Na Isri Mohamed
Mwili wa muigizaji Grace Vicent Mapunda maarufu kwa jina la Tesa umezikwa leo Novemba 4, 2024 katika makaburi ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Awali kabla ya mazishi mwili wake ulipewa heshima za mwisho katika hafla iliyofanyika viwanja vya Leaders Club na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Naibu Waziri wa Sanaa, Utamaduni na Michezo, Hamis Mwinjuma pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila.
Akizungumza katika hafla hiyo, Naibu waziri Mwinjuma amewahakikishia wasanii kuusimamia vyema mfuko wa waigizaji ili uwasaidie inapotokea muigizaji amepata ugonjwa wa ghafla aweze kupatiwa fedha za matibabu.
Aidha Naibu Waziri Mwinjuma amesema serikali kupitia wizara yao ipo katika maongezi ya mwisho na mifuko ya hifadhi za jamii kuhakikisha wasanii wanaweza kuchangia katika mifuko ya jamii kwa hiari ili wapate kuwa na mafao.
Marehemu Grace alijipatia umaarufu mkubwa kupitia tamthilia nyingi, lakini mpaka umauti unamkuta alikuwa akihudumu kwenye tamthilia ya Huba akitumia jina la Tesa.