Bunge la Kenya limeidhinisha ombi la Baraza la Ulinzi la kutumiwa kwa Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF) kutoa ulinzi kufuatia maandamano ya kupinga muswada wa Fedha kote nchini.

Kulingana na Waraka wa Amri ya Ziada iliyopangwa Jumatano, Juni 26, hatua hiyo itaambatana na Kifungu cha 241 cha Katiba kinachohitaji kuidhinishwa na Bunge kabla ya wanajeshi kutumiwa kushughulikia masuala ya usalama wa ndani.

Hoja hiyo iliwasilishwa Bungeni baada ya ombi kutolewa na Baraza la Ulinzi siku ya Jumatano.

“Kwa mujibu wa Kifungu cha 241(3)(c) cha Katiba na vifungu 31(1)(b), 31(1)(c) na 32 vya Sheria ya Majeshi ya Ulinzi ya Kenya, Sura ya 199, Bunge hili linaidjinisha ombi la Baraza la Ulinzi la tarehe 26 Juni 2024 na, kwa maslahi ya usalama wa taifa, IMERIDHIA kutumwa kwa Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF) kusaidia Huduma ya Kitaifa ya Polisi katika maeneo mbalimbali ya Jamhuri ya Kenya yaliyoathiriwa na maandamano ya ghasia yanayoendelea. ambayo yamesababisha uharibifu wa miundombinu muhimu hadi hali ya kawaida irejeshwe,” sehemu ya ilani hiyo ilisema.

Bunge aidha, limeahirisha vikao vyake vya kawaida hadi Jumanne, Julai 23 vyombo vya habari vya ndani vinaripoti.

Hii inafuatia maandamano ya Gen Z ya kupinga Muswada wa Fedha ambapo vijana hao walivamia majengo ya bunge na kusababisha uharibifu na kuteketeza sehemu ya bunge hilo wakati wa maandamano hayo.