*Barabara duni Ilala zamnyima usingizi

 

Amejikita zaidi katika masuala ya siasa, lakini taaluma yake ni ujuzi na maarifa ya kuunda, kutunza, kutengeneza na kuongoza mitambo ya ndege. Unaweza kumwita injinia wa ndege.

 

Huyu si mwingine bali ni Mussa Zungu Azzan, ambaye kwa sasa ni Mbunge wa Jimbo la Ilala kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).

 

Mtazamo wa kiongozi huyu ni kuendelea kutumia wadhifa huo wa kisiasa kutafuta maendeleo endelevu ya wananchi jimboni hapa na Taifa letu kwa jumla.

Alianza siasa lini?

Katika mahojiano maalum na JAMHURI Dar es Salaam wiki iliyopita, Zungu amejitaja kuwa ni muumini mkubwa wa Siasa ya Ujamaa tangu enzi za chama cha siasa cha Tanganyika African National Union – TANU).

 

Anafafanua kwamba alijiunga na TANU mwaka 1969, na muda mfupi baadaye akapewa wadhifa wa Katibu Msaidizi wa Tawi la chama hicho katika Shule ya Sekondari ya Tambaza, jijini Dar es Salaam.

 

Anabainisha kuwa alijielekeza kwenye siasa ili kupata fursa ya kushiriki ipasavyo katika harakati za kutafuta maendeleo endelevu ya Taifa letu, baada ya kukombolewa kutoka katika utawala wa kimabavu wa wakoloni.

 

“Faraja ni kwamba juhudi za Taifa letu zimechangia mafanikio ya ukombozi wa nchi mbalimbali katika Bara la Afrika kutoka mikononi mwa wakoloni,” anasema.

 

Juhudi za Zungu katika tasnia ya siasa zilimwezesha kuchaguliwa kuwa Diwani wa Kata ya Mchikichini, Dar es Salaam, katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000. Miaka mitatu baadaye alichaguliwa kuwa Naibu Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala.

 

Baada ya kuona wananchi wengi wana imani naye, alijitosa katika kinyang’anyiro cha ubunge katika jimbo hilo mwaka 2005, akashinda. Mwaka 2010 aligombea na kufanikiwa kuchaguliwa tena kuwa Mbunge wa Ilala.

 

Lengo langu katika harakati hizi ni kuhakikisha tunaendeleza udugu na uhusiano mwema ukiwamo wa kisiasa, kuboresha huduma za jamii na kupambana na umaskini miongoni mwa wananchi jimboni hapa,” anasema Zungu.

 

Mafanikio jimboni

Mbunge huyu anataja mafanikio yaliyopatikana Ilala chini ya uongozi wake kuwa ni pamoja na uboreshaji wa hospitali za Amana na Mnazi Mmoja. “Pia huduma ya maji imeboreshwa, idadi ya madawati katika shule mbalimbali imeongezeka na kwenye michezo tumejipanga vizuri,” anaongeza.

 

Kwa mujibu wa Zungu, mpango wa kusimamia michezo, hususan soka umeimarishwa, ambapo klabu 32 zimewezeshwa kushiriki mashindano ya ligi mbalimbali. Klabu za soka zimepatiwa vifaa na viwanja vimeboreshwa.

 

Zungu anaeleza kwamba mpango huo pia umefanikisha ujenzi wa kiwanja kipya cha michezo katika eneo la Kidongo Chekundu. Mbunge huyu anaongeza kwamba klabu ya soka ya Sunderland inayoshiriki Ligi Kuu ya Uingereza imekubali kusaidia kuinua klabu za soka za vijana wadogo katika jimbo hili.

 

“Kwa upande mwingine, tumeweza kuvisaidia vikundi vya wajasiriamali kwa kuvipatia elimu ya ujasiriamali na mitaji, lengo ni kuwapatia wananchi wengi ajira, hasa vijana ili wasijiingize katika vitendo vya uhalifu,” anasema.

 

Changamoto jimboni

Miongoni mwa matatizo makubwa yanayoikabili Halmashauri ya Manispaa ya Ilala, Dar es Salaam ni barabara duni, ambazo zimekuwa kikwazo kwa watumiaji, hasa wakati wa masika.

 

Zungu anathibitisha ukubwa wa tatizo hilo akilitaja kuwa miongoni mwa mengine kadhaa yanayomnyima usingizi. “Nina changamoto kubwa ya kuhakikisha tatizo hili linatokomezwa,” anasisitiza.

