Tangu Oktoba, mwaka jana nimekuwa nikiandika juu ya fursa ya kilimo cha muhogo. Maandishi yangu haya yametokana na ziara niliyoifanya nchini China. Taifa hilo limetenga wastani wa dola za Marekani bilioni 5 kununua muhogo kutoka Tanzania. Kufikia mwaka 2020 nchi hiyo inataka kupunguza matumizi ya mafuta ya petroli na dizeni kwa asilimia 20.
Hii ina maana kuwa wanataka kuzalisha mafuta kutokana na mimea na mazao ikiwamo muhogo (biofuel). Uamzui huu ni fursa kubwa kwa mkulima wa Tanzania. Nimepata kuonyesha hesabu za kilimo cha muhogo, ambapo ekari moja kama mkulima ametumia mbegu aina ya kiroba inavyoweza kumpatia hadi Sh milioni 4.8.
Hii ni baada ya Tanzania kuwa imesaini mkataba na China wa kuuza muhogo nchini humo mwezi Mei, mwaka jana. Ni bahati mbaya kuwa awali Wizara ya Kilimo haikulipa kipaumbele suala hili, ila sasa kwa mujibu wa vyanzo vyangu baada ya kuliandika kwa kina na kueleza kinachotakiwa ndani ya mkataba huo, wizara imeanza kuamka kuna kampuni kama tatu sasa zilizosajiliwa kununua muhogo na kuendesha kilimo hicho hapa nchini.
Bado nafanya mawasiliano na kampuni hizo na punde nitaeleza mtandao wake, utaratibu zinaotumia kununua muhogo. Hata hivyo, wakati naendelea na mchakato huo ni mepata mawasiliano na watu kadhaa wanaoeleza muhogo unavyoweza kukuza uchumi wa wananchi. Nimeelezwa kuwa muhogo unaweza kuwa chanzo cha kumiliki viwanda.
Kwa mwananchi wa kawaida anayelima muhogo anaweza kumiliki mashine ndogo ya kusindika muhogo akazalisha unga wa muhogo na kuuza unga huo katika nchi za Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) na kwingine. Pia masalia ya unga wa mihogo anaweza kuyatumia kulisha mifugo kama ng’ombe, kuku na nguruwe.
Miti ya mihogo inayong’olewa shambani inaweza kusagwa kwa mashine maalum ikatoa vumbi la unga linalotumika kutengeneza mkaa na hivyo mtu akawa anapata faida mara nne hadi tano kutokana na kilimo cha muhogo shambani. Kilimo hiki ni fursa ya ajira kwa vijana wanaomaliza vyuo.

Nafahamu shuleni walimu wanatuahidi kazi za benki na viwandani, lakini tujifunze ujasiriamali. Ujasiriamali utatufanya tuwe wabunifu. Ingawa nimetumia muda mrefu kuandika habari za muhogo, ila nashawishika kusema kilimo ni fursa ya aina yake kwetu sisi Watanzania. Tumezungukwa na nchi kama Zambia na Kenya ambazo kwao njaa ni jambo la kawaida. Tukilima mahindi, tukasaga unga na kuuza katika nchi hizo tunavuna utajiri.
Nchi yetu inanunua mafuta ya mawese kutoka nchi za ughaibuni wakati sisi tunaweza kuzalisha. Katika dhana ya viwanda tunapaswa kuanza kuzalisha mazao kama mawese, kisha tuwe na kiwanda cha kusindika mafuta.

Kwa kufanya hivyo tutakuwa tumeongeza faida katika kilimo chetu. Nchi yetu itakuwa imeongeza mnyororo wa thamani na kutengeneza ajira nyingi zaidi Katika makala zote nilizoziandika naomba kuwashukuru wasomaji kwani wengi wameonesha nia ya kuungana nami kuhakikisha tunaondoka katika umaskini kwa kuendesha kilimo cha kisasa na chenye tija katika muhogo na mazao mengine. Mungu ibariki Tanzania.