Kesho ni Siku ya Nyerere, siku inayoadhimisha miaka 16 tangu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere afariki mwaka 1999. Ni mwaka pia wa Uchaguzi Mkuu; mwaka unaotoa fursa kwa Watanzania kuchagua viongozi watakaotuongoza kwa miaka mitano ijayo kwenye ngazi za udiwani, uwakilishi, ubunge, na urais.

Kwenye mazingira ya sasa ya kisiasa, leo ni fursa nzuri ya kukumbuka maneno aliyoasa Mwalimu Nyerere aliposema: “Tupingane bila kupigana”, alipozungumzia siasa za ushindani zilizoletwa na mfumo wa siasa wa vyama vingi.

Kuna baadhi ya watu wanasema kuwa wamechoka kusikia watu wakirudia maneno aliyosema Mwalimu Nyerere. Kama ni maneno yanayofaa, mimi naona tusichoke kuyasikiliza kwa sababu hatutapungukiwa chochote zaidi ya kujikumbusha namna bora ya kuishi kwenye jamii inayozingatia haki, usawa, utu, na heshima kwa binadamu wenzetu. Sioni cha kuchosha kwenye ujumbe wa aina hii.

Yapo mengi mengine ya kujifunza kutoka kwake. Alikuwa kiongozi mwadilifu ambaye hakusahau kuwa kiongozi wa umma ana wajibu wakati wote wa kuwatumikia wale anaowaongoza, na siyo kujitumikia mwenyewe.

Aliamini juu ya usawa wa binadamu kwa dhati, na siyo kama kibwagizo cha kisiasa tu. Kwa mantiki hiyo hiyo, alisema binadamu wote wanastahili heshima. Muhimu kuliko yote na suala ambalo limeibua mjadala usioisha juu ya rasilimali za Taifa na jinsi gani zitanufaisha wote, alisema kuwa raia wote kwa pamoja wanapaswa kumiliki utajiri wa asili wa nchi yao ukiwa kama dhamana ya vizazi vyao.

Na aliamini kuwa serikali ni lazima iwe msimamizi wa njia muhimu za kukuza uchumi. Aliona serikali kuwa ina wajibu wa kuhakikisha ustawi wa raia wake wote bila kutoa mwanya kwa kikundi kimoja kidogo kuwa na hali nzuri dhidi ya kundi kubwa la raia waliobaki. Haya yote na mengine yaliainishwa kwenye Imani ya chama cha TANU alichokiongoza na kilicholeta Uhuru mwaka 1961.

Alisisitiza kuhusu umuhimu wa kilimo kwa nchi kwa sababu sehemu kubwa ya Watanzania wanaishi vijijini na kwa kuendeleza kilimo ndiyo aliamini ingekuwa njia ya haraka zaidi ya kuinua hali ya maisha ya watu walio wengi. Hakuhubiri tu kilimo, bali mwenyewe alishiriki kwenye kilimo akiwa rais. Hata baada ya kustaafu rasmi kwenye uongozi aliendelea kuwa mkulima wa mfano kijijini kwake Butiama.

Aliweka mkazo kuhakikisha kuwa serikali aliyoiongoza ilikuwa na viongozi ambao hawakukiuka maadili ya uongozi na ili kuhakikisha hilo, Azimio la Arusha la mwaka 1967 liliweka masharti kadhaa kwa viongozi wote ikiwa ni kuwapiga marufuku kushiriki kwenye shughuli za biashara wakati wakiwa bado wanashika nyadhifa za uongozi.

Anayesema amechoka kumsikia Mwalimu Nyerere achunguze jinsi baada ya masharti haya kulegezwa na awamu za serikali zilizofuata na viongozi kuruhusiwa kushiriki kwenye biashara jinsi hali hiyo ilivyoambatana na kufumuka kwa tuhuma dhidi ya viongozi kuhusu vitendo vya kifisadi, na kashfa mbalimbali zilizohusisha kupotea kwa pesa nyingi za umma.

Kwenye upande wa elimu, aliamini kuwa ni wajibu wa serikali kugharimia elimu ili kuhakikisha kuwa malengo ya usawa, haki, na elimu ya msingi na ile ya watu wazima kwa wote yanafikiwa na Watanzania wengi.

Kwenye miaka ya 1970, karibia robo ya bajeti ya serikali ilitengewa sekta ya elimu. Tofauti na elimu tuliyorithi kutoka kwa Waingereza ambayo msingi wake ulikuwa kuandaa watumishi wa kutumikia watawala, yeye alisisitiza mitaala ya elimu iakisi mahitaji ya jamii ya Watanzania ili kuwaandaa wahitimu wapate uwezo na ujuzi utakaowawezesha kukabiliana na maisha kwenye maeneo watakayoishi.

Alichukia ubaguzi wa kila aina, kuanzia wa dini, ukabila, rangi, na wa jinsi na kutukumbusha athari za ubaguzi katika kudhoofisha umoja wa kitaifa.

Leo hii wale ambao hawakumsikia moja kwa moja wanapata fursa ya kusikia chuki yake dhidi ya ubaguzi kwenye hotuba zake zinazorudiwa mara kwa mara kwenye baadhi ya vyombo vyetu vya habari. Lakini siyo wote wanaosikia au kuamini juu ya umuhimu wa aliyoyasema. Leo tunaanza kusahau athari za ubaguzi na baadhi yetu tunajaribu kushawishi wapigakura watuchague kwa kuchochea ubaguzi wa aina moja au nyingine.

Alichukia ubaguzi kwa kiasi kwamba hata katika kupinga ubaguzi wa rangi Afrika Kusini, Rhodesia (sasa Zimbabwe), na kwenye makoloni ya Ureno ambayo yalikuwa hayajapata uhuru akiwa madarakani, alitukumbusha kuwa Tanzania na nchi wanachama za Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) zilipinga watawala wa nchi hizo si kwa sababu ya rangi ya ngozi yao, bali kwa sababu walisimamia sera ambazo ziliwabagua wananchi wa nchi zao kwa misingi ya rangi.

Leo hii tumemsikia Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe akikumbusha Waafrika kutosahau mchango mkubwa wa baadhi ya viongozi wa Afrika kuunga mkono jitihada za kuleta uhuru, haki, na usawa, kwenye nchi zilizokuwa zinapambana dhidi ya tawala hizi za kibaguzi. Hao viongozi ni pamoja na Mwalimu Nyerere, Rais Kenneth Kaunda wa Zambia, na Sir Seretse Khama wa Botswana.

Akikabidhi uenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi Zilizo Kusini mwa Afrika (SADC) kwa Rais Ian Khama wa Botswana mwezi Agosti, Rais Mugabe alisema: “Tuwakumbuke wale waliotupatia urithi huu. Inaweza kuwa kwa njia ya kuanzishwa mfuko kwa ajili ya kumbukumbu yao.”

Huu ni mfano wa kuigwa. Watanzania hatuna budi kuenzi yale yanayojenga umoja, na kupiga vita yale yanayoleta utengano. Na tuwapuuze waliochoka kusikia ujumbe huu.