Jeshi la Polisi nchini Kenya limetangaza kumkamata kijana Collins Jumaisi Khalusha (33) ambaye amekiri kuwaua Wanawake 42, baada ya kugunduliwa kwa miili tisa iliyokatwakatwa na kutupwa jalalani pembezoni mwa Mji mkuu wa Nairobi.

kwa mujibu wa mkurugenzi wa makosa ya jinai ( DCI) Mohamed Amin, amesema Collins amekamatwa na maafisa wa upelelezi wa jinai katika mtaa wa Kayole jijini Nairobi, akiwa klabu alipokwenda kutazama fainali ya michuano ya kandanda ya Ulaya iliyowakutanisha Uhispania na Uingereza Jumapili Julai 14.


Collins alianza kufanya mauaji kwa mara ya kwanza kwa kumuua mkewe mwaka 2022, na kuufunga mwili wake kwenye kiroba na kisha kuutupa jalalani, na mauaji yake ya mwisho alifanya Julai 11, 2024.

Collins amekamatwa baada ya uchunguzi wa kitaalamu wa simu ya mkononi ya mwanamke mmoja aliyemuua anayefahamika kwa jina la Josephine Owino.


Baada ya kukamatwa Polisi walikwenda katika chumba chake alichopanga jirani na eneo linapotupwa miili hiyo na kukuta laini za simu 24, panga, magunia ya nailoni ambayo yanayofanana na yale yaliyotumika kufungia maiti zilizookotwa, raba za viwandani, mikoba ya wanawake, na jozi mbili za nguo za ndani za wanawake zenye rangi ya pink, pamoja na vitu vingine.

Jeshi la Polisi lilifanya msako mkali kuanzia Ijumaa hadi Jumapili ambapo wamefanikiwa kupata miili tisa tu kati ya 42 ya wanawake waliouawa na Collins, katika eneo la Kware huku wengi wao wakikadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 18 hadi 30.