Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Njombe
Jeshi la Polisi mkoani Njombe, linamshikilia Juma Kyando (36), mkazi wa Dombwela, wilayani Makete mkoani Njombe kwa tuhuma za kumkata kata vipande mkewe kisha kwenda kuvitupa mtoni.
Akizungumzia tukio hilo kwa niaba ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Mkuu wa upelelezi mkoani humo, Mrakibu wa Polisi Joseph Mwalongo amesema kuwa tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia Januari 8, 2024 katika mtaa wa Dombwela.
Kamanda amesema kuwa mtuhumiwa amemkata kata marehemu mke wake Tumaini Luvanda (35), kwa kumtenganisha kichwa na kiwiliwili na kisha kwenda kutupa baadhi ya viungo katika mto ulio jirani na nyumba yake eneo la Kabinda wilayani hapo.
Amesema kuwa Jeshi la Polisi limesikitishwa na kitendo hicho kwani mtuhumiwa alikuwa akiwatishia majirani na panga waliokuwa wakitaka kuamua ugomvi kutokana na marehemu kupiga kelele za kuomba msaada.
‘Niwape pole kwa niaba ya Kamanda wa Jeshi la Polisi, mwenzetu huyu Juma (mtuhumiwa) amejichukulia sheria mkononi, Jeshi la Polisi lazima tumchukulie hatua za kisheria ili iwe fundisho kwa wengine wanaojichukulia sheria mkononi” amesema.
Hata hivyo amesema kuna watu wanasumbuliwa na msongo wa mawazo hivyo ni vyema kama kuna mtu ana changamoto akamshirikisha rafiki yake ili apate ushauri.
“Nawaombeni msiyarundike matatizo yenu kichwani shirikisheni watu ndugu na jamaa ili kusaidia kupatikana kwa ufumbuzi’ amesema Mwalongo.
Naye Mwenyekiti wa Mtaa wa Dombwela, Joseph Mbilinyi, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo katika mtaa wake na kusema kuwa baada ya kupata taarifa za kuwepo kwa ugomv huo alikwenda haraka eneo la tukio lakini hawakuweza kufanya jambo lolote kutokana na mtuhumiwa kushika panga.
‘Nilipigiwa simu na jirani kuwa kuna mtu anamshambulia mke wake, baada ya kufika pale nikakuta mtuhumiwa ameshika panga na anatishia kukata watu.
” Nikiamua kupiga simu Polisi kuomba msaada mpaka Jeshi la Polisi likafika usiku huo yayaro mtuhumiwa alikuwa ametekelezs azimio lake’ amesema mwenyekiti.
Ameongeza kuwa baada ya kutekeleza unyama huo mtuhumiwa alikwenda kutupa viungo vya mwili wa marehemu mkewe kwenye mto ambao upo karibu na nyumba yao.
‘Baada ya kumuua kwa kumkakata vipande, alimuweka kwenye mfuko kisha kwenda kutupa kwenye mto, na wakati tunatafuta baadhi ya viungo tulikuta uwanjani kuna moyo na viungo vingine vya marehemu ,tukaanza kufuata alama za mfuko aliokuwa akiburuzwa mpaka kwenye mto.
“Tukaona baadhi ya viungo vikielea juu ya maji, tukaviopoa tukaanza kufuata , pia tunaona kiungo kingine ambacho ni titi na pia tukaona shingo.
” Tulipopata viungo hivyo tukaanza kutafuta kichwa hicho ndio kimetusumbua hadi kukipata kwa kuwa alikitupa sehemu tofauti’ amesema kwa masikitiko Mbilinyi.
Medrick Kyando ni ndugu wa mtuhumiwa amesema kuwa ameshangazws na tukio hilo la kinyama kwani ndugu yake hana historia ya kuwa na matatizo ya akili.
‘Ndugu yetu hana historia ya tatizo la afya ya akili kwani ni fundi ujenzi mzuri tu sijui kitu gani kimempata.
” Inasikitidha sana sasa mama yuko mochwali,baba yuko Polisi na watoto wapo watatu ni wadogo sana sijui wataishi mazingira gani, lakini kwa hili ni fundisho kwa tulio hai tujifunze kupitia kwa ndugu yetu ukikumbwa na changamoto yeyote mwambie hata rafiki au mtu yeyote atakusaidia” amesema Kyando.
Baadhi ya majirani waliohojiwa walisema wameshangazwa sana na tukio hilo na kusema kuwa mtuhumiwa na marehemu walikuwa wakiishi vizuri na hawakuwahi kupigana.
” Hatuwezi kujua nini kimemsibu jirani mpaka kuchukua masmuzi magumu kama haya ambayo hatasimuliki, kwa kweli ametusikitisha sana tena sana kwa kitendo alichonfanyia marehemu mkewe” amesema kwa uchungu Daniel Mwamengo.