Na Lookman Miraji, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Tamasha maarufu la mchezo wa ngumi ambalo hufanyika kila disemba 26 ya mwaka husika katika miaka ya karibuni lijulikanalo kama Boxing Derby linatarajiwa kufanyika mwaka huu wilayani Muleba mkoani Kagera.

Tamasha hilo ambalo huandaliwa na kampuni ya uratibu wa mapambano ya ngumi ya Peaktime promotion agency linatarajiwa kufanyika mwaka huu likijumuisha mabondia wa kulipwa wa kitanzania ambao watachuana katika tamasha hilo.

Akizungumza wakati wa utambulisho wa pambano hilo, Mratibu wa matukio kutoka kampuni ya Euromax limited, Bwn: Bakari Khatibu amesema kuwa pambano hilo linafanyika kwa mwaka huu ikiwa sehemu ya kusheherekea ujio wa aina mpya ya kifungashio kwa vinywaji aina ya Smart gin ambazo zinatarajiwa kuzinduliwa kupitia tamasha hilo boxing.

Aidha Bwn: Bakari ameongeza kuwa kampuni hiyo mara zote imekuwa ikizingatia ubora wa bidhaa zake huku akielezea kuwa ujio wa aina hiyo mpya kifungashio kwa bidhaa hizo umekuja ili kukabiliana hali ya usalama kwa wanamichezo viwanjani.

Pambano kuu la ngumi katika tamasha hilo linatarajiwa kuwa kati ya bondia wa kimataifa wa kitanzania Abdallah Pazi( Dulla mbabe) ambae atapanda ulingoni dhidi ya bondia mkongwe wa ngumi za kulipwa nchini Mada Maugo.

Kwa upande wa bondia Abdallah Pazi ( Dulla mbabe) ametamba kuwa amejiandaa vizuri kuelekea pambano hilo na kuahidi kuwa atampiga bondia Mada Maugo.

Mbali na pambano hilo kuu pambano jingine linatarajia kuwakutanisha mabondia kati ya Karim Mandonga dhidi ya bondia Said Mbelwa.

Nae bondia Karim Mandonga kama ilivyo kawaida kwake kuwa na utajiri wa maneno ametamba kuwa yuko kamili kukabiliana na bondia bondia Said Mbelwa katika pambano hilo la siku ya boxing.

Tamasha hilo linatarajiwa kufanyika Disemba 26 mwaka huu katika uwanja wa zimbhihile wilayani Muleba mkoani Kagera .