Dar es Salaam
Na Mwandishi Wetu
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula, amesema Tanzania na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi Duniani (UNHCR) wataendelea kushirikiana katika kuwarejesha nyumbani wakimbizi wa Burundi.
Akizungumza wakati wa hafla ya kupokea hati za utambulisho kutoka kwa mwakilishi wa (UNHCR) nchini, Mahoua Parums na mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya Watu (UNFPA), Mark Bryan Schreiner, Balozi Mulamula amesema mashirika hayo yamekuwa na mchango mkubwa katika kuiunga mkono serikali kushughulikia masuala ya wakimbizi na kukuza maendeleo.
“Tumekubaliana na UNHCR kuendelea kushirikiana kwa karibu na Wizara ya Mambo ya Ndani katika mchakato wa kurudisha wakimbizi wa Burundi nchini kwao kusudi hali ya Burundi iendelee kutengamaa, kwani kurudi kwa wakimbizi hao kutachangia maendeleo ya Burundi,” amesema.
Balozi Mulamula amesema Rais wa Burundi, Evariste Ndayishimiye, alipofanya ziara nchini Oktoba mwaka jana, alitoa rai kwa wakimbizi wa Burundi kurudi kwao wakachangie maendeleo ya taifa hilo.
Amesema mwakilishwa wa UNFPA amekuja wakati muafaka ambapo serikali inatarajia kufanya sensa ya watu na makazi Agosti mwaka huu, hivyo kutoa rai kwa shirika kuwashirikisha na kuwawezesha vijana na wanawake wa Kitanzania katika maendeleo ya teknolojia.
“Rai yangu kwao ni kuwahusisha vijana na wanawake kwani UNFPA mbali na kushughulika na idadi ya watu wana programu ya kuwashirikisha na kuwawezesha vijana, ni vema washirikiane kwa pamoja na mashirika mengine ya Umoja wa Mataifa kwa maendeleo ya pande zote mbili,” amesema Balozi Mulamula.
Mwakilishi wa UNHCR, Parums, ameishukuru serikali kwa kuwapokea na kuwalinda wakimbizi kwa muda mrefu.
“Tumekubaliana kushirikiana katika kuwalinda na kuwasaidia wakimbizi na kuwapatia baadhi ya mahitaji muhimu. Tunaomba tuendeleze ushirikiano huu kwa maendeleo yetu,” amesema.
Naye Mwakilishi wa UNFPA, Schreiner, amesema UNFPA itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kuhakikisha kuwa inasonga mbele kimaendeleo, ikiwa ni pamoja na kusaidia katika zoezi la sensa linalotarajiwa kufanyika Agosti 2022 ili kuiwezesha Tanzania kupata takwimu sahihi kuhusu idadi ya watu na kuiwezesha kusonga mbele kimaendeleo.
Katika tukio jingine, Waziri Mulamula amekutana na kufanya mazungumzo na Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), Sarah Gordon-Gibson.
Pamoja na mambo mengine, viongozi hao wamejadiliana masuala mbalimbali ya kuendeleza na kuimarisha ushirikiano uliopo baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na WFP.