Mtoto Benjamin William Mkapa, alifundishwa kupika chakula na mama mzazi, Stephania, akiwa mdogo. 

Alipokwenda shuleni hapo kijijini Lupaso, Ndanda na hatimaye St. Francis Pugu na Makerere, alifundishwa kupika, kufinyanga, kubuni na kuchambua mawazo na kuyaweka sawa kama msomi mbunifu na mwandishi. 

Kitabu hiki ni zao la mpishi wa mawazo mahiri aliyebobea. Ni kitabu cha kurasa mia tatu na kumi na tisa, katika sura kumi na sita.

Kuna utangulizi ulioandikwa na Joaquim Chissano, Rais mstaafu wa Msumbiji. Pia kuna picha nyinge nzuri, na viambatisho viwili.  Mchapaji Mkuki na Nyota wamefanya kazi nzuri sana, sikubaini kosa hata moja.

Wasilisho hili linamega simulizi hii katika sehemu kuu tatu. Kwanza, tunapewa vionjo vitamu tukielezwa kuzaliwa kwake, kukua na kwenda shule. Hii ilikuwa matayarisho ya kufikia nia au azima yake ya maisha. Kisha tunaletewa mlo wenyewe (main course) uliosheheni kumbukumbu na ngano za huyo kijana – sasa mtu mzima akiwa kazini, mpaka akaukwaa urais wa Tanzania. Mwisho, tunaelezwa kwa ufupi maisha yake baada ya kumaliza ngwe yake ya miaka kumi ya urais.

 Kuzaliwa, malezi na elimu

Baba yake mzazi, mzee William Matwani, alikuwa mpishi msaidizi huko Misheni Ndanda. Wamisionari wakambatiza, wakamfundisha kusoma, kuandika na kuhesabu na kumfanya katekista. Alipelekwa Lupaso, ambapo alieneza dini na kufundisha bush school ya wamisionari.

Alimwoa Bibi Stephania Nambanga, ambaye hakujua kusoma wala kuandika. Walijaliwa watoto wanne – Benjamin akiwa wa mwisho. Kama ilivyo kwa kabila la Makua, Benjamin alipewa jina la ujombani, Mkapa. 

Mama hakuwa na muda wa kujifunza kusoma na kuandika, kwani yeye ndiye alikuwa msingi wa familia, akihakikisha analima, kulisha familia na kuwalea watoto.  

Alikuwa mkali lakini msikivu na mpenda haki. Wazazi hawa ndio vinara wa sehemu hii ya kwanza ya simulizi hii. Waliishi pamoja kwa uadilifu na heshima kubwa, na mapenzi ya pamoja kwa watoto wao.

Ingawa wazazi hawakwenda shule, walipenda sana watoto wao wote waende shule. Hii pamoja na kwamba Baba Matwani alikuwa na kipato kidogo lakini cha uhakika kila mwezi, kiliifanya familia ionekane iko tofauti. Hii ilisababisha wivu na hatimaye chuki kutoka kwa jamii.

Wivu huu na chuki ulisababisha tukio moja baya sana ambalo Mheshimiwa Mkapa analikumbuka kwa uchungu. Mwaka 1947, kulitokea ukame mkali, basi watu wakamleta mganga wa kienyeji akaamua kuwa mama mzazi (wa Benjamin) na bibi wa mama yake ndio walikuwa wameloga na kuzuia mvua. Walipigwa na kuteswa sana hadi padri Mzungu alipofanikiwa kuwanasua. Bibi wa mama aliaga dunia muda mfupi baada ya tukio hilo.

Kijana Benjamin na mwenzie mmoja ndio waliopata bahati ya kuendelea na masomo ya sekondari, kutoka darasa la watoto 25 hadi 30.   Kuchaguliwa ilikuwa bahati nasibu.

Shule ya Sekondari ya Ndanda ilikuwa kilometa 60 kutoka Lupaso. Yeye na wenzie walitembea kwa miguu, bila viatu, kwa siku mbili, wakiwa wamebeba kichwani vitu vyao ambavyo vilikuwa vimefungwa katika mkeka. Baadaye alipata sanduku la chuma.

Walimu wa Ndanda walikuwa wamisionari na walikazia sana sala na kazi (‘Ora et labora’).  

Wanafunzi walipika chakula chao wenyewe. Kwa kuwa kijana Benjamin alikuwa mdogo sana alipewa kazi ya kuosha vyombo. Kawaida alivibeba vyombo kichwani mpaka mahali pa kuvioshea na kuvirudisha. Anasema kubeba vyombo hivyo ndiyo sababu ana upara hadi leo.

