Muswada wa Haki ya Kupata Habari (ATI) uliowasilishwa bungeni wiki iliyopita umeboreshwa kwa kuulinganisha na miswada iliyotangulia awali, ila umebaki na makosa ya msingi yanayopaswa kufanyiwa marekebisho kabla ya kupitishwa bungeni, wadau wa habari wameshauri.
Uchambuzi uliofanywa na wadau wa masuala ya habari baada ya muswada huo kuwasilishwa umeonyesha kuwa musawada una upungufu katika kifungu cha sita kinachozungumzia habari zilizozuliwa.
“Kifungu hiki kimeweka maneno yanayoweza kuleta utata. Kwa mfano kinazungumzia suala la kuzuia habari zinazohatarisha masilahi ya kibiashara, masilahi ya taifa, uhusiano wa kimataifa, habari za askari waliopelekwa mahala na masuala mengine, lakini maneno hayo hayana tafsiri ya kisheria kueleza yanamaanisha nini,” anasema Makamu Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania, Deodatus Balile.
Balile anasema aliyeandika kifungu hicho amesahau kuwa Tanzania huwa inapeleka askari nje ya nchi kwa ajili ya ulinzi wa amani, lakini chini ya Sheria hii kuandika habari za jeshi kupeleka walinzi wa amani nje ya nchi litakuwa kosa ikiwa itapitishwa kama ilivyopendekezwa, wakati askari nao wanahitaji hamasa.
Pia, amesema muda uliowekwa wa kuhifadhi taarifa kabla ya kuziondolea usiri wa miaka 30 ni mwingi na baadhi ya taarifa zinaweza kupoteza umuhimu.
“Eneo jingine ni kifungu cha 6(6) hiki kimekaa vibaya mno. Adhabu inayotolewa inaonekana kama imelenga kukomoa, kwani wanasema yeyote atakayefanya kosa la kuchapisha taarifa zilizozuiliwa atafungwa jela si chini ya miaka 15 na si zaidi ya miaka 20. Ajabu kabisa, hakuna fursa ya mtu kutoa faini ni kifungo tu utafikiri ni jinai wakati kosa hili ni la madai. Hii ikibaki hivi inaweza kugeuka sheria mbaya kuliko zote hapa nchini,” amesema.
Balile ambaye pia ni Mjumbe wa Umoja wa Haki ya Kupata Habati Tanzania (CORI) ameeleza kushangazwa kwake na Serikali kutaka wachapishaji wa taarifa wapewe kifungo kisicho chini ya miaka 15, lakini kwa upande wa maafisa wa Serikali watakaofanya kosa chini ya sheria hiyo hiyo, wametumia maneno na utaratibu unaokubalika katika kutunga sheria chini ya kifungu cha 22.
Kifungu hicho kinasema: “Mtu yeyote ambaye anabadili, anafuta maandishi yasisisomeke, anazuia, anafuta, anaharibu au aficha kumbukumbu zozote zinazoshikiliwa na mmiliki wa taarifa kwa dhamira ya kuzuia upatikanaji wa taarifa kutoka kwa mmiliki huyo wa taarifa anatenda kosa na akitiwa hatiani atatozwa faini isiyozidi shilingi milioni tano au kifungo kisichozidi miezi kumi na mbili au vyote kwa pamoja.”
Anahoji inakuwaje adhabu inayotolewa kwa watoa habari inakuwa laini na yenye kufuata utamaduni wa Jumuiya ya Madola wa kutunga sheria, lakini inayotolewa kwa wachapishaji wa taarifa hizo inaweka vitisho vya ajabu. “Hapa sheria hii inaandaa mazingira ya kutisha watu wasitafute taarifa na haitoi adhabu yoyote kwa anayekatalia taaria. Hii si sahihi,” anasema Balile.
Mwanasheria huyo, anahoji kwa nini Sheria hii haikuanzisha chombo cha kupitia rufani za wanaokataliwa taarifa, ambapo kifungu cha 19 kinataka mtu kukata rufaa kwenye chombo ambacho hakikuelezwa kiko wapi, na mbaya zaidi chombo hicho kisichofahamika muundo wake, kifungu cha 19 kinasema mrufani asiporidhika na uamuzi wake anaweza kukata rufaa kwa waziri mwenye dhamana na uamuzi wa waziri utakuwa wa mwisho.
“Waziri ni mwanasiasa. Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 107A Mahakama ndicho chombo pekee chenye mamlaka ya kutoa haki hapa nchini, hivyo Waziri kufanya kazi ya Mahakama si utawala wa sheria. Mtu atakayekuwa hajaridhika na chombo hicho, ambacho sheria inapaswa kukitaja, basi aruhusiwe kwenda mahakamani,” anasema Balile.
Ukiacha upungufu huo, Balile amesema muswada huu uliowasilishwa bungeni na Waziri wa Sheria na Katiba, Dk. Harrison Mwakyembe, uko bora zaidi kuliko miswada iliyowasilishwa na mawaziri waliomtangulia, hivyo wabunge wanapaswa kurekebisha maeneo aliyoyataja kisha sheria hiyo itakuwa nzuri. “Baadhi ya wabunge wanaweza kudhani hii ni sheria kwa ajili ya wanahabari. Wasipotusikiliza wakaendelea nayo kama ilivyo, siku ikianza kuwaumiza watajuta,” ameongeza.
Dk. Mwakyembe wiki iliyopita amewasilisha Muswada wa Haki ya Kupata Habari bungeni ukasomwa kwa mara ya kwanza na kwa sasa muswada huo uko huru kujadiliwa na wadau kwa kutoa maoni yao wakilenga kuuboresha na kuipa Tanzania haki ya kupata habari ambayo ni haki ya msingi kwa maendeleo ya taifa lolote duniani.