Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia
Hospitali ya Taifa Muhimbili imezindua mafunzo ya kimataifa ya awamu ya tatu ya upasuaji wa sikio na upandikizaji wa vifaa vya kusaidia kusikia (Cochreal Implant) kwa watu wanaozaliwa na changamoto ya kusikia.
Mafunzo hayo yanajumuisha washiriki kutoka Hospitali za ndani na nje ya Tanzania.
Akizungumaza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji, Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji MNH Dkt. Rachel Mhavile amesema kuwa huo ni muendelezo wa mfululizo wa mafunzo ya kimataifa ambayo hufanyika kila robo ya mwaka na kwa robo hii imehusisha madaktari bigwa wa upasuaji wa Masikio, Pua na Koo kutoka Hospitali za ndani ya nchi na nchi jirani ambazo ni Kenya, Uganda, Ethiopia, Rwanda na Ghana.
“Lengo kuu ni kuweza kuwajengea uwezo wataalamu hao ili waweze kufanya aina hii ya upasuaji kwa hospitali zao, hivyo kupanua wigo wa huduma za upasuaji wa sikio na upandikizaji wa vifaa vya kusaidia kusikia” amesema Dkt. Rachel.
Amesema katika mwaka wa fedha 2022/23 MNH imefanya upasuaji kwa kupandikiza vifaa vya kusaidia kusikia kwa kwa watu 11 na wiki hii watafanyiwa upasuaji huo watu sita.
Dkt. Rachel amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kusaidia wataalamu wanne kwenda kusoma masomo ya ubobezi nje ya nchi, na kwamba wengine saba wanategemea kwenda nchini Misri kujiendeleza kupitia programu ya “Samia Scholarship”