Tuache lawama. Tunakuwa wa kwanza kulaumu kwamba mabadiliko ya tabia ya nchi yamebadilika na wakati huo huo tunakuwa wa kwanza kukata miti ovyo pasipo kupanda miti mingine.
Tunajenga viwanda ovyo pasipo kuzingatia usafi wa mazingira. Tuwe na sababu za kulaumu pale ambapo mchango wetu umeonekana lakini haukufaulu kushinda kwa lililokusudiwa.
Katika hali isiyo ya kawaida, unakuta serikali inafumba macho kwa taasisi zinazojenga viwanda kiholela pasipo kubaini athari za jamii husika na mazingira.
Inatosha kusema; dunia yetu haiwezi kuwa salama kama mazingira hayako salama. Hewa tunayovuta haiwezi kuwa salama kama mazingira yetu hayako salama.
Dk. Hans Heinz katika kitabu chake cha Mungu katika historia alitabiri kwa kusema: “Jinsi tunavyokaribia mwisho, ndivyo watu watakavyoendelea zaidi kuishi bila Mungu.” Ni kweli kabisa, kwa sababu dunia ya leo inatamani kuishi bila Mungu. Imefika mahali mwanadamu anafikiri kwamba, kuna mambo mengine ambayo Mwenyezi Mungu aliyapanga kimakosa au aliyaweka kwa kusahau. Inatia huruma.
Mababu zetu kwa mila na desturi za wakati wao waliyapenda mazingira na waliyalinda pia. Sayansi yetu inayatazama maisha waliyoishi mababu zetu kama maisha yasiyo na maono, lakini ukweli ni kwamba sayansi yetu ndiyo haina maono.
Sayansi pekee haiwezi kuyaongoza maisha ya binadamu. Binadamu si sayansi na hawezi kuwa sayansi kamwe. Binadamu anatakiwa kuiongoza sayansi na si sayansi kumwongoza binadamu.
Ni kwa bahati mbaya kuwa uelewa wa sayansi unavyozidi kuwa mpana, ndivyo na sayansi yetu inavyozidi kuwa haribifu. Mwandishi Kornrad Lorenz alimnukuu Papa Paul II akisema: “Mwanadamu yu karibu kujiangamiza mwenyewe.” Jamii yetu kwa kujua au kutokujua imeshindwa kutunza mazingira kwa kisingizio cha ujio wa Sayansi na Teknolojia.
Ni kama dunia inaelekea kuangamia. Dunia yetu inaelekea kuwa jangwa kavu. Tutaishi wapi kama dunia yetu itageuka kuwa jangwa? Tutalima wapi kama dunia yetu itageuka kuwa jangwa? Mazingira yakiangamia na binadamu ataangamia. Mazingira yakipotea na binadamu atapotea.
Mwandishi wa Marekani, Sallie Mcfague, anasema: “Kutokutunza mazingira ni kuangamiza maisha yetu.” Leo, kuliko wakati mwingine wowote wanahitajika wanaume kwa wanawake ambao ni watetezi wa mazingira. Mazingira yetu yanahitaji kutunzwa, kulindwa na kupendwa.
Papa Fransisko anatukumbusha kwa ujumbe huu: “Tumeupokea ulimwengu huu ukiwa ni urithi kutoka kwa kizazi kilichopita. Lakini pia ni kama mkopo wa kizazi kijacho, ambao tunapaswa kuukabidhi kwao ukiwa salama.”
Hatupaswi kukubali kuitafuta dunia nyingine ya kuishi, lakini tunalo jukumu la kuiweka dunia hii tunayoishi katika hali ya ulinzi na usalama.
Tuipende dunia yetu tunayoishi. Tuyapende mazingira yetu tunayoishi. Kutunza mazingira ni suala la kimaadili. Bahati mbaya inayomkumba binadamu wa leo ni kwamba “binadamu wa leo hana maadili ya kutunza mazingira anayoishi.” Sura ya dunia imebadilika kwa sababu ya uharibifu wa mazingira.
TAMATI…