 

Bajeti ya uboreshaji wa miundombinu ya barabara hizo inategemea mapato ya fedha kutoka vyanzo mbalimbali vya Halmashauri ya Manispaa ya Ilala. Hata hivyo, Zungu anasema kumekuwapo na udhaifu katika ukusanyaji wa mapato hayo.

 

Changamoto nyingine zinazolikabili Jimbo la Ilala, kwa mujibu wa kiongozi huyu wa wananchi, ni kukomesha matatizo ya upungufu wa dawa, huduma duni za matibabu kwa wazee, kina mama na watoto hospitalini.

 

Anasema anaendelea kushirikiana na viongozi wengine kuihimiza Serikali itekeleze ahadi yake ya kuongeza bajeti ya kugharimia matibabu kwa makundi hayo ya jamii. Zungu anaongeza kwamba elimu ya kulipa kodi ya pango ni miongoni mwa changamoto zinazomzunguka. Kwamba elimu hiyo ikitolewa kwa wakazi wa Ilala itawezesha ongezeko la mapato ya manispaa hii.

 

“Mpangaji anatakiwa kulipa kodi ya pango serikalini, lakini wengi wanalipa kwa wamiliki wa nyumba, hili ni tatizo,” anasema Zungu na kuendelea: “Ikiwa wastani wa shilingi milioni 300 zinalipwa na wapangaji kama kodi ya pango kwa ghorofa moja kwa mwaka, hapo kuna kodi ya Serikali shilingi milioni 30, lakini wenye nyumba hawakubali.

 

“Wastani wa shilingi bilioni kumi hupotea kila mwaka hapa Ilala, kiasi hicho cha fedha zingetumika kugharimia huduma bora za jamii.” Anasema kimsingi jukumu la kufuatilia ili kuhakikisha asilimia 10 ya kodi ya pango inalipwa serikalini, ni la Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), lakini yeye kwa wadhifa wake wa ubunge, pamoja na jitihada nyingine, ataendelea kuihimiza Serikali iwaelimishe wahusika umuhimu wa kulipa kodi hiyo.

 

Ndoto ya Zungu

“Mungu akiendelea kunijaalia uzima na wapiga kura wakiendelea kunikabidhi ridhaa ya kuwatumikia, nitahakikisha ninaelekeza nguvu kubwa katika kutafuta uboreshaji zaidi wa huduma za jamii na kupambana na umaskini miongoni mwa wananchi. “Nitashirikiana na viongozi wengine kutafuta mikopo kwenye taasisi za fedha kwa ajili ya kugharimia uboreshaji wa huduma za jamii na maisha ya wananchi,” anasema mbunge huyu.

 

Wito kwa jamii

Zungu anatumia nafasi hii pia kutoa wito wa jumla kwa wananchi kujenga utamaduni wa kutekeleza wajibu wao kwa Serikali, ikiwa ni pamoja na kulipa kodi kwa mujibu wa sheria za nchi yetu. “Wananchi wawajibike kuchangia maendeleo yao. Maendeleo hayawezi kuletwa na Serikali pekee, na tusisahau kwamba mapato ya Serikali yanategemea kodi mbalimbali,” anasisitiza.

 

Kwa upande mwingine, ametoa wito kwa wanasiasa kujenga dhana ya kukubali matokeo ya chaguzi zinazofanywa na wananchi. “Wanasiasa tuheshimu uamuzi wa wananchi katika chaguzi mbalimbali,” anasisitiza Zungu.

 

Elimu ya Zungu

Mbunge huyu wa Ilala anasema alizaliwa mwaka 1952. Alipata elimu ya awali na ya msingi katika Shule ya St. Joseph’s (kwa sasa Forodhani) jijini Dar es Salaam kati ya mwaka 1958 na 1965. “Baada ya kuhitimu elimu ya msingi, nilichaguliwa kwenda kusoma katika Shule ya Sekondari ya Kinondoni mwaka 1966 hadi mwaka 1967 kabla ya kwenda katika Shule ya Sekondari ya Tambaza mwaka 1968 hadi 1969,” anasema.

 

Zungu anaeleza kwamba baadaye alikwenda Toronto, Canada kusoma sayansi na ufundi wa vyombo vya anga ukiwamo urubani hadi mwaka 1982. “Baada ya masomo nilifanya kazi za field aviation huko Toronto, Canada na katika Kikosi cha Anga Tanzania kabla ya kuanza shughuli zangu binafsi,” anasema Zungu.