwa mpigakura. Alishitakiwa mwaka 1957 na kuzuliwa kuwa aliingia Visiwani akitoka Bara. Penye ukweli uongo hujitenga. Basi, kesi hiyo ilifutwa Juni 11, 1957 pale ilipothibitika kuwa Karume alikuwa na umri wa miaka 49 wakati mshitaka wake Mwarabu aliyeitwa Ali Ahmed Riyami (na washiriki wake Waafrika wanne) alikuwa na umri wa miaka 37 tu. Ingewezekanaje kijana huyu mdogo amwone Karume anaingia Visiwani kwa ngarawa kutoka Bara wakati alikuwa hajazaliwa? Ndiyo visa vya Visiwani. Yale yale ya hadithi ya mbwa mwitu na mwanakondoo katika kitabu cha Esopo.
Ulifika wakati Waafrika Unguja na Pemba walitoa matamshi namna hii nanukuu “…sisi watu weusi wa Unguja na Pemba tumeshituka kujua kwamba wahamiaji wachache wana njozi za ajabu na potofu kwamba Visiwa vya Unguja na Pemba si nchi halali za Waafrika, bali kwa bahati mbaya Waafrika wamejikuta katika Visiwa hivi. Mtu yeyote mwenye njozi kama hizi lazima afahamu kwamba anajidanganya” (Gazeti la Afrika Kwetu toleo la 13/06/1957). Kuna wakati mwingine Waafrika walitoa matamko namna hii, nanukuu; “…Waasia ni Wahindi na Waarabu. Waarabu kama hawakushirikiana na Waafrika kwa kitendo chochote wafahamu hawataweza kuendelea zaidi”.
Wakati unafika Mwafrika anajivuna yupo kwao katika ardhi ya Mmama. Je, ninyi mpo katika ardhi ya nani? (Afrika Kwetu Aprili 25, 1957). Ifahamike tu kuwa kuna chuki na uhasama miongoni mwa wananchi wa Zanzibar kutokana na mbari zao tangu zamani sana.