Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), leo imesaini mkataba wa makubaliano na Kiwanda cha Dawa cha Kairuki (KPTL) kwa lengo la kuboresha upatikanaji wa dawa Muhimbili Upanga na Mloganzila .
Mkataba huo umehusisha maeneo mawili , kuboresha upatikanaji wa dawa ambazo hazipatikani kwa urahisi kwenye soko ikiwemo zinazotumika katika upandikizaji wa viungo mbalimbali mwilini kama figo, kongosho pamoja na dawa zenye ujazo mdogo zinazotumika kwa watoto na wagonjwa wa saratani.
Eneo la pili la makubaliano ni kuwajengea uwezo wataalamu wa Muhimbili katika uzalishaji wa dawa na namna ya kuzitumia dawa zinazozalishwa na kiwanda hicho.
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Prof. Mohamed Janabi amesema hiyo ni hatua nzuri kuwepo kwa kiwanda cha dawa ambacho kinamilikiwa na wazawa na kukidhi viwango vinavyohitajika .
Amefafanua kuwa Muhimbili ni Hospitali ya Rufaa ya Kitaifa na kubwa kuliko zote nchini ina vitanda 2,150 ambapo Upanga kuna vitanda 1,550 na Mloganzila kuna vitanda takribani 600 hivyo inahudumia wagonjwa wengi.
Awali Mkuu wa Idara ya Famasi Muhimbili, Mfamasia Nelson Faustine amesema wameona umuhimu wa kuingia makubaliano ya pamoja ili kutatua baadhi ya changamoto na kuongeza ufanisi katika utendaji hususani kwa upande wa MNH kwani kiwanda hicho kitaweza kuzalisha bidhaa kutokana na mahitaji.
“Tuliwafuata kutokana kuwepo kwa changamoto ya upatikanaji wa baadhi ya dawa kwenye soko hususani zinazoendana na huduma za kibobezi, baadaye Kairuki wakatembelea Muhimbili na kufanya majadiliano , tulikubaliana baadhi ya bidhaa ambazo wanaweza kuzalisha kwa makubaliano baada ya kupokea oda kutoka Muhimbili’’ ameeleza Mfamasia Faustine.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda cha Dawa cha Kairuki Dkt. Muganyizi Kairuki amesema kiwanda hicho kimedhamiria kuzalisha bidhaa kulingana na mahitaji yaliyopo na kuhakikisha mkataba uliosainiwa unakua na tija kwa hospitali.