Mwaka 1952, akiwa na umri wa miaka 15, aliamua kwenda seminari darasa la nane. Baada ya muda mfupi aliamua kuwa upadri haukuwa wito wake, akarudi Ndanda kuendelea na shule. Mwaka 1957, alichaguliwa kwenda St. Francis College Pugu ikiwa ni shule kuu ya Wakatoliki Tanganyika. 

Akiwa Pugu, kijana Benjamin alianza kupata mwamko wa kisiasa. Aliunga mkono harakati za kupata uhuru kwa kuandika barua kwa Mhariri wa Gazeti la Tanganyika Standard ambalo sasa ni Daily News, akiunga mkono hoja ya Uhuru. Barua ilichapishwa. Ila kijana Benjamin alitumia jina bandia!

Mhe. Mkapa alishinda mitihani yake ya kujiunga Chuo Kikuu Makerere, kwa kupata daraja la kwanza, akiwa kati ya wanafunzi watatu bora katika darasa la wanafunzi 51.

Makerere alikumbana na mambo mengi mapya. Alikuwa darasani na wanafunzi wa rangi tofauti, kwa mara ya kwanza alikwenda kucheza dansi ya kisasa, alipangiwa chumba cha kulala nk.

Mwamko wake wa kisiasa uliendelea. Alijiunga na Bodi ya Wahariri ya Gazeti la Transition, alikuwa mwanachama hai wa kikundi cha wanafunzi cha TANU, akiwa katibu na hatimaye mwenyekiti wake. Alishiriki  kwenye siasa za wanafunzi hapo chuoni. Aligombea urais na ingawa hakushinda, wanafunzi wa kike walimpigia kura nyingi si kwa sababu alikuwa na rafiki wa kike, ila kwa jinsi alivyoweza kujieleza kuliko mpinzani wake. Alikuwa ‘More articulate!’ (alijieleza kwa ufasaha).

Aliteuliwa Makamu wa Rais wa Serikali ya Wanafunzi, na hatimaye alikuwa mwenyekiti wa Baraza la Wawakilishi la Wanafunzi hapo Makerere. Alihitimu masomo yake Aprili 1962, miezi minne baada ya Tanganyika kupata Uhuru. Alipata shahada ya lugha na fasihi ya Kiingereza na Fonetiki.  Alikuwa tayari kuifukuzia nia na ndoto yake.

Maisha na kazi

Simulizi ya maisha ya utu uzima iko katika sehemu mbili.  Kwanza, ni alipoanza kazi mpaka alipogombea urais. Pili, ni maisha ya urais. Sehemu hii ya simulizi imejaa sifa, heshima na upendo mwingi kwa Mwalimu. Anastaajabu kwa jinsi Mwalimu alivyoiunganisha nchi katika kupigania vita vya ukombozi wa Bara la Afrika. 

Kama wazazi wake, mzee Matwani na Bibi Nambanga walikuwa mashujaa wa sehemu ya kwanza ya maisha yake, hakika Mwalimu ndiye shujaa katika sehemu hii ya pili. Anamuelezea Mwalimu kama labda alitumwa na Mungu kwa makusudi.

Akiwa mtu mzima na mhitimu wa Chuo Kikuu Makerere, Mheshimiwa Mkapa alipenda kuajiriwa kwenye Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje, kwanza ilishindikana, lakini baadaye akaambiwa, itawezekana kama ataajiriwa kwanza kama bwana shauri mkufunzi wa wilaya, wakati akisubiri.  Kwa hiyo aliajiriwa hivyo huko Dodoma Aprili 1962.

Baada ya miezi mine, Agosti 1962, aliitwa Dar es Salaam aende kujifunza udiplomasia Columbia, Marekani.

Baada ya mwaka mmoja alirudi nchini akaajiriwa wizarani. Kazi yake kubwa ilikuwa kuchukua muhtasari wa mazungumzo ya waziri wake au Mhe. Rais alipopata wageni. Anamsifia kwa ujasiri pale alipovunja uhusiano na Uingereza. Wakati huu Mhe. Mkapa alitumia muda wake binafsi ama kusoma habari Radio Tanzania Dar es Salam, ama kumchumbia Bi. Anna.

Siku moja aliambiwa anaitwa Msasani kwa Mwalimu. Walipaita Msasani nyumbani kwa Mwalimu ‘The Clinic’.  Mwalimu akamwambia anamteua kuwa Mhariri Mtendaji wa Gazeti la The Nationalist. Ilibidi aende Uingereza kujifunza mambo ya magazeti kwenye magazeti ya The Mirror.

Alirudi na kuanza kazi chini ya Mwalimu kama Mhariri Mkuu, Mhe. Mkapa alikuwepo Arusha wakati wa Azimio, mwenzie Nsa Kaisi ndiye aliyebuni neno la Arusha Declaration (Azimio la Arusha), walilitumia kwenye The Nationalist, Mwalimu akalipenda, basi hayo maamuzi yakaitwa hivyo.

Mhe. Mkapa aliruhusiwa kuhudhuria mikutano ya Kamati Kuu ya TANU, ambayo wakati ule ilitawaliwa na malumbano ya hoja na uchambuzi yakinifu ambao umepotea. Alihusika katika kutayarisha sera mbalimbali za chama kutokana na umahiri wake wa kumudu lugha.

Mwalimu na msaidizi wake, Joan Wicken, ndio waliomfundisha ujamaa na alivutiwa na msimamo wa usawa na umuhimu wa kujitegemea.  Aliunga mkono wazo la Jeshi la Kujenga Taifa na akamuomba Mwalimu akamkubalia ajiunge kwa hiari.   Alijiunga na kuhitimu. 

Siku ya kuhitimu Mwalimu alikuwa ndiye mgeni rasmi.  Mheshimiwa Mkapa alichaguliwa na wenzie kusoma risala na Mwalimu alicheka sana alivyomtambua kuwa ni yeye, kwani alikuwa amepoteza ratili nyingi za uzito. Alikuwa ‘slim fit’. Mheshimiwa Mkapa aliitwa huko ‘The Clinic’ Msasani mara kadhaa.

Aprili 1972 Mwalimu alimteua kuwa Mhariri Mtendaji wa Daily News. Muda mfupi baadaye Mwalimu alimteua kuwa Press Secretary wa Rais.  Anasema huu ndio ulikuwa mwanzo wa maisha yake kama mwanasiasa.

Mwaka huohuo, Mwalimu alimuagiza aanzishe Shirika la Habari Tanzania – SHIHATA na kuwa Mtendaji Mkuu wake. Mwaka 1976 akamteua Balozi huko Nigeria. Mwaka mmoja baadaye akaitwa tena ‘The Clinic’ na kuteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje. 

Hapa alikuwa kama msaidizi wa Rais, kwani Mwalimu ndiye aliyeendesha mambo ya Nchi za Nje. Alifanywa pia mbunge wa kuteuliwa. Aliteuliwa kuwa Balozi wa Canada mwaka 1982 na Balozi Marekani 1983 – 1984. Akateuliwa Waziri wa Habari na Utamaduni mwaka 1980 – 1982, Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje tena mwaka 1984.  

Anabaini kuwa kwa kweli Mwalimu aliipa familia mtihani mkubwa na hii hamahama, lakini familia chini ya Mama Anna walikubali na kupokea yote kwa mikono miwili

Hakika Mwalimu ndiye shujaa mkuu wa simulizi hii.  Mheshimiwa Mkapa anamuelezea Mwalimu kuwa:

Alikuwa jasiri, na kiongozi lazima awe jasiri. Alikuwa msikivu, kamwe hakumkatiza mtu hata kama alikuwa anaeleza pumba tu. Alikuwa mtu wa msimamo, hakuyumbayumba. Alikuwa mpatanishi na mjenga madaraja kuwaunganisha mahasimu. Alikuwa communicator wa ajabu.

Alikuwa fundi wa kutafuta sehemu za makubaliano kati ya wanaotofautiana. Alikuwa mtaalamu wa kutumia mawazo ya wengine kurutubisha na kuboresha ya kwake. Aliupa umuhimu wa kipekee umoja wa kitaifa. Hakupenda ukandamizaji, ndiyo sababu hakupenda kuikalia Uganda baada ya vita mwaka 1980.

Mheshimiwa Mkapa anasema: “Mwalimu alikuwa mwalimu wangu kwa kila kitu.”

Alikuwa mwana demokrasia, mtu aliyempenda kama mrithi wake – mwaka 1985 alipokataliwa na wenzie katika Kamati Kuu, Mwalimu alikubali. Alikuwa kiongozi mwenye maono – visionary, aliangalia masilahi na mustakabali wa taifa ndani na nje ya mipaka yake.

Wazazi wa Mheshimiwa Mkapa walifariki dunia akiwa waziri, wakiwa na furaha na faraja kwa mafanikio yake, ingawa hakuwa padri, daktari au mwalimu kama baba yake mzazi mzee Matwani alivyotaka.

Urais 

Baada ya kutafakari na kushauriana na rafiki zake, Mheshimiwa Mkapa anasema kwanza alimwambia Mama Anna juu ya kugombea urais. Mama Anna alisita kidogo, ila akakubali. Pili, alimweleza Mwalimu kwa barua, kwani alikuwa Butiama, kisha akakutana naye ana kwa ana. Alimpa Mwalimu sababu kuu nne za uamuzi wake wa kutaka kugombea.

Kwanza, alitaka kurekebisha na kurejesha uhusiano chanya kati ya chama na serikali yake, na vyama vya ushirika ambao ulikuwa umefifia. Pili, alitaka kuimarisha uhusiano na vyama vya wafanyakazi ambao walikuwa wanatishia kugoma kwa mara ya kwanza. Tatu, ilikuwa kurekebisha mahusiano mabaya na wahisani kuhusiana na kushamiri kwa rushwa. Nne, alitaka kurudisha uhusiano na mashirika ya fedha ya kimataifa ambao walikuwa wamekataa kuanzisha miradi mipya. Mwisho, aliwapima hao waliokuwa wamechukua fomu akaona atajilaumu hapo baadaye kama naye hatagombea.

Mwalimu alimshukuru, akamwambia hakuwaza kuwa naye angegombea, alikuwa anamfikiria mtu mwingine ambaye alikuwa anasitasita.  Akamwambia hatamzuia kama amefanya uamuzi huo.  

Mwalimu aliwaomba watu kadhaa kumuunga mkono, Mwalimu alipenda hasa uwezo wake wa kufanya maamuzi, Mwalimu alishiriki katika kampeni ambapo Mheshimiwa Mkapa alisisaitiza ilani, si mambo binafsi. 

Mdahalo wa wagombea wote ambao ulirushwa mubashara ndio ulimfundisha njia ya  ushindi.   Ulikuwa ‘Game Changer’ anasema.

Novemba 23, 1995 aliapishwa kuwa Rais. Katika kuunda Baraza la Mawaziri, Mwalimu alikataa kujihusisha, hakuwa muingiliaji – interventionist.  Mheshimiwa Mkapa hakuwa mgombea wa mtu. Kwa hiyo hakuna aliyetegemea fadhila.

Hali ya nchi ya uchumi ilikuwa mbaya sana, lakini anasema hakuogopa, kiongozi lazima awe jasiri.   Alikumbana na uzembe, kutowajibika na rushwa.

Kazi kubwa – kwanza ilikuwa kuwashawishi wahisani kuwa mambo yatabadilika. Nchi ilikuwa na madeni makubwa sana. Deni letu lilikuwa dola bilioni saba, tulisamehewa bilioni tatu, hii ilikuwa hatua kubwa sana na ilimfurahisha Mwalimu ambaye alikwishaanza kuumwa.

Mheshimiwa Mkapa aliamini kwamba tulihitaji kujiangalia upya na kujifikiria kimkakati upya namna tulivyo kuwa tunaendesha nchi.

Mheshimiwa Mkapa anasema kuwa walioiona staili yake ya ‘kusema na kuelekeza’ kuwa ilijaa kiburi na majivuno ilikuwa lazima kuonyesha kuwa hatatetereka.

Matokeo yake ni kwamba mapato yaliongezeka karibu mara tatu kutoka dola 612,587 mwaka 1995 kufikia dola 1,796,862 miaka kumi baadaye. Fedha za kigeni ziliongezeka kutoka uwezo wa kununua bidhaa za mwezi mmoja na nusu kufikia uwezo wa kununua bidhaa za miezi mitano na theluthi moja.  Riba za benki zilishuka kutoka asilimia 36 kufikia asilimia 15 mwaka 2005.

Ilianzishwa TRA kuimarisha ukusanyaji wa mapato Julai 1996. Ukaanzishwa mfumo wa VAT Julai 1998, Public Service and Act pamoja na Public Procurement Regulatory Authority (Wakalala wa Manunuzi) vilianzishwa mwaka 2001, Commission for Human Rights and Good Governance (Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora) ilianzishwa Julai 2001, Prevention of Corruption Bureau (Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa – Takukuru) nayo ilianzishwa. Mheshimiwa Mkapa akaitwa ‘Mr Clean’.

Regulatory Agencies (Wakala za Udhibiti) zilianzishwa, na nyingine nyingi zilianzishwa, ikiwa ni pamoja na Brela, EWURA, TCCRA, SUMATRA, Viwanja vya Ndege, Maji Safi na Taka, TANROADS na National Business Council – kuimarisha mahusiano na wafanyabiashara.

“Kati ya mageuzi tuliyofanya yaliyokuwa na utata sana ni kubinafsisha mashirika ya umma, mageuzi/maboresho ya utumishi na uuzaji wa nyumba za serikali.

Kwa kweli mashirika ya umma yalikuwa yanaendeshwa kwa hasara. Kuna wanaodai kuwa Mwalimu hakupenda ubinafsishwaji na alisema hivyo hasa wakati wa mtangulizi wake,” anasema. Mheshimiwa Mkapa anabainisha kuwa: “…lakini Mwalimu hakunisema, na sijui kwa nini, ukweli ni kwamba Mwalimu alikuwa pragmatist na aliona hali halisi.  Kwa bahati mbaya sikufuatilia utendaji wa mashirika.”