Makabiliano makali yamezuka katikati ya mji wa Nairobi baada ya polisi kuwatawanya waandamanaji wa kupinga muswada wa fedha wa 2024.
Umati wa waandamanaji ulikuwa umekusanyika katika barabara mbalimbali kupinga Muswada wa Fedha wa 2024 wakati makabiliano yalipozuka.
Polisi waliwarushia vitoa machozi waandamanaji waliokuwa wamejihami kwa maji na simu za rununu ili kueleza msimamo wao dhidi ya Muswada huo.
Umati huo ulianza kukusanyika mapema saa moja asubuhi karibu na Hifadhi ya Kitaifa ya Kenya.
Vikundi hivyo vilikuwa vikiimba kauli mbiu za pingamizi dhidi ya Muswada wa fedha huku maduka kadhaa yakisalia kufungwa katika maeneo mbalimbali ya katikati ya mji huo.
Waandalizi wa maandamano hayo, vijana ambao wanafahamika kama Gen Z wanatoa wito kwa zaidi ya watu milioni moja kujitokeza na kushiriki.
Maandamano hayo yaliyopewa jina la “Kenya Reject-Finance Bill 2024,” yamekuwa yakishika kasi na kuwavuta maelfu ya watu mitaani wiki jana kutoa upinzani wao.
Kulingana na michakato ya bunge, leo hii ni hatua ambapo wabunge hupitia Mswada kifungu kwa kifungu kinachopendekeza marekebisho katika kile kinachojulikana katika lugha ya bunge kama kamati ya bunge zima.
Muswada huo ulipita awamu ya pili wiki iliyopita baada ya wabunge 204 kuunga mkono huku 115 wakiupinga. Baada ya hapo muswada huo utasogea awamu ya tatu ambapo Bunge litaupigia kura ukiwa na marekebisho mapya.
Waandamanaji wanahoji kuwa mpango wa kukusanya kodi zinazopendekezwa za katika muswada huo zitazidisha hali ngumu ya kiuchumi kwa Wakenya wa kawaida.
Siku ya Jumatatu, serikali ilionya Wakenya wanaopanga kuandamana Jumanne dhidi ya aina yoyote ya ghasia na uharibifu wa mali.
Waziri wa Mambo ya Ndani Kithure Kindiki, mbali na kukiri kwamba kila Mkenya ana haki ya kuandamana au kulaani, alisisitiza kwamba waandamanaji hawapaswi kukiuka haki na uhuru wa wengine.