*Hospitali yakumbwa na upungufu mkubwa wa damu salama, wagonjwa hatarini
*Ikiomba chupa 150 kutoka Mpango wa Damu Salama, inapewa 12 kwa siku
*Mkurugenzi aomba Watanzania kuacha kasumba ya kuogopa kuchangia damu
*Tatizo limeanzishwa na Wizara ya Afya kuagiza wagonjwa wawekewe damu bila ndugu kuchangia
Dar es Salaam
Na Waandishi Wetu
Hali si shwari katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) iliyopo jijini Dar es Salaam, JAMHURI linafahamu.
Hii inatokana na uhaba mkubwa wa damu unaoikabili hospitali hiyo kubwa nchini kwa takriban miezi miwili sasa, huku juhudi za ukusanyaji damu salama zikionekana kugonga ukuta.
Uchunguzi wa Gazeti la JAMHURI umegundua kwamba mahitaji ya damu salama ya Muhimbili kwa siku ni kati ya ‘unit’ 80 hadi 120, lakini hadi wiki iliyopita hospitali hii imekuwa ikipata si zaidi ya ‘unit’ 12 tu kwa siku.
Unit moja ya damu ni sawa na mililita 450, hivyo kwa lugha rahisi mahitaji ya damu salama kwa Muhimbili ni kati ya lita 36 hadi 54 kwa siku, lakini upatikanaji wake kwa sasa ni chini ya lita sita tu kwa siku, hivyo kuwatia hofu watu wenye wagonjwa wanaohitaji kuongezewa damu.
JAMHURI limeelezwa kwamba juhudi za Muhimbili kwa upande mmoja na Mpango wa Taifa wa Damu Salama (NBTS) Kanda ya Mashariki kwa upande wa pili kukusanya damu kwa ajili ya watu wenye mahitaji, zimeshindwa kuzaa matunda.
Alipoulizwa kuhusu uhaba wa damu salama Muhimbili, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Profesa Abel Makubi, ameliambia JAMHURI kuwa suala hilo wenye uwezo wa kulitolea ufafanuzi ni Muhimbili wenyewe.
Akizungumzia hali ilivyo hospitalini hapo, Mkurugenzi wa Huduma Shirikishi na Tiba wa MNH, Dk. Praxeda Ogweyo, anakiri kuwapo kwa uhaba wa damu salama Muhimbili.
“Zamani timu yetu ilikuwa na uwezo wa kukusanya unit 40 za damu kutoka kwa jamii, lakini hali imebadilika. Wakienda mitaani wanapata unit nne hadi tano tu,” anasema Dk. Praxeda.
Nini chanzo cha uhaba huu?
Dk. Praxeda anataja sababu kadhaa zilizoleta uhaba wa damu salama Muhimbili, mojawapo ikiwa ni maelekezo yaliyowahi kutolewa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (wakati huo) mwaka jana kwa wakurugenzi wa hospitali 11 nchini.
Barua inayodaiwa kusababisha hali hii ni ya kutoka wizarani yenye Kumb. Na. DA.126/156/159/01/12 ya Desemba 2, 2021 (nakala tunayo) ikiwa na kichwa cha habari: ‘Hospitali kusitisha utaratibu wa kulazimisha wagonjwa kuleta ndugu wa kuchangia damu kabla ya kupata huduma’.
Pamoja na kusitisha utaratibu huo uliokuwa umeanza kuzoeleka, barua inasisitiza ukusanyaji wa damu kufanywa na timu maalumu zilizopo kwenye kanda, mikoa, halmashauri na hospitali maalumu, kutoka kwa wachangiaji wa hiari (voluntary non-renumerated blood donations).
Hospitali zilizoandikiwa mwongozo huo wa wizara ni Muhimbili (Upanga na Mloganzila), Bugando (Mwanza), Benjamin Mkapa (Dodoma) na Rufaa Kanda ya Mbeya.
Nyingine ni KCMC (Kilimanjaro), JKCI, MOI, Ocean Road, Mirembe (Dodoma) na Kibong’oto (Kilimanjaro).
Lakini Dk. Praxeda anasema ukusanyaji wa damu salama kwa hiari umekuwa ukikumbana na changamoto nyingi, ikiwamo kupungua kwa kiwango kikubwa kwa wachangiaji.
“Juzi tumewaomba NBTS watupatie unit 150 za damu salama, lakini wametupatia unit 12 tu. Hapo unaweza kuona ukubwa wa tatizo,” anasema.
Mpango wa Damu Salama wazungumza
Kwa upande mwingine, Mpango wa Taifa wa Damu Salama (NBTS) nao wanakiri kuwapo kwa uhaba wa damu Muhimbili.
Akizungumza na JAMHURI, Ofisa Ubora na Viwango wa NBTS Kanda ya Mashariki, Samwel Mduma, anasema juhudi zinaendelea kuondoa tatizo hilo.
“Uhaba wa damu salama huwa upo wakati wote kutegemea kundi gani la damu linahitajika hospitalini kwa wakati husika. Hospitali zinapaswa kupunguza matumizi makubwa kwa kutumia bidhaa za damu kulingana na mahitaji,” amesema.
Mduma anasema NBTS huzipatia kati ya asilimia 40 hadi 45 ya mahitaji ya damu salama hospitali zote za Kanda ya Mashariki.
Anakiri kuwa kwa sasa NBTS huipatia Muhimbili kiwango kidogo cha damu salama kwa kuwa wao pia wanakusanya damu kidogo sana kwa sasa.
“Muhimbili wana timu za ukusanyaji damu salama, kama hata wao hawakusanyi vizuri ni kwa sababu hizo hizo. Ukusanyaji damu salama kwa Novemba na Desemba hupungua, tofauti na miezi mingine. Tatizo hili limekuwapo ingawa huwa si kubwa kama sasa,” anasema Mduma.
Anasema sasa hivi wamelazimika kukusanya damu hadi makanisani na misikitini kutafuta wachangiaji wa hiari huku wakitarajia ongezeko la wachangiaji baada ya kufunguliwa kwa shule za sekondari na vyuo.
“Damu inapatikana kwa binadamu, sasa kuna wakati hamasa ya watu kuchangia damu hupungua,” anasema.
Mduma hakutaka kuzungumzia iwapo agizo la serikali kusitisha ndugu wa wagonjwa kuchangia damu limechangia uhaba, akisema yeye ni sehemu ya taasisi yenye jukumu la kukusanya damu salama.
“Kiafya mtu anayechangia damu kwa hiari ni bora zaidi kuliko anayechangia kwa lazima. Ni muhimu hamasa ikabaki katika kuchangia kwa hiari,” anasema.
Anataja faida za kuchangia damu kwa hiari kuwa ni mchangiaji kutambua kiwango chake cha damu, kundi la damu yake na kupata ushauri sahihi ili kuimarisha kiwango chake cha damu.
Mduma anasema kampeni ya kukusanya damu salama katika viwanja vya wazi kama maeneo ya Karume imeshindikana kwa kuwa kwa sasa eneo hilo kuna ujenzi wa barabara unaendelea na watu hawapo.
JAMHURI linafahamu kwamba wamachinga walikuwa miongoni mwa wachangiaji wakubwa wa damu na huenda kuondolewa kwao mitaani kumepunguza ukusanyaji wa damu salama.
Dk. Praxeda anaunga mkono kauli ya Mduma wa NBTS akisema baadhi ya wachangiaji wakubwa wa damu waliokuwa wakikusanyika mijini kwa sasa wamehamisha shughuli zao.
Anasema mabadiliko ya hali ya hewa kama vipindi vya joto au mvua huathiri uwezo wa timu ya wakusanyaji wa damu salama wa Muhimbili.
“Kama kuna mvua hata uweke tamasha la muziki watu hawatakuja. Watanzania hawapendi kujitolea kwa hiari kwenye uchangiaji wa damu. Hii inatupa wakati mgumu sana.
“Kwa hiyo tumebaki kuwa na wachangiaji wa damu wale wale! Hata mitaani ambako timu yetu inakwenda kuhamasisha, wachangiaji wapya wanaojitokeza ni wachache sana,” anasema.
Miongoni mwa juhudi za Muhimbili kukusanya damu ni kukodi wanamuziki na watu wenye ushawishi ili kuhamasisha watu kujitokeza, hivyo kuiongezea mzigo wa gharama hospitali huku wakiambulia kiwango kidogo sana cha damu.
Wingi wa hospitali Kanda ya Mashariki nao unapunguza wigo wa ukusanyaji damu salama kwa Muhimbili, kwani hujikuta wakigongana na wenzao katika maeneo muhimu kama shule za sekondari na vyuoni.
“Unaweza kwenda eneo fulani na kumwomba mwenyekiti wa mtaa kwamba unataka kufanya kampeni watu wachangie damu, anakueleza watu wa Hospitali ya Amana walikuwa hapa jana tu.
“Unakuwa umekwama. Ni lazima ufikirie sehemu nyingine ya kwenda kukusanya damu kwa sababu watu hawawezi kutoa damu mara mbili ndani ya muda mfupi,” anasema.
Uatafiti wa ndani uliofanywa na Muhimbili umebaini kuwa madaktari, hasa wanafunzi, huomba damu kutoka benki ya damu ya hospitalini hapo bila kuzingatia vipimo vya mgonjwa wala mahitaji ya damu.
“Madaktari wanafunzi huogopa kufanya upasuaji kwa mgonjwa bila kuwa na damu. Wakati mwingine huwa ni wasiwasi tu kwa kuwa kuna upasuaji unaoweza kufanywa pasipo mgonjwa kuhitaji kuongezewa damu.
“Tumawaelekeza wakuu wa idara kutoa elimu kwa madaktari na manesi kuhakikisha wanaomba damu kwa kuzingatia vipimo vilivyofanywa kwa mgonjwa husika,” anasema Dk. Praxeda.
Uchache wa wataalamu wa kutenganisha bidhaa za damu nalo ni tatizo linaloikabili Muhimbili.
Kuhusu agizo la wizara, Dk. Praxeda anasema limesababisha manesi na madaktari kupata kigugumizi inabobainika kuwa mgonjwa aliyepo wodini anahitaji kuongezewa damu.
Anasema ndugu wa mgonjwa wanapoelezwa kujitolea damu, hugoma wakidai kuwa serikali ilikwishatoa mwongozo wa kuwapatia damu wagonjwa pasipo ndugu kutakiwa kuchangia.
Ugunduzi wa ziada
Uchunguzi wa Gazeti la JAMHURI umebaini pia kuwapo kwa uhaba wa mabegi ya kukusanyia damu Muhimbili.
JAMHURI linafahamu kwamba Bohari Kuu ya Dawa (MSD), wenye dhamana ya kupeleka Muhimbili na hospitali nyingine mabegi hayo, hawajafanya hivyo kwa miezi minne sasa.
Hospitali kubwa za Dar es Salaam, Muhimbili na Mloganzila, kwa pamoja zimesaliwa na maboksi mawili tu ya mabegi hayo.
Dk. Praxeda hakuwa tayari kuzungumzia suala hilo akisema bandarini lipo kontena la mabegi hayo likisubiri kushushwa kutoka kwenye meli.
Kwa nini watu hawachangii damu?
Akizungumzia sababu ya Watanzania kutokuwa na hamasa ya kuchangia damu, Fundi Msanifu Mkuu wa Kitengo cha Uchangiaji Damu na Msimamizi wa Maabara wa Muhimbili, Mariana Shirima, anasema husababishwa na saikolojia ya watu, wakiamini kuwa taarifa zao zitawekwa wazi hivyo hali ya afya zao kujulikana.
“Taarifa za wachangiaji wetu ni siri. Zimehifadhiwa sehemu ambapo hakuna anayeruhusiwa kwenda kuziangalia bila kibali cha uongozi,” anasema Mariana.
Anasema kuna imani imejengeka kwa watumishi wa hospitali hiyo kuwa kwa sababu wanajuana, wakijitolea kuchangia damu taarifa za afya zao zitakuwa wazi huku akisema kuwa wanafanya jitihada za kuwaelimisha ili waachane na imani hiyo.
“Wengine wakija hapa wanadai wanataka kuchangia damu lakini hawataki taarifa zao ziandikwe popote. Kwa mfano mtu kama huyu akipatwa na tatizo bila kuwa na taarifa zake tutashindwa kumtambua katika data zetu, ni rahisi kumsaidia tukiwa na record yake,” anasema Mariana.