Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) itaanzisha huduma ya upandikizaji Ini ifikapo mwaka 2025 ikiwa ni mwendelezo wa azma ya Serikali kuhakikisha kwamba huduma za ubingwa bobezi zinapatikana nchini.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Prof. Mohamed Janabi wakati akifungua mafunzo ya awali ya uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya ini yaliyofanyika hospitalini katika kuelekea kwenye kongamano la wataalamu wa magonjwa Ini Barani Afrika (COLDA) linalotarajiwa kufanyika September 7 hadi 9 Jijini Dar es Salaam.
Prof. Janabi amesema katika kuelekea hatua ya upandikizaji Ini mafunzo mbalimbali ya wataalamu yanaendelea kutolewa kupitia Kituo cha kutoa mafunzo, uchunguzi na matibabu ya kibobezi ya Magonjwa ya Mfumo wa Chakula na Ini katika Ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Sahara Afrika kilichopo MNH kilichoanzishwa mwaka 2012 kwa ushirikiano na ufadhili wa Taasisi ya Munich Foundation ya Ujerumani, Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili hivyo kuifanya hospitali kuwa miongoni mwa vituo vichache vyenye hadhi ya namna hii Barani Afrika, vituo vingine vipo Rabat Morocco, Johannesburg Afrika ya Kusini na Cairo Misri.
Amesema kuwa kongamano la wataalamu wa magonjwa Ini Barani Afrika linalotarajiwa kufanyika Septemba 7 hadi 9 ni moja ya maandalizi ya kusaidia huduma za upandikizaji Ini kuanza kufanyika nchini kwa kuwa litatoa fursa ya wataalamu kujifunza, kujadili na kupanga mwendelezo wa mafunzo ya mara kwa mara ya ndani na nje ya nchi ambayo yatawajengea uwezo wataalamu wetu kuanzisha huduma ya upandikizaji Ini nchini
“Hii safari ni ndefu na nzito lakini tunaamini kwa msaada wa Serikali na wadau mbalimbali, tutafanikiwa kwani hadi sasa kituo kina uwezo wa kutoa huduma kwa wagonjwa waliofanyiwa huduma hiyo nje ya nchi wanaporejea hapa nyumbani tofauti na awali ambapo walilazimika kurudi nje ya nchi. Jambo hili linaenda sambamba na uboreshaji wa maabara za kiuchunguzi wa patholojia, uchunguzi wa damu, uchunguzi wa radiolojia na tiba radiolojia na uboreshaji wa vyumba vya wagonjwa mahututi” amesisitiza Prof. Janabi.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Huduma za Tiba MNH, ambaye pia ni Daktari Bingwa wa Mfumo wa Chakula na Ini Dkt. John Rwegasha amesema kuwa katika Kongamano hilo wataalamu watajifunza namna mbalimbali za kutibu magonjwa ya kuondoa mawe kwenye mfumo wa nyongo na ini bila kuhitaji upasuaji mkubwa na litahusisha wataalamu kutoka nchi za, Malawi, Gambia, Afrika ya Kusini na Nigeria.
Naye Dkt. Wongani Mzumara ambaye ni mshiriki kutoka nchi ya Malawi amesema Kongamano hilo ni fursa ya wataalamu wa Kiafrika kujifunza mbinu mpya za kutibu magonjwa wa mfumo wa chakula na ini na ameona fursa ya ushirikiano kati ya MNH na Malawi katika eneo hilo.