Mahakama Kuu huko Abuja amemhukumu Peter Nwachukwu, mume wa mwimbaji maarufu wa injili Osinachi, kifo kwa kunyongwa kwa kupatikana na hatia ya mauaji.
Hukumu hiyo, iliyotolewa na Jaji Nwosu-iheme, inatolewa miaka mitatu baada ya kifo cha Osinachi kilichotokea mnamo Aprili 8, 2022.
Kesi hiyo imevutia nadhari kwa sababu ya umaarufu wa Osinachi katika muziki wa injili wa Nigeria na jamii ya Wakristo.
Polisi walikuwa wamemkamata Bwana Nwachukwu baada ya mkewe, kufariki akiwa katika hospitali moja huko Abuja.
Ripoti za awali zilikuwa zimependekeza kwamba mwanamke huyo aliyekuwa na umri wa miaka 42 alikuwa mgonjwa wa saratani ya koo, lakini familia yake ilikataa na kudai kwamba alikuwa mwathirika wa unyanyasaji wa nyumbani.
Walimshutumu mumewe kwa unyanyasajina kusababisha kifo cha mke wake.
Baadaye mahakama iliamuru kwamba arudishwe kizuizini gerezani. Bwana Peter Nwachukwu alishtumiwa kwa “vitendo vya vurugu na kumshambulia mkewe na ufahamu kuwa kifo hicho kitakuwa ni matokeo ya matendo yake.”
Mashahidi 17, pamoja na watoto wawili, waliitwa na upande wa mashtaka wakati wa kesi hiyo. Hati 25 pia zilitolewa kama kithibitisho mbele ya mahakama.
Marehemu Osinachi na mume wake aliyehukumiwa Peter Nwachukwu walijaaliwa watoto wanne